UONGOZI
wa kampuni ya Bakhresa inayomiliki klabu ya Azam umemwaga dola milioni
moja (zaidi ya Sh bilioni 1.6) ili kupata haki ya udhamini wa Ligi Kuu
Bara kama warushaji wa matangazo ya televisheni.
Mwenyekiti wa Simba, Aden Rage.
Kutokana na kumwaga fedha hizo, kampuni hiyo kupitia kituo chake
kipya cha televisheni yake ya Azam TV, kitakachoanza kurusha matangazo
hivi karibuni, kitapewa haki ya kuonyesha mechi zote za Ligi Kuu Bara. Kampuni
hiyo iliyokuwa inapambana na Supersport ya Afrika Kusini iliyokuwa
tayari kutoa dola 500,000 imeihakikishia bodi ya ligi hiyo kuwa iko
tayari kutoa fedha hizo na kila klabu zikiwemo Yanga na Simba zitapata
Sh milioni 140 kila moja kwa msimu. Pamoja na fedha hizo kutoka kwa
wamiliki hao wa Azam FC ambayo ndiyo wapinzani wakubwa wa Simba na
Yanga, klabu hizo kongwe zimesema zinataka kulipwa zaidi kwa kuwa ndiyo
zenye mashabiki wengi.
Mwenyekiti wa Yanga, Yusuf Manji.
Katika kikao kilichofanyika juzi, kumezuka mjadala mkubwa huku Simba
na Yanga zikisisitiza kwamba haitakuwa haki zenyewe kupewa Sh milioni
140 sawa na klabu nyingine ambazo zina mtaji mdogo wa mashabiki. “Lakini
watu wa bodi ya ligi wameonyesha kutokuwa waungwana maana wameendelea
kulazimisha Simba na Yanga zilipwe sawa na klabu hizo ndogo. Sisi
tunaona hii si sahihi,” kilieleza chanzo cha uhakika.
Chanzo
kingine kimeeleza, uamuzi huo wa kampuni ya Bakhresa kupewa nafasi
kulikuwa kunapingwa ‘kiana’ na watu wa klabu hizo kubwa bila ya kujali
inatoa fedha nyingi mara mbili ya SuperSport kwa madai eti ni kubwa na
wataonekana nchi nyingi. Lakini wajumbe wengine walisisitiza suala la
fedha lipewe kipaumbele na fedha nyingi ndiyo zichukuliwe, hapo ndipo
kukaibuka suala la mvutano wa Yanga na Simba kutaka kupewa zaidi. Taarifa
zinaeleza tayari ufungaji wa mitambo ya Azam TV inaendelea kwa kasi ya
‘kimondo’ na baada ya siku kadhaa itaanza kazi huku ikitumia mitambo ya
kisasa zaidi nchini.