Search in This Blog

APELEKWA MAHAKAMANI NA KUPEWA DHAMANA KWA KOSA LA KUKOJOLEA KITABU KITUKUFU CHA QUR'AN

MKAZI wa Nsemlwa Kichangani mjini Mpanda, Mkoa wa Katavi, Japhet Nobert (15), amefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Mfawidhi mbele ya Hakimu Chiganga Ntengwe kwa tuhuma za kukojolea Quran Tukufu.
Mshitakiwa huyo anadaiwa kutenda kosa hilo juzi saa tano asubuhi katika eneo la Msikiti wa Kichangani uliopo katika Mtaa wa Nsemlwa mjini hapa.
Mwanasheria wa Serikali Mkoa wa Katavi, Mwandolomi, aliileza mahakama kuwa siku ya tukio mtuhumiwa alikojolea Quran hiyo ambayo ilikuwa imewekwa na watoto wa Kiislamu ambao walikuwa wakisoma madrasa katika msikiti huo.
Ilielezwa kuwa wakati watoto wa madrasa wakiendelea kucheza mpira wa miguu wakati wa kipindi cha mapumziko, Japhet alifika eneo hilo na kuanza kutenda kosa hilo, na hivyo wakamfuata na kuanza kumshambulia kwa kipigo.
Kwamba, Japhet aliendelea kupokea kipigo hadi hapo alipookolewa na mwalimu wa madrasa hiyo, Ustadh Khalfan Juma na Sheikh wa Mtaa, Yusuph Mkumba, ambao walilazimika kumhifadhi kwenye nyumba ya mwalimu wa madrasa hiyo na baada ya hali kuwa tulivu walimpeleka kituo cha polisi cha Mpanda mjini.
Japhet baada ya kusomewa mashitaka, alikiri kutenda kosa hilo, lakini alijitetea kuwa hakufanya kitendo hicho kwa makusudi bali wakati akiikojolea hakujua kama ni Quran bali alidhani ni kasha la kuhifadhia kanda za video.
Baada ya mshitakiwa kukiri kosa, hakimu Ntengwa aliahirisha kesi hiyo hadi Novemba 14 mwaka huu, huku akimpatia Japhet dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini wa kusaini bondi ya sh milioni 1.5.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger