MY GOD! Kiongozi wa Kanisa la Greek Orthodox duniani, Papa Theodor’s II ameamuru kufungwa kwa ukumbi uliopo ndani ya eneo la kanisa hilo lililopo Kiwanja Namba 7509 katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi jijini Dar es Salaam kufuatia kuwepo kwa picha za utupu za wanawake ukutani, Uwazi limechimbua.
Kaunta iliyopo ndani ya ukumbi huo.
PAPA THEODOR’S II ATUA BONGO
Papa huyo alifikia uamuzi huo Februari 19, mwaka huu baada ya kutua nchini ambapo alifanya mazungumzo na Rais Jakaya Kikwete.
Mbali na mazungumzo na JK, alipata nafasi ya kutembelea ukumbi huo ulio
kwenye eneo la kanisa hilo ndipo ‘alikutana’ na picha za wanawake wa
Kiafrika na Kizungu zikiwa zimetundikwa ukutani wakiwa kama
walivyozaliwa.
Kiongozi wa Kanisa la Greek Orthodox duniani, Papa Theodor’s II.
Mbali na picha hizo za utupu, pia kulikuwa na picha ya mwanamitindo
maarufu Bongo, Mariam Julius Odemba. Picha yake ilimwonesha akiwa amevaa
nguo ya heshima na maandishi juu ya picha yakiwa yameandikwa; ‘Thanks
British Legion for all your support. Miriam Odemba, 1st Oct 1999’.
Kufuatia hali hiyo, aligundua kwamba watu hao walikuwa wakinywa pombe hadi usiku wa manane jambo ambalo ni kinyume na maadili ya imani hiyo. “Kesho yake Papa Theodor’s aliamua kutembelea ndani ya klabu hiyo ndipo aliposhuhudia picha hizo chafu nyingi zikiwa zimetundikwa ukutani na chupa tupu za vinywaji vikali.
PAPA AAGIZA KIKAO CHA KUJADILI TUKIO “Kuona hivyo papa alimuagiza kiongozi wa Bodi ya Wadhamini wa Kanisa, Dimitri Kimon akutane na mapadri wote mwezi wa nne (uliopita) na ujadili hilo nia ikiwa ni kurejesha usafi na kuondoa uchafu huo kanisani hapo. “Katika mkutano huo waliamua kufunga na kuomba kisha kumtafuta wakili ili aweze kuwatoa waliokuwa wakiendesha ukumbi huo,” kilisema chanzo. Chanzo kiliongeza kuwa, Julai 8, mwaka huu viongozi hao waliamua kufunga geti la kanisa hilo na kuimarisha ulinzi kwa kutumia kampuni ya ulinzi ili kuzuia wanachama wa klabu hiyo kuingia eneo hilo isipokuwa waumini.
WALIOKODI UKUMBI WAPEWA UKWELI Habari zinasema viongozi wa kanisa hilo waliwaambia waliokuwa wakiendesha ukumbi huo kwamba kiongozi wao mkuu hakupendezwa na picha chafu za ukutani na alihoji endapo dini nyingine zikigundua uchafu huo wataelewekaje kwa jamii?
HAWA NDIYO WANACHAMA WA UKUMBI HUO Kuna madai kwamba wengi waliokuwa wakiingia kwenye ukumbi huo ni vigogo katika ngazi ya mawaziri na wabunge ambapo waandishi wetu walibahatika kuona jina la mbunge mmoja likiwa limeorodheshwa katika kitabu cha waliokuwa wakiingia.
KUNA HATARI YA KUFIKISHANA MAHAKAMANI Mwanachama mmoja wa klabu hiyo ambaye hakutaka jina lake kuandikwa gazetini kwa madai kuwa si msemaji, alisema wanakusudia kufungua kesi mahakamani ili kupinga adhabu ya kufungwa ukumbi huo kwa kuwa wapo eneo hilo kwa muda mrefu. “Sisi tupo katika eneo hili na tumefanya shughuli zetu siku zote hizo, tunashangaa leo kuona kanisa linatufungia geti. Ni lazima tutachukua hatua za kisheria,” alisema mwanachama huyo.
MAWAKILI WA PANDE ZOTE WAZUNGUMZA Gazeti hili lilimpata wakili wa kanisa hilo ambaye pia ni Katibu Myeka, Edward Chuwa alipoulizwa kuhusu mgogoro huo alikiri kuwepo. “Ni kweli kuna huo mgogoro kati ya kanisa na waendesha klabu hiyo lakini kwa kuwa mimi ni wakili naomba nisiseme chochote kwa sababu za kimaadili,” alisema Chuwa. Naye wakili wa waendesha klabu hiyo, Evodi Mmanda alipopigiwa simu na kuulizwa kuhusu mgogoro huo naye alikiri kuwepo. “Mgogoro huo naujua lakini kwa kuwa mimi ni wakili wao siwezi kusema chochote kutokana na maadili ya kazi yangu.” alisema Mmanda bila kusema ni lini kesi hiyo itasikilizwa.

