DIWANI mmoja wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) aliyekuwa anagombea umakamu mwenyekiti wa halmashauri ya
Geita, aliomba kura kwa kunadi sera za Chama cha Mapinduzi (CCM),
imefahamika. Diwani huyo, Dioniz Bugali wa Kata ya Kamhanga, vilevile
alimteua Diwani wa CCM kuhesabu kura zake.
Bugali alifanya kituko hicho mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa
halmashauri ya Wilaya ya Geita kwenye mkutano wa nne wa baraza la
madiwani kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Katika uchaguzi huo wa makamu
mwenyekiti wa halmashauri, mgombea wa wa CCM alikuwa Masoud Kimondo
ambaye ni diwani wa kata ya Kaseme na kwa Chadema alikuwa yeyé, Bugali.
“Nimesimama hapa kuomba kura…kabla ya kuomba kura naomba niseme
neno…nafasi hii ya makamu mwenyekiti wa halmashauri sikuwa naitaka
isipokuwa nimelazimishwa na chama changu(CHADEMA)kugombea.
“Nachotaka kusema hapa ni kwamba nikishindwa sitakata rufaa.
“Ninampongeza sana mgombea mwenzangu wa CCM,mimi hapa pamoja na kuwa
ni diwani wa Chadema na ninagombea nafasi hii kupitia chadema,lakini
bado ni katibu mwenezi wa CCM kwenye kata yangu ya Kamhanga…nipeni kura
zenu,”alijinadi Dionizi baada ya kupewa nafasi kuomba kura.
Kauli hiyo ilisababisha madiwani wa CCM kulipuka kwakicheko wakidai
Bugali ni mwenzao na wengine wakiitambia Chadema kwa kusema,
“Haloohalooooooooooooooo … Chadema mmesikiaaaa…hiyo ndiyo CCM…Spidi
120…Chadema hamna chenu Kamhanga huyo ni mwenzetu.”
Pia baada ya kura kupigwa diwani huyo wa Chadema alimteua Diwani wa
CCM Kata ya Nkome, Karema Chiratu kuwa wakala wake wa kuhesabu kura huku
madiwani wenzake wanne wa Chadema wakibaki mdomo wazi.
Akisoma matokeo hayo Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya hiyo Lupuga,
alimtangaza Kimondo kuwa mshindi kwa kupata kura 29,dhidi ya Bugali
aliyepata kura mbili.