Search in This Blog

MTOTO WA MIAKA MIWILI AUAWA KIKATILI NA MJOMBA'KE TEJA,DAR

Kijana Said Hassan anadaiwa kumuua kikatili mtoto wa dada yake, Fatihia ‘Fety’ Said (2) na kuibua simanzi nzito.

Tukio hilo la kinyama lilitokea hivi karibuni maeneo ya Keko-Tolori jijini Dar ambapo ilidaiwa kuwa jamaa huyo ni teja.

Akizungumza kwa uchungu, mama wa Fatihia alisema kuwa siku ya tukio (Jumatano iliyopita) aliamka asubuhi salama na mtoto wake ambapo ilipofika muda wa saa 2:00 asubuhi alimpa mwanaye chai akawa anakunywa huku anatembea, wakati huo yeye alikuwa akifanya kazi zake za usafi wa ndani.

“Nilipomaliza usafi na kazi zangu nikaanza kumtafuta mtoto, sikumuona, niliingiwa na hofu hivyo nikawa namsaka kila kona ya nyumba lakini sikumuona.

“Nilikwenda nyumba ya jirani ambapo ndiko huwa anakwenda mara nyingi kucheza lakini pia sikumkuta, baada ya kujiridhisha kuwa hayupo nilienda kutoa matangazo msikitini kuwa mtoto amepotea,” alisema Mwamvita Hassan, mama wa mtoto huyo.

Alisema kuwa baada ya jitihada zote hizo bila mwanaye kupatikana aliondoka na wenzake na kwenda Mbagala, Dar akihisi labda kuna mtu amemchukua mtoto wake kwani huko kuna nyumba yao nyingine lakini nako hawakumkuta.

Kwa mujibu wa bibi wa mama Fatihia, walipomuuliza mtoto wa jirani alisema kuwa amemsikia mtoto akilia chumbani kwa mjomba’ke Said waende wakaangalie huenda alikuwa huko.

“Kweli tulivyoangalia tulimkuta mtoto amewekewa nguo chini ya kitanda, juu yake kawekewa magodoro, tayari alishaaga dunia, hatukujua kama alimnyonga au alimfanya nini kwani bado uchunguzi unafanyika kwa sababu mtoto alikutwa na mapovu mdomoni,” alisema bibi huyo.

Mjomba wa mtuhumiwa, Shaban Juma alisema kuwa mtuhumiwa hakuwa na akili nzuri kwani mara nyingi amekuwa akimpeleka Hospitali ya Wilaya ya Temeke, Dar na akawa anapewa dawa ingawa yeye hakutambua ni dawa gani.

Mjomba huyo alipoulizwa kama mtuhumiwa alikuwa akitumia madawa ya kulevya, alikubali na kusema kuwa kuna mtu alimthibitishia kuwa amekuwa akimuona ‘akijidunga’.

Habari za uchunguzi zilibainisha kuwa mtuhumiwa huyo amewahi kufanya matukio mbalimbali kama kujaribu kuchoma nyumba yao, kukojolea maji ya kunywa na kutishia kufanya kitu cha ajabu ambacho watu hawatakisahau.

Baba wa mtoto aliyejitambulisha kwa jina moja la Said alisema kuwa alisikitishwa na tukio lililompata mtoto wake lakini huyo shemeji yake alikuwa akimtishia kila siku.

“Nimeumia sana lakini naacha sheria ichukue mkondo wake kwa sababu ameshakamatwa,” alisema.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger