Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa
WANACHUO 435 wa mwaka wa pili katika Chuo cha Ualimu Bunda, mkoani
Mara, juzi waligoma kula chakula cha jioni kutokana na madai mbalimbali,
ikiwa ni pamoja na kubadilishiwa ratiba ya chakula kwa kutopikiwa wali
kama ratiba ilivyokuwa inaonesha na badala yake wakapikiwa ugali.
Kufuatia hali hiyo, jana polisi wakiwa wamejiandaa kwa mabomu ya
machozi na silaha mbalimbali walifika chuoni hapo kwa ajili ya
kuimarisha ulinzi.
Aidha, Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Bunda, chini ya
uenyekiti wa Mkuu wa Wilaya, Joshua Mirumbe aliyewakilishwa na Katibu
Tawala wa wilaya hiyo, Dominicus Lusasi ilifika chuoni hapo na kukutana
na wanachuo hao ambao ni wa mwaka wa pili.
Katika kikao hicho iliamriwa kuwa kuanzia sasa ratiba ya chakula
ifuatwe na wanachuo hao siku zinazoonesha ratiba ya kula wali wapikiwe
chakula hicho.
Wakizungumza katika kikao hicho, waliyataja madai mengine kuwa ni
kutorudishiwa kwa pesa zao walizotumia kununua vifaa vya kufundishia
wakati wa mafunzo kwa vitendo.
Walisema kuwa wakati wa mafunzo kwa vitendo serikali ilikuwa
haijaleta fedha za kununua vifaa vya kufundishia, hali iliyowalazimu
kila mwanachuo kutoa fedha zake na kununua vifaa hivyo, ili kazi hiyo
iende vyema.
“Tulitumia fedha zetu kununua vifaa vya kufundishia ili zoezi hilo
liweze kwenda vizuri, lakini sasa tunashangaa hawataki kuturudishia,”
alisema mwanachuo mmoja.
Walisema kuwa sasa wanautaka uongozi wa chuo hicho uwalipe fedha hizo
kwani tayari wizara ilikwishazituma na kwamba kila mwanafunzi anatakiwa
alipwe kiasi cha Sh 48,000.
Waliongeza kuwa, madai mengine ni pamoja na michango mbalimbali
wanayodaiwa kuchangishwa, licha ya kuwepo waraka wa serikali wa kuzuia
michango hiyo na kwamba sasa wanataka muafaka ili waweze kupewa fedha
zao.
Alisema wamekuwa wakichangishwa Sh 5,000 za mahafali, lakini chakula
wanachokula siku hiyo ni cha shule, wanafanyishwa kazi ya ulinzi,
upasuaji kuni na mwaka jana pesa za chakula wakati wa mafunzo kwa
vitendo zilikuwa Sh 50,000 kwa kila mwanafunzi lakini walipatiwa Sh
14,500.
Kwa upande wake mkuu wa chuo hicho Josephat Rweyemamu alikanusha
madai yote ya wanachuo hao na kusema kuwa fedha hizo za vifaa vya
kufundishia wizara ilitoa agizo kuwa zinunue vifaa vya kufundishia na
sio kuwapatia pesa taslimu wanachuo hao.
Hata hivyo, Katibu Tawala alimwagiza mkuu wa chuo hicho kuiandikia
barua wizara kuhusu madai ya wanachuo hao kuhusu fedha zao walizonunua
vifaa vya kufundishia ili waweze kurejeshewa.
No comments:
Post a Comment