Jeshi la Magereza limesema linakabiliwa na msongamano
mkubwa wa wafungwa katika magereza yake na kwamba limeanza kupanga
mikakati ya kukabiliana na tatizo hilo.
Hayo yalisemwa jana na Kamishina Jenerali wake, John Casmir Minja
wakati akizungumza na waandishi wa habari katika sherehe za kuwatunuku
nishani maafisa na askari vyeo mbalimbali wa jeshi hilo zilizofanyika
kwenye viwanja vya Magereza mkoani Shinyanga.
“Kweli kumekuwapo na msongamano katika magereza yote nchini kutokana na
wafungwa kuwa wengi ikiwa kwa sasa idadi ya wafungwa 35,000 badala ya
29,552 hali ambayo imekuwa ni tatizo kubwa” alisema.
Katika hafla hiyo askari 43 wametunukiwa nishani mbalimbali kwa maafisa
na askari wa vyeo tofauti tofauti wakiwamo askari waliotumikia
jeshi hilo kwa muda mrefu.
Nishani hizo zilikuwa katika makundi manne maalumu ambayo ni nishani ya
utumishi uliotukuka, utumishi wa muda mrefu Tanzania, utumishi wa muda
mrefu na tabia njema na nishani ya Mwenge wa Uhuru daraja la nne.
Minja alisema hicho ni kitendo cha historia kwake cha kuwatunuku nishani
hizo kwani lilikuwa ni jukumu la Rais Jakaya Kikwete kuwavisha siku ya
sherehe za Muungano lakini aliamua kumpatia jukumu hilo.
Mmoja wa maafisa hao ambaye ni Mkuu wa Magereza kutoka mkoani Mwanza,
R. Mollel alitunukiwa nishani ya utumishi uliotukuka Tanzania na kueleza
kuwa nishani hiyo ni furaha kwake kwa kulitumikia taifa na kuwa
mzalendo ndani ya nchi yake ya Tanzania.
Maafisa na askari hao kutoka mikoa ya Mwanza, Mara, Kagera, Shinyanga, Geita na Simiyu nao walitunukiwa nishani hizo.