HALI
ya mambo huenda ikavurugika tena mkoani Mtwara baada ya kuwepo kwa
taarifa za maandalizi ya mgomo na maandamano ya kudai kunufaika na gesi,
Tanzania Daima la leo limeandika
Mwishoni
mwa mwaka jana wananchi wa Mtwara walifanya maandamano kupinga ujenzi
wa bomba la gesi kutoka Mtwara kwenda Dar es Salaam uliopangwa
kutekelezwa na serikali.
Februari
mwaka huu wananchi hao waliamua kufanya maandamano mengine
yaliyoambatana na vurugu ikiwemo kuchoma nyumba za viongozi wa CCM.
Baada
ya kutokea matukio hayo, viongozi mbalimbali wa serikali, akiwemo
Waziri Mkuu, walikwenda kuzungumza na wananchi hao jinsi ambavyo
wangelinufaika na gesi hiyo.
Miongoni
mwa ahadi walizopewa ni kuboreshwa kwa bandari ya Mtwara, kujengwa kwa
kiwanda cha saruji na uwanja wa ndege wa kisasa ambavyo vitachangia
kukua kwa uchumi wa mkoa huo.
Tanzania
Daima limedokezwa kuwa baadhi ya watu wamesambaza vipeperushi mitaani
kuwahamasisha wananchi kujiandaa kusikiliza na kuangalia hotuba ya
Wizara ya Nishati na Madini.
Kwa
mujibu wa baadhi ya wananchi, vipeperushi hivyo vinawataka wasifanye
shughuli yoyote siku bajeti hiyo itakaposomwa ili wajue hatima ya gesi
iliyoko mkoani mwao.
“Tuliambiwa
leo bajeti ya Nishati na Madini itasomwa lakini baadaye tunaambiwa
itasomwa wiki ijayo…hapa watu wamejipanga kuifuatilia,” alisema Nchiman
Joseph.
Moja ya vipeperushi kilisomeka: “Zinduka kusini, wananchi kwa pamoja. JK ameamua kutumia nguvu kwenye suala la gesi.
“Kwa
pamoja Mei 17, 2013 saa tano asubuhi tukusanyike kwenye vituo vya
runinga ili kusikiliza bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini; tutambue
vema sakata la gesi, sambamba na hilo tusitishe huduma zote za jamii
ikiwemo bodaboda, teksi, bajaji na magari ya abiria-zinduka Mtanzania!”
Tanzania
Daima imedokezwa kuwa Kamanda wa Polisi mkoa wa Mtwara, Linus Sinzumwa,
ameonekana katika kituo cha redio kiitwacho Pride FM kuwatahadharisha
wananchi kuhusu vipeperushi hivyo.
Kamanda
huyo aliwaambia wananchi wasihofu juu ya usalama wao kwa kuwa polisi
imejipanga kuhakikisha vurugu zilizotokea huko nyuma hazitokei tena.
Tanzania
Daima iliwasiliana na Kamanda Sinzumwa ambaye alikiri kuna taarifa za
vipeperushi hivyo na kuwataka wananchi wavipuuzie.
“Ni
kweli vipeperushi vipo ila hali ni shwari…, nyie mnataka kukuza tu,
nimeshatoa tahadhari na tutafanya udhibiti mkubwa sana,” alisema.
Nyumba za kulala wageni
Chanzo
chetu cha taarifa kimedokeza kuwa nyumba ya kulala wageni zilikuwa na
wegeni wengi ambao wengine wakisadikiwa ni askari kutoka makao makuu ya
jeshi la polisi.
Mmoja
wa wananchi alizungumza na gazeti hili kwa simu alisema: “sisi wananchi
wa Mtwara tumekuwa gizani kwa kipindi kirefu bila kujua lengo la
serikali katika suala la gesi ambayo itachimbwa huku tumekubaliana na
masuala ambayo tuliyataka yatolewe ufafanuzi ambapo serikali haikufanya
hivyo.”
Aliongeza
kuwa wananchi wanataka kuona mambo waliyokubaliana na serikali katika
mikutano mbalimbali yanatekelezwa kwa kuwekwa katika bajeti hiyo.
“Sisi
hatuna ugomvi na serikali; tunachotaka ni kuona utekelezaji wa masuala
tuliyokubaliana yanakuwepo katika bajeti ambayo kwetu yatatuwezesha
kuendelea kiuchumi na sio kuonekana wazalishaji lakini wananufaika
wengine,” alisema Mpendela.
Baadhi
ya wananchi hao walilalamika kuwa suala la gesi linapelekwa kisiasa
huku wananchi wakiwa njia panda bila kujua ni maslahi gani
watakayonufaika nayo.
Shura ya Maimamu
Viongozi wa Shura ya Maimamu ni miongoni watu waliofanya mazungumzo na kamanda wa polisi mkoa wa Mtwara juu ya tisho la vurugu.
“Sisi
tumefanya vikao sio leo tangu juzi, kamanda wa polisi alituita ingawa
yeye bado ni mgeni alitaka tujadili suala la amani ya mji wa Mtwara na
dhana ya utii wa sheria bila shuruti katika kikao hicho tuliunda kamati
ya watu 10, Wakristo watano na Waislamu watano.
“Leo
alituita ili tujadili ni nani anahusika na vipeperushi hivi. Kwa hiyo
tumetoa tamko kuwa kesho wananchi waendelee na shughuli zao kwani siku
ya kesho sio ya kujadili Bajeti ya Nishati na Madini, tumemkabidhi
kamanda wa polisi wa mkoa aende kwenye vyombo vya habari kuisoma ili
awaarifu wananchi,” alisema mmoja wa viongozi wa taasisi hiyo.
Kiongozi huyo alitaka elimu iendelee kutolewa kwa wananchi ili mtoaji wa vipeperushi hivyo ajulikane.
“Hatutaki
vurugu zitokee hii leo,…. maana wengine wanaweza wakaleta dhana ya
udini ikaonekana Waislamu wametengeneza au Wakristo wanatumia mwanya huo
kuharibu Ijumaa.
“Sisi Waislamu na Wakristo tulio katika tume hiyo tunawaasa wananchi wasifanye hivyo.