Pichani
juu ni bunduki aina ya Shortgun Mossberg ikiwa na risasi sita ambayo
ilikutwa kwenye begi la dereva huyo wa Boda boda aliyekamatwa na polisi
tarehe 28.04.2013
Jeshi la
Polisi Mkoani hapa limemkamata mtu mmoja aitwaye Ally Rashid Salimu (23)
Mwendesha pikipiki za abiria maarufu kwa jina la “Boda Boda” mkazi wa
kata ya Sombetini jijini hapa akiwa na bunduki aina ya shortgun Mossberg
yenye namba T292166 ikiwa na risasi sita.Akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake leo saa 5:30 asubuhi Kamanda wa Polisi
Mkoa wa Arusha, Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Liberatus Sabas
alisema kwamba, tukio hilo lilitokea juzi tarehe 28.04.2013 muda wa saa
3:00 asubuhi katika maeneo ya Shamsi yaliyopo jijini hapa.
Alisema
siku ya tukio dereva huyo wa pikipiki akiwa katika eneo hilo alikuwa
anaendesha pikipiki aina ya Skymark yenye namba za usajili T. 615 BZL
huku akiwa amebeba begi lilionekana kutuna sana, ndipo askari waliokuwa
doria katika eneo hilo walimtilia shaka na kisha kumfuatilia na
kufanikiwa kumsimamisha.
“Mara
baada ya kumsimamisha askari hao walipekua begi hilo na kukuta silaha
hiyo ikiwa na risasi sita na kisha kumfikisha mtuhumiwa huyo katika
kituo kikuu cha polisi cha hapa Arusha mjini”. Alifafanua Kamanda Sabas.
Kamanda Sabas alisema upelelezi juu ya tukio hilo bado unaendelea na mtuhumiwa atafikishwa mahakamani pindi utakapokamilika.
Tukio
hilo la ukamataji wa bunduki hiyo limekuja wiki tatu tu baada ya jeshi
hilo kukamata bastola moja pamoja na risasi 41 kutoka kwa watuhumiwa
waliokuwa wanahusishwa na matukio ya kumjeruhi Sister Mary Shobana na
kisha kumnyang’anya fedha taslimu Tsh 30,000,000/= (Milioni thelathini)
eneo la Notre Dame Njiro lililopo jijini hapa, fedha ambazo alitoka
kuchukua benki ya Exim tawi la Shoprite.