Search in This Blog

TAIFA STARS KUUMANA NA MOROCCO LEO

a7 5e4f7

Taifa Stars yetu inaingia uwanjani kupambana na Morocco. Ni ‘ Mama’ wa mechi zote.  
Ni mechi muhimu sana kuwahi kuchezwa na Stars kuwania tiketi ya kucheza mashindano makubwa kabisa ya soka hapa duniani; Fainali za Kombe la Dunia.
Matokeo ya mechi ya usiku huu kwa kiasi kikubwa sana yataamua hatma ya safari ya Stars yetu kwenda Brazil.

Tukishinda ina maana kubwa hata kisaikolojia kwa wachezaji wetu na wapinzani wetu pia. Kwetu kutakuwa na momentum ya ushindi kwa wachezaji wetu watakayokwenda nayo kwenye mechi mbili zilizobaki; moja nyumbani na nyingine ugenini.

Na Ivory Coast watakuwa na presha kubwa sana. Itatusaidia zaidi sisi. Tukifungwa usiku huu , basi, mbele ya njia yetu ya kwenda Brazil kutakuwa kumejitokeza mlima mkubwa sana na mgumu kuupanda. Sare pia itatuweka mashakani. Kinachotakiwa ni kushinda tu.

Niliwaona Morocco walipokuwa Dar. Stars wasibweteke na ushindi ule dhidi ya Morocco wakadhani kuwa Morocco ni wepesi. Wakumbuke ni Morocco hawa waliotoka sare na Ivory Coast.

Morocco niliowaona pale Neshno Stadium ni wazuri. Walikuwa na mpango kwenye mechi. Moja ya mpango wao ilikuwa kucheza kwa kuitafuta droo. Bahati mbaya kwao, kuwa Samatta na Ulimwengu waliwavurugia sana mpango wao na wakawa katika hali ya kuchanganyikiwa uwanjani.

Morocco tutakaokutana nao leo ni wengine kabisa. Ni Morocco wanaowajua akina Samatta na Ulimwengu. Ni Morocco watakaoingia uwanjani wakiwa na mpango mwingine kabisa wa mchezo. Na sisi lazima tuwe nao wa kwetu. Na si wa kuitafuta droo. Mpango wa KUSHINDA MECHI. Kupambana kwa dakika zote za mchezo hata tukiwa nyuma ya goli moja.

Ni muhimu ni kujitahidi kufunga goli ndani ya dakika 15 za mwanzo ili kupunguza presha ya mashabiki wa Morocco dhidi yetu.

Naam, mechi ya leo ni ‘ Mama’ wa mechi zote. Watanzania kwa Umoja wetu tuwaombee na kuwashangilia Stars. Kwa nguvu zote.

KILA LA HERI STARS, MUNGU IBARIKI TANZANIA.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger