Search in This Blog

MTOTO ALIYEFARIKI MIAKA MITATU ILIYOPITA AKUTWA AKIWA HAI


MTOTO Shabani Maulidi (15) aliyefariki miaka miwili na miezi tisa iliyopita na kufanyiwa matanga, ameonekana akiwa hai baada ya kukutana na mama yake ana kwa ana juzi nje kidogo ya mji wa Geita wakati akienda kwenye shughuli zake za kibiashara.
Maulidi alitoweka ghafla na kushindwa kurudi nyumbani kwao Januari Mosi 2011, wakati alipokuwa amepeleka mbuzi machungani na mwili wake kuonekana baada ya siku tatu akiwa amefia kwenye kisima cha maji.
Kwa mujibu wa baba yake, Maulid Shabani, mtoto wake hakurudi nyumbani siku hiyo. Waliendelea kumtafuta bila mafanikio na ndipo baada ya siku tatu walimkuta akiwa amefia ndani ya kisima cha maji kilicho maeneo ya Kijiji cha Nyankumbu, Kitongoji cha Mwembeni.
Baba huyo alisema baada ya hapo walitoa taarifa polisi kisha waliruhusiwa kuuchukua mwili wa mtoto wao na kwenda kuuzika katika Kitongoji cha 14 Kambarage ndani ya mji wa Geita.
Alisema kuwa walifanya shughuli zote za matanga na wakajua tayari mtoto wao ameishafariki, kwamba hawakuwa na wazo lolote la kumpata akiwa hai tena kama ilivyotokea.
Shabani aliongeza kuwa tukio hilo ni la kustaajabisha kwake.
Naye mama mzazi wa mtoto huyo, Aziza Ramadhani akisimulia namna alivyokutana na mtoto wake, alisema kuwa alikuwa akienda kwenye shughuli zake za ujasiriamali, ndipo akakutana naye eneo la Nyankumbu nje kidogo ya mji wa Geita.
Alisema kuwa alipomuona alimwita kwa jina lake akisema “mwanagu Shabani ni wewe”, naye akamwitikia akiema “ni mimi”, kisha akamshika mkono huku akiwa haamini macho yake.
“Nilimpigia simu mume wangu, akaja tukamchunguza vizuri na kubaini kuwa ni yeye Shabani aliyesadikiwa kuwa alifariki na kuzikwa,” alisema mama huyo.
Aliongeza kuwa mtoto huyo alikuwa na alama ya kinundu kwenye paji la uso na mguuni akiwa na alama ya kovu iliyosababishwa na kuchomwa na mwiba. Pia alikuwa na mwanya kwenye meno uliofanana na wa baba yake.
Mtoto huyo aliyevuta hisia za watu wengi mjini Geita, ameendelea kuthibitishwa na walimu wake wa Shule ya Msingi Mwatulole pamoja na wanafunzi aliokuwa anasoma nao darasa la tano kabla ya kifo hicho cha utata.
Akizungumza na gazeti hili, makamu mkuu wa Shule ya Msingi Mwatulole, Joseph Nungula aliyekuwa akifuatilia kwa karibu tukio hilo, alisema kweli mtoto huyo anaonekana ni yeye bila kutiliwa shaka yoyote.
Mwalimu huyo alisema kuwa alimtambua mtoto huyo kwa sura na alama, hasa ya usoni huku akimwelezea kuwa alikuwa na mahudhurio mazuri shuleni. Pia maendeleo yake kitaaluma yalikuwa mazuri.
Mtoto huyo ambaye anaendelea kupewa huduma ya kitabibu katika Hospitali ya Wilaya ya Geita kwa uchunguzi zaidi wa kiafya, anaongea kwa shida wanapokuwepo watu wengi.
Hata hivyo, amewatambua baba na mama yake na kila wanapomuuliza maswali anawajibu.
Jeshi la Polisi mkoani hapa limethibitisha kutokea kwa tukio hilo, huku likiahidi kuendelea kutoa habari zaidi wakati huu ambapo wananchi wanasubiri kibali cha jeshi hilo kwa ajili ya kufukua kaburi alilokuwa amezikwa mtoto huyo.
-Tanzania Daima
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger