Search in This Blog

ANANAJISI WATOTO NA KUWATOBOA MACHO

http://www.habarileo.co.tz/images/polisi.jpg
MTUHUMIWA sugu wa matukio ya unajisi na vitendo vya kikatili dhidi ya watoto, anashikiliwa Polisi mkoani hapa, baada ya kukurupushwa katika jaribio la kutaka kumnajisi na kumtoboa macho mwanafunzi mwenye umri wa miaka minane.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evarist Mangala alisema ofisini kwake jana, kuwa mtuhumiwa huyo, Jacob Mayani (28), ameshanajisi watoto wanne wa umri wa kati ya miaka minane hadi 10 na kuwatoboa macho.

‘’Mayani anatuhumiwa kunajisi na kufanyia ukatili wa kutoboa macho watoto wanne wenye umri wa kati ya miaka nane hadi 10, kwa lengo la kutaka kuvuruga ushahidi ili wasimtambue,’’ alidai Kamanda Mangala.

Kwa mujibu wa madai ya Kamanda Mangala, mtuhumiwa alikamatwa mwishoni mwa wiki kwenye shamba la mahindi katika mtaa wa Mwasele manispaa ya Shinyanga, baada ya jaribio lake la kutaka kumnajisi mtoto mmoja kushindwa.

Inadaiwa jaribio hilo lilishindwa baada ya mtoto aliyekusudiwa kunajisiwa, kufanikiwa kuponyoka mikononi mwa mtuhumiwa na kutimua mbio huku akipiga kelele za kuomba msaada. Kutokana na kelele hizo, Kamanda Mangala alisema wasamaria wema walijitokeza wakamkamata mtuhumiwa na kumfikisha kituo cha Polisi.

Watoto wanne Kamanda Mangala alisema mtuhumiwa alifanya unyama huo katika muda usiozidi mwezi mmoja katika matukio na maeneo tofauti ya Kitangili, Ndembezi na Ndala.

Alisema watoto wawili kati yao, walilazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando na mmoja hospitali ya Mkoa wa Shinyanga. Kwa mujibu wa madai hayo, madaktari walitoa taarifa Polisi kwamba jicho la mmoja wa watoto hao limeharibika baada ya kutobolewa.

Utambuzi, hofu Kamanda Mangala alisema baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo jana, watoto wawili waliopata kufanyiwa unyama huo, walifika kwenye kituo cha Polisi mjini hapa na kumtambua mtuhumiwa kwenye gwaride la utambulisho.

Alisema mtuhumiwa ni mkazi wa mshikamano katika manispaa ya Shinyanga na hujishughulisha na kazi ya kutoa huduma ya usafiri wa baiskeli, maarufu kwa jina la bodaboda na uuzaji wa urembo.

Inadaiwa mtuhumiwa alikuwa akirubuni watoto hao kwa kuwapa mahindi mabichi ya kuchoma na mavazi ya kubana au vipodozi vya urembo.

Kamanda wa Polisi alisema kutokana na tabia na mwenendo wa mtuhumiwa, inahofiwa kuna watoto wengi waliofanyiwa vitendo hivyo, lakini kwa sababu moja au nyingine wazazi au watoto hawajaripoti matukio hayo.

Kamanda huyo alitoa mwito kwa wazazi na walezi, kutoa taarifa kama watoto wao walinajisiwa na mtuhumiwa. Mtuhumiwa anashikiliwa na Polisi na baada ya uchunguzi kukamilika, atafikishwa mahakamani kujibu mashitaka yanayomkabili.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger