SAKATA la biashara ya dawa za kulevya limeibuka upya, baada ya Mbunge wa
Mwibara, Kangi Lugola (CCM), kusema ataanika majina ya vigogo
wanaofanya biashara hiyo haramu.
Akizungumza bungeni juzi, Lugola
alisema anakusudia kupeleka bungeni majina ya viongozi wa taasisi za
Serikali wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya kabla ya
kumalizika kwa mkutano huu wa Bunge.
Mbunge huyo pia aliwatuhumu viongozi hao wakiwemo mawaziri, kwa kuhusika na vitendo vya rushwa ama mihadarati.
Katika
Bunge la tisa chini ya Spika Samuel Sitta, aliyekuwa Mbunge wa Viti
Maalum, marehemu Amina Chifupa (CCM), aliwahi kutangaza kuwa yupo tayari
kutaja hadharani watu wanaofanya biashara ya dawa za kulevya.
Amina
ambaye kwa sasa ni marehemu, katika mchango wake bungeni alinukuliwa
akisema. “Nitawataja hadharani kwa majina, hata kama ni mume wangu
anauza dawa za kulevya nitasimama na kumtaja bila kuogopa.” Mohamed
Mpitanjia aliyekuwa mume wake naye ni marehemu.
Katika kile
kinachoonekana ni kufuata nyayo hizo, Lugola alisema kitendo cha
viongozi wa juu serikalini kushindwa kuwataja na kuwachukulia hatua
wafanyabishara hao licha ya kuwajua, ni wazi kuwa nao wanahusika.
Lugola
alitoa kauli hiyo juzi, wakati akichangia Hotuba ya Makadirio ya
Matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, inayoshughulikia Tawala za Mikoa na
Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
Katika mjadala huo, Lugola aliweka
wazi msimamo wake wa kutounga mkono bajeti hiyo ya waziri mkuu, kutokana
na sababu mbili, rushwa na dawa za kulevya.
“Ninawaomba wabunge
wenzangu, kabla ya kumaliza mkutano huu wa Bunge nitakuja na orodha ya
viongozi wa taasisi za Serikali, wanaojihusisha na madawa ya kulevya
naomba mniunge mkono,” alisema.
Hata hivyo, Lugola alisema
Kamishina wa Tume ya Kudhibiti Dawa za Kulevya, Christopher Shekiondo,
anapaswa kuwajibishwa kwani ameshindwa kazi.
Lugola alisema
biashara hiyo imezongwa na rushwa na kwamba hiyo ndiyo sababu
inayomfanya Shekiondo ashindwe kuwakamata watu hao, licha ya kuwafahamu
kwa majina.
“Kwa nini Shekiondo anatuambia anajua majina ya watu
wanaofanya biashara ya kulevya, lakini hatutajii eti kwa kuwa
wanashindwa jinsi ya kuwakamata.
“Hakuna cha kushindwa hapa kama
sio rushwa nini, awajibishwe kama anashindwa kuwakamata, kwanini kama
kuwakamata ni tatizo wasiombe msaada hata kwa FBI kama walivyoletwa juzi
baada ya mauaji ya Padri,” alisema.
Alisema yeye hakubaliani na msemo wa Serikali wa vita dhidi ya dawa za kulenya, isipokuwa vita anayoinoa yeye ni vita ya rushwa.
“Kama
viongozi hawa wameshindwa kuwakamata wahusika wanaosema wanawajua, basi
wanahusika kuchukua rushwa au la sivyo, hata mawaziri na wenyewe
wanahusika na biashara hiyo.
“Ninyi wabunge kama mnataka pesa zimiminike kwenye halmashauri zetu, tupambane na rushwa na dawa za kulevya,’ alisema.
Lugola
alisema, Serikali haiwezi kupambana na rushwa bila kuwekeza fedha na
kwamba isiwalaumu polisi kwa vitendo vya rushwa badala yake wawaongezee
mishahara.
“Wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA), waliongezewa
mishahara ili wasichukue rushwa kwa nini Serikali inapata kigugumizi
kuongeza mishahara ya polisi?
“Mimi sitaunga mkono hoja hii kama
Serikali haitaanzisha mfuko maalumu katika Jeshi la Polisi ili kuboresha
maslahi yao,” alisema.
Mbunge huyo pia alilalamikia kitengo cha maafa kwa kudai kuwa kitengo hicho ni ulaji wa Serikali.
Alisema
Serikali inasubiri wananchi wa jimbo lake wakumbwe na njaa ndipo
wajenge miundombinu ya kilimo cha umwagiliaji kutoka Ziwa Victoria hadi
Mwibara.
Mazishi ya vigogo yatengewa Sh bil. 1
Mbunge
aliishangaa Serikali kutenga Sh bilioni 1 katika bajeti ya ofisi hiyo,
kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa kitaifa, huku huduma za wananchi
zikizorota.
“Na hii Sh bilioni 1 iliyotengwa kwa ajili ya
mazishi ya viongozi wa kitaifa, ni wizi mtupu, wabunge wenzangu
tusukubaliane na maneno matamu ya bajeti hii,” alisema.
Kwa
upande wake, Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Kessy (CCM) alisema wabunge
wanapoteza muda kujadili bajeti ambayo sehemu kubwa imejaa ahadi za
wafadhili.
“Hapa tunapiga kelele kupitisha bajeti tukienda kwenye
halmashauri fedha hakuna, wafadhili hawajaleta, kwani tulidai uhuru
kutegemea fedha za wafadhili?” Alihoji.
Aidha, alizitaka halmashauri zisiadhibiwe kwa kutopelekewa fedha, kutokana na ubadhirifu unaofanywa na watumishi wachache.
Alisema
kuziadhibu halmashauri ni kuwaonea wananchi wasio na hatia kwa kosa la
watendaji wachache waliopelekwa katika halmashauri na Serikali yenyewe.
Kessy
pia alitaka Serikali kujenga uwanja wa ndege katika jimbo lake, ili
kumaliza tatizo la maji na kujenga barabara zilizopo kandokando ya Ziwa
Tanganyika kwa kuwa hali zake ni mbaya.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment