Dar es Salaam. Serikali imependekeza 
marekebisho ya sheria ya kudhibiti dawa za kulevya itakayotoa hukumu ya 
kifungo cha maisha na kufuta kipengele kwenye sheria ya sasa kinachompa 
mshtakiwa nafasi ya kulipa faini.
Sheria iliyopo sasa ya Udhibiti wa Dawa 
za Kulevya ya mwaka 1995 (Sura ya 95, Ibara ya 16) inasema, endapo mtu 
atakamatwa kwa kosa la kumiliki, kusafirisha, kuzalisha au kutengeneza 
mashine ya dawa za kulevya, atahukumiwa kifungo cha maisha jela au 
kulipa faini ya Sh10 milioni.
Hatua hiyo inakuja wakati idadi ya Watanzania wanaosafirisha, kuzalisha na kutumia dawa hizo ikiongezeka hapa nchini.
Pamoja na mapendekezo hayo, wadau 
mbalimbali wamesema kufanyika kwa maboresho hayo hakutasaidia kupambana 
na tatizo lililopo hivi sasa, ikiwa maadili ya wananchi na viongozi 
yaliyoporomoka hayatarekebishwa.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam
 (UDSM), Dk Kitila Mkumbo alisema sheria yoyote itakayowekwa haiwezi 
kuwa ‘mwarobaini’ wa kutibu tatizo la dawa za kulevya hapa nchini kama 
wanaohusika hawatawajibishwa.
“Hivi sasa zipo sheria, lakini 
hazitekelezwi. Kuna baadhi ya viongozi wakubwa kabisa wametajwa 
kujihusisha na dawa za kulevya, lakini hakuna hatua zozote 
zilizochukuliwa,” alisema Mkumbo.
Mbunge wa Kawe na Mjumbe wa Kamati ya 
Katiba, Sheria na Utawala ya Bunge, Halima Mdee, alisema Tanzania ina 
sheria nzuri na bora, lakini changamoto ipo katika utekelezaji wake kwa 
kuwa rushwa ina mchango mkubwa katika kudhoofisha maendeleo ya taifa.
Mdee alisema ingawa sheria ya rushwa 
iliyopo hivi sasa ni nzuri, ina kasoro kadhaa zinazohitaji kufanyiwa 
marekebisho ili kuipa nguvu zaidi.
Alisema baadhi ya viongozi waliopewa dhamana na wananchi wanatuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.
“Kama mtandao wa dawa za kulevya 
tunaousikia upo kuanzia viongozi wakubwa hadi wa chini, unadhani hata 
ukiwa na sheria nzuri itatekelezwa na nani? alihoji Mdee.
Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia na 
Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Godfrey Nzowa alisema mapendekezo 
ya sheria ya dawa za kulevya ni mazuri, lakini yana changamoto nyingi 
katika utekelezaji wake.
Alisema ingawa sheria mpya 
inayopendekezwa inataja adhabu ya juu kuwa ni kifungo cha maisha kwa mtu
 anayejihusisha na biashara ya dawa za kulevya, haijaweka wazi kiwango 
cha chini kwa mtuhumiwa atakayepatikana na kosa hilo.
“Kwa namna ilivyo sasa, sheria hii 
inaweza kuleta shida kwa sababu haitaji ‘minimum sentence’ (kiwango cha 
chini cha hukumu), hivyo mtu anaweza kusema mtuhumiwa afungwe mwaka 
mmoja,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema sheria ya dawa za kulevya 
iliyopo inaweka kiwango cha chini cha adhabu kuwa kisiwe kifungo cha 
chini ya miaka ishirini.
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki 
za Binadamu (LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema kinachotakiwa si 
sheria kali, bali viongozi wawajibike kwa kuwa kuna baadhi ya watu 
walikamatwa na vidhibiti lakini wameachiwa huru.
“Sheria kali zitakuwa kwa ajili ya 
wafanyabishara wadogo tu kwa sababu wale wakubwa wana fedha nyingi, 
ndiyo maana tunahitaji viongozi kama Dk Harrison Mwakyembe (Waziri wa 
Uchukuzi)wanaopambana, ingawa anaonekana kama anapigana na maji 
yanayomrudisha nyuma,” alisema Dk Kijo-Bisimba.
Mmoja wa vijana walioathiriwa na dawa za
 kulevya, ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa sababu za usalama, 
alisema sheria kali hazitasaidia chochote, kwa sababu wafanyabiashara 
wakubwa ndiyo wanaotoa rushwa ili waendelee kufanya biashara hiyo.
“Kama kweli wanataka biashara ya dawa za kulevya iishe kabisa hapa nchini, waanze kwanza kutokomeza rushwa,” alisema.
Mwanamke mmoja ambaye ametumia dawa za 
kulevya kwa muda mrefu, ambaye pia aliomba jina lake lisitajwe gazetini,
 alisema sheria hiyo ni kali na kwamba kama itatekelezwa kikamilifu 
‘mateja’ wengi ndiyo watakaopelekwa gerezani, kwa sababu wengi wao ni 
maskini.
“Ninachoona sheria hii itaongeza viwango
 vya kutoa rushwa kwa viongozi wasio waaminifu na kuwaacha watumiaji 
wengi maskini wakiozea jela,” alisema.
Jitihada zaidi
Mbali na mapendekezo ya kuboreshwa kwa 
sheria ya dawa za kulevya, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, 
Uratibu na Bunge, William Lukuvi alisema Serikali pia imetoa mapendekezo
 ya kuundwa kwa chombo maalumu kitakachokuwa na mamlaka kamili ya 
kumshtaki mtuhumiwa.
“Tume ya Kuratibu Dawa za Kulevya haina 
mamlaka kisheria ya kukamata, kukagua na kumfikisha mtu mahakamani na 
badala yake majukumu hayo yako kwa Kikosi Maalumu cha Jeshi la 
Polisi(Task force),” alisema.
Aidha, Lukuvi alisema mbali na kuwapo 
kwa kikosi hicho kinachoshirikiana na tume kutekeleza majukumu hayo, 
changamoto bado ni kubwa.
Mwananchi

 
 
 
 
 
