JESHI la Polisi nchini limewafukuza
kazi askari wake 56 katika kipindi cha mwaka mmoja, kutokana na makosa
ya kuomba na kupokea rushwa pamoja na utovu wa nidhamu.
Kamishna msaidizi wa jeshi hilo,
Patrick Byatao, alisema hayo jana alipokuwa akitoa ufafanuzi juu ya
mambo mbalimbali hususan masuala ya nidhamu kwa askari wake katika
warsha ya siku maalumu ya polisi iliyofanyika mjini Bukoba.
Alisema kuwa askari waliofukuzwa ni
kutoka katika mikoa mbalimbali nchini ambao wamekutwa na tuhuma za utovu
wa nidhamu ikiwemo kuomba rushwa kwa wananchi. Kwa kipindi cha mwaka
2012, waliwafukuza askari 35 na mwaka huu 21.
Kwa mujibu wa Byatao, wapo baadhi ya
askari ambao wamekuwa wakitoa visingizio vya kuomba rushwa kwa sababu
mishahara yao ni midogo na haitoshelezi mahitaji yao.
Alisema ni heri askari wa aina hiyo
wakaacha jeshi, vinginevyo wataendelea kuchukuliwa hatua kama
hawatafuata masharti ya kazi yao.
Akitoa mada juu ya kuimarisha maadili
ndani ya jeshi hilo, Mrakibu Msaidizi wa Polisi kutoka makao makuu,
Andrew Makungu, alisema wameanzisha mkakakati wa kudhibiti vitendo vya
ukiukwaji maadili kwa askari wake ikiwemo rushwa.
Alitaja maeneo lengwa kuwa ni chumba
cha kupokea taarifa za mashitaka, usalama barabarani na upelelezi wa
makosa ya jinai. Bado juhudi zinaendelea ili kuboresha maeneo mengine.
Makungu alisema ubia wa kiutendaji wa
jeshi hilo umekuwa ukiimarika kila siku baada ya sehemu kubwa ya jamii
kutambua nafasi yao katika jukumu hilo.
Alisema mambo hayo yanaonekana
kutokana na wananchi kufanya ulinzi wa maeneo yao, kuchangia rasilimali
kwa jeshi, kutoa taarifa sahihi za uhalifu, kujenga vituo vya polisi na
kuanzisha vikundi vya ulinzi shirikishi. Hadi sasa viko vikundi 5,344
nchi nzima huku Mkoa wa Kagera ukiwa na 431.
Naye mgeni rasmi katika warsha hiyo,
Meya wa Manispaa ya Bukoba, Anatory Amani, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa
wa Kagera, Kanali mstaafu Fabian Massawe, alisema kuwa Jeshi la Polisi
limekuja na mkakati wa polisi jamii/ulinzi shirikishi unaoelekeza kuwapo
kwa mashauriano, majadiliano ya kiutendaji yanayosisitiza uwepo wa
maadili katika kazi, ikiwemo mapambano dhidi ya rushwa ndani ya jamii.