Search in This Blog

MJUE MWANAUME ASIYEKUPENDA

Dalili za mwanaume ambaye hakupendi kwa dhati
Ni mtu wa maneno matupu
Mwanaume ambaye ana nia ya kukutumia na kukuacha, unaweza kupima hata maneno yake, mara nyingi anakuwa mtu wa maneno mengi ambayo hayatekelezeki. Ahadi zake ni nyingi ambazo baadaye unagundua kwamba ni hewa.

Huyu hana mapenzi ya kweli na nia yake ni kukuchezea na kukuacha na ndiyo maana anaweza kuropoka hata mambo ambayo anajua wazi kwamba hana uwezo wa kuyatekeleza. Mchunguze zaidi mwanaume wa aina hii, kwani dalili hii ni moja kati ya dalili 10 za msingi za kumtambua mwanaume ambaye hakupendi kwa dhati.
Hataki kuongelea maisha
Hataki kabisa kuzungumzia juu ya mustabali wa maisha yenu ya baadaye. Hataki mijadala ya mambo ya ndoa na ukianzisha anakukatisha. Hata mijadala hiyo inapotokea kwenye runinga au redio mkiwa naye, atabadilisha channel ili asisikilize au kuona.

Huyu bado yupo yupo, anapendezwa na uzuri na mwonekano wako ambao kwake ni pambo la muda tu, na siyo la kudumu kama ambavyo wewe unawaza. Hana mpango na wewe.
Uhusiano wa siri
Hataki uhusiano wenu ujulikane na ndugu zake au ndugu zako wa karibu. Hata inapotokea akalazimika kufanya hivyo, hutoa visingizio vingi. Anaogopa kukutambulisha kwa sababu anafahamu wazi kwamba hana nia ya kuishi na wewe hapo baadaye badala yake anakutumia tu.

Mpenda starehe sana
Hafikirii kabisa kuhusu maisha, muda wote anawaza starehe. Wengi wa aina hii ni wale ambao bado wanaishi na wazazi au ndugu, wakiwategemea kwa kila kitu.

Lakini pia kuna wengine ambao wanafanya kazi, lakini hawana malengo na kazi zao, muda wote ni starehe sana. Ni rahisi kukutana naye akiwa na fedha, lakini anapoishiwa hukukwepa. Anaogopa kwa sababu wewe kwake ni wa kujistarehesha tu.
Msiri kupitiliza
Hataki mambo yake yawe wazi sana, ukimwuliza anakuwa mkali. Hapendi umchunguze kuhusu mambo yake ya kazi, mbaya zaidi ni msiri hata kwa mambo ambayo una haki ya kuyafahamu.

Mathalani, simu yake inaweza kuingiza ujumbe mfupi wa maneno ambao utautilia mashaka au akapigiwa simu na kwenda kuzungumzia nje, akirudi ukimwuliza kwanini alitoka nje, anakuwa mkali. Huyu hana nia na wewe na ndiyo maana haoni thamani yako.
Hakujali
Kwakuwa anakupenda kwa ajili ya starehe, ukiumwa au kupata tatizo ambalo utahitaji msaada wake, hatoi ushirikiano.

Hawezi kuja kukujulia hali wala kukusaidia kwa namna yoyote ile. Hii inasababishwa na penzi lake ambalo siyo la kweli kwani yupo na wewe kwa ajili ya starehe tu.
Muda mwingi anakuwa bize
Mara nyingi amekuwa hataki kuwasiliana na wewe, unaweza kumtumia sms asikujibu na kama akijibu hujibu kwa kufupi sana. Tabia hii ni mpya ambayo mwanzoni hakuwa nayo.

Ukimlalamikia, atakujibu kwamba yupo bize na kazi. Kama ni suala la u-bize, basi alipaswa kuwa nao tangu awali, lakini hilo ni kinyume chake, kwani ni tabia mpya ambayo inakushangaza. Ukiona alama hii, ujue kuna tatizo.
Anakupuuza
Hapendi kukusikiliza katika suala zima la maisha yake, ukiachana na hilo pia, hapendi kukupa nafasi ya kutoa mawazo yako kuhusu jambo lolote lile. Mara zote, amekuwa akikuburuza kwa kila kitu.

Kama anakupenda, ni wazi kwamba angekupa nafasi ya kutoa mawazo yako kwa kila jambo linalohusu uhusiano wenu. Kukunyima nafasi hiyo, ni sawa na kukuambia wazi kwamba, hana future na wewe.
Anatishia kukuacha
Hata kosa dogo tu, kwake ni kubwa sana na linatosha kabisa kukutishia kukuacha. Katika hali ya kawaida, kama anakupenda hawezi kukutishia kukuacha.

Mtu anapokosea huonywa na siyo kutishiwa kuachwa. Mpenzi ambaye kijiugomvi kidogo kinapotokea anakutishia kukuacha ana matatizo na ni wazi kwamba hana nia nzuri na wewe.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger