Search in This Blog

MASTAA WALIOKUFA NA SIRI ZA WAPENZI WAO.


UHUSIANO wa kimapenzi kwa mastaa wengi Bongo huwa ni wa siri, mara nyingi hata inapotokea staa husika amefariki, huacha siri nzito kwa familia yake.
Wengi wao wanapofariki dunia, ndipo wanapoibuka wasichana na kudai kuwa walikuwa wapenzi wa marehemu jambo ambalo linawaacha mashabiki katika hali ya ‘sintofahamu’ kama madai yao yanakuwa na ukweli au la!
Tabia ya kutoweka wazi uhusiano wa mapenzi imekuwa kama staili ya mastaa wengi Bongo. Wengi huhofia kuanika uhusiano wao kwa kuwa wanakua na wapenzi wengi.
Wapo pia ambao huwaficha wapenzi wao kutokana na maadili ya Mtanzania, wanaamua kukaa kimya hadi pale utakapofikia muda wa kufanya mipango ya ya ndoa, ikitokea bahati mbaya mmoja wao amefariki kabla, ndipo wanapoacha siri kubwa ya mapenzi yao.
Amani linakuletea orodha ya baadhi ya mastaa ambao wamefariki katika miaka tofauti iliyopita na kuacha siri nzito za mapenzi.

STEVEN KANUMBA
Alifariki dunia Aprili 7, 2012 akiwa na mpenzi wake, Elizabeth Michael ’Lulu’ ambaye watu wengi hawakuwa wakifahamu uhusiano huo kabla.
Mashabiki wengi pamoja na familia yake walibaki na maswali mengi, usiri ulikuwa mkubwa na hakukuwa na mtu aliyefahamu mazungumzo ya marehemu na Lulu walipokuwa chumbani.
Kama hiyo haitoshi, baadaye walijitokeza wasichana kadhaa na kudai kuwa wamezaa na Kanumba ingawa familia yake iliwakataa kwa sababu marehemu hakuwahi kuwatambulisha kama ana mchumba wala mtoto.

HUSSEIN MKIETI
‘SHARO MILIONEA’
Alifariki dunia Novemba 26,2012 kwa ajali ya gari, Muheza-Tanga naye pia alikufa na siri ya mpenzi wake kwani hakujulikana hadi leo ingawa kuna Mtangazaji wa Redio Chemchem ya Mjini Sumbawanga, Marry Lucas aliibuka na kudai alikuwa na mimba ya marehemu.
Hadi sasa, hakuna mtu ambaye amekitegua kitendawili cha mtangazaji huyo ambaye alidai kuwa na mimba ya marehemu.

ALBERT MANGWEHA ‘NGWEA’
Huyu yeye kifo chake ndiyo hakina muda mrefu. Alifariki dunia Mei 28, mwaka huu huko Afrika Kusini.
Haikujulikana mara moja kuwa mpenzi wake ni nani baadhi ya marafiki zake walikuwa wakimtambua mzungu, Michelle lakini wengine wakamtaja Siwema ambaye ana ujauzito wa Emmanuel Elibarik ‘Nay wa Mitego’.
Haikuishia hapo, baadaye alijitokeza mwanamke aishiye mkoani Dodoma na kusema kuwa alizaa na Ngwea mtoto wa kike aitwaye Paulina. Lakini familia iliahidi kumsikiliza baada ya mazishi.

MARIAMU KHAMIS ‘PAKA MAPEPE’
Alikuwa Mwimbaji Taarab wa Bendi ya Tanzania One Theatre (TOT), alifariki dunia Novemba 13, 2012 katika Hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na matatizo ya uzazi, siku ya msiba baadhi ya watu walikuwa wakisema kuwa kuna mfanyabiashara mmoja maarufu Bongo ndiye aliyempa mimba hiyo huku wengine wakisema ni ya mumewe, Haji Kijungu aliyefunga naye ndoa.
Hata hivyo, Kijungu naye alizungumzia pigo alilolipata huku akionesha kuumizwa sana na kifo cha mkewe huyo ambaye tayari alizaa naye mtoto mmoja aitwaye Tariq.

MASTAA WENGINE
Wapo mastaa wengi waliokufa na siri ya mapenzi akiwemo Vivian na Complex ambapo mashabiki wengi walikuja kugundua kuwa wawili hao walikuwa na mipango ya kuoana baada ya mauti kuwakuta wakiwa safarini, mbaya zaidi safari hiyo ndiyo ilikuwa ya kwenda kutambulishana kwa wazazi.
Marehemu, Steve 2K, Faza Nelly na wengine wengi waliotangulia mbele za haki lakini suala la uhusiano wao wa kimapenzi lilikuwa siri na mambo mengi yaliibuka mara baada ya mastaa hao kufariki dunia.

NINI CHA KUFANYA?
Kila nafsi itaonja mauti ni vyema pia tukajiandaa na maisha ya kifo. Wakati umefika sasa wasanii kuweka wazi uhusiano wao hata kama siyo kwa mashabiki wote, japo hata ndugu wa karibu ambao wanamzunguka ili kuondoa mkanganyiko kwa mashabiki.
Haina haja ya kuogopa au kuishi kwa wiziwizi, maisha ya siku hizi yanapaswa kuwa wazi. Unapoweka maisha yako wazi inarahisisha kuepusha ugomvi usiokuwa wa lazima miongoni mwa warithi wa mali zako.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger