Search in This Blog

KIBADENI AFICHUA HUJUMA SIMBA, WACHEZAJI WA YANGA WALISHANGILIA USHINDI KABLA YA MECHI KUISHA

KOCHA wa Simba Abdallah Kibadeni amelaumu kuwa kuna hujuma imefanyika kwa wachezaji wake, wakati Mholanzi wa Yanga, Ernest Brandts amesema wachezaji wake hawako kiprofesheno. Kibadeni aliweka wazi kuwa Yanga isingeweza kuwafunga mechi hiyo lakini kwa sababu kuna watu wamevamia kambi yake na kuwadanganya wachezaji wakacheza chini ya kiwango. “Nawajua wachezaji wangu, kiwango kile si chao, hawakutaka kucheza ndiyo maana tulifungwa mabao yale matatu kipindi cha kwanza. Kuna watu wanakuja kambini na kuwapandikiza maneno wachezaji na hao waliopandikizwa maneno hawakucheza vile inavyopaswa kipindi cha kwanza wakaruhusu mabao matatu ya haraka haraka,”alisema Kibadeni katika Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam jana Jumapili. “Tulivyokwenda mapumziko, nilizungumza nao na nikawaambia, mmeshawapa mabao matatu yanatosha, sasa chezeni mpira,”alisema Kibadeni ambaye alienda mbali na kuwazungumzia kiungo, Abdulhalim Humoud ‘Gaucho’ na winga, Haruni Chanongo ambao aliwatoa na kuwaingia, Said Ndemla na William ‘Gallas’. “Siwezi kuwataja kwa majina, watajijua na kujichuja wenyewe. Yule Humoud nilimpanga kwa makusudi kama mlivyoona ndiyo maana nilimtoa,”alisema Kibadeni ambaye wiki iliyopita alikuwa akilalamika kwamba kuna wachezaji ndani ya Simba ambao wanamtengenezea majungu kwavile anawaambia ukweli na hawataki kufuata utaratibu wa kambi yake.

Kocha wa Yanga, Mholanzi Ernest Brandts alisema: “Tulistahili kushinda na ninachowalaumu wachezaji wangu hawako kiprofesheno kwa sababu baada ya kushinda mabao 3-0 kwenye mapumziko waliingia wanashangilia wakati mechi inaendelea. Nilishangaa sana. “Wakati wa mapumziko walivyoingia kwenye vyumbani walikuwa wanashangilia kama wameshinda mchezo, mpaka nikashangaa, sare wameitaka wenyewe, tulipata nafasi nyingi na tukashindwa kuzitumia. Timu nzima ilikuwa na upungufu, Luhende na Chuji walifanya makosa mawili yakatugharimu,”alisisitiza Brandts. Na alipoulizwa kama kuna hujuma, Brandts alisema inawezekana. “Haiwezekani tuongoze mabao matatu na baadaye warudishe yote, haiwezekani wachezaji wametuhujumu na kinachotakiwa tuwachomoe baadhi yao,”alisikika shabiki mmoja
maarufu.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger