MBUNGE wa Nkasi Kaskazini, Ali Keissy (CCM), amesema kuwa bila
Watanzania kuwa makini na sheria mpya ya ndoa ijayo, huenda nchi ikapata
rais, wabunge na madiwani wanaojihusisha na mapenzi ya jinsia moja
(mashoga).
Keissy alitoa kauli hiyo wakati akichangia mada katika mkutano wa siku
tatu wa Chama cha Wabunge cha Kupambana na Ukimwi (TAPAC) uliomalizika
jana mjini Dodoma.
Mbunge huyo aliwaomba viongozi wa dini kukemea kwa nguvu vitendo hivyo,
pia alipinga hatua ya wazazi kuwapeleka watoto wao wadogo shule za bweni
akidai kuwa huko ndiko wanakojifunza vitendo hivyo.
“Mnashindwa kulea watoto wenu, mnawapeleka shule za bweni wakiwa na
miaka mitatu ili walelewe kizungu. Huko watapakwa mafuta ya KY na
wataingiliwa,” alisema.
Keissy alitolea mfano mkutano mmoja uliofanyika jijini Dar es Salaam
kuwa uliwashirikisha mashoga 400, jambo alilodai ni ishara kwamba
wanaojihusisha na vitendo hivyo wanaongezeka, na hivyo kuitaka serikali
kuwapiga marufuku.
Hata hivyo, baada ya mbunge huyo kuhitimisha mchango wake, mmoja wa
vijana wanaojihusisha na mapenzi hayo ya jinsia moja, Abdilah Ally
ambaye alikuwa amealikwa na TAPAC, alitetea kuwa jamii inapaswa kukubali
kwamba matendo hayo yanafanyika.
“Tunatambua kuwa sheria haziruhusu vitendo hivi, lakini vipo na
vinafanyika na tunapata maambukizi kwa kiwango kikubwa. Tunachokitaka
tusinyanyapaliwe na jamii, bali tupewe huduma ya afya ya kujikinga na
maambukizi.
“Mathalani mimi hapa nina wapenzi wanaume watatu ambao nashiriki nao
mapenzi, sasa kama nimeathirika ina maana wote wale nao wamethirika,”
alisema.
Akifunga mkutano huo, Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy
Mwalimu, aliwasihi wanasiasa wasiwabague makundi ya watu wanaojihusisha
na vitendo vya ushoga, usagaji na matumizi ya dawa za kulevya.
Alisema kuwa makundi hayo yanakabiliwa na janga la maambukizi makubwa ya
virusi vya ukimwi, hivyo wanahitaji kusaidiwa kuondoka katika makundi
hayo badala ya kuwahukumu.
Mwalimu alifafanua kuwa miongoni mwa washiriki wa mkutano huo kutoka
katika makundi hayo, alikuwa mtumiaji wa dawa za kulevya, lakini baada
ya kupata msaada wa kiafya ameachana na vitendo hivyo na sasa anaendelea
vizuri chini ya uangalizi.
Mkutano huo uliratibiwa na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS),
kama wadau wakuu waliotoa mada mbalimbali kuhusu jinsi wanavyopambana
kupunguza maambukizi mapya ya virusi vya ukimwi.
Katika hilo, Mwalimu alisema kuwa serikali dhamira yake ni kufikia
maambukizi asilimia sifuri, hasa kwa kutoa msukumo mkubwa kwa makundi ya
wanawake, vijana na watoto ambayo yana maambukizi zaidi.
Mbunge wa Chambani visiwani Zanzibar, Yusuf Salam Hussein (CUF), alisema
kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imefanikiwa kupunguza maambukizi
hayo kwa wanandoa kutokana na sheria ya kuwataka wapime ukimwi kabla ya
kufunga ndoa.
“Zanzibar mtu hawezi kufunga ndoa kanisani kwa padri wala msikitini kwa sheikh ikiwa hana kibali cha sheha,” alisema.