Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(Chadema) kanda ya Kaskazini, kimemsimamisha Uongozi Mwenyekiti wa chama
hicho Mkoa wa Arusha Samson Mwigamba kwa madai ya kukihujumu chama
hicho.
Taarifa ambazo tumezipata kutoka
ndani ya kikao cha Baraza la uongozi kanda ya Kaskazini, kilichofanyika
katika Hotel ya Corridor Spring leo usiku, zimedai uamuzi wa
kusimamishwa Mwigamba umefikiwa na Kikao hicho baada ya kuwasilishwa kwa
vielelezo kadhaa vya Mwigamba na yeye kukiri kuwa ni vyake huku
vingine vikimuonyesha kuwa ndiye mmiliki wa Akaunti ya Jina la ‘Maskini
Mkulima’ ambalo limekuwa likitumika kukichafua chama kwenye mitandao ya
kijamii.
Hakuna kiongozi ambaye amekuwa tayari
kuzungumzia suala hili kiofisi, lakini taarifa za uhakika ambazo
tumezipata kutokana na maamuzi ya kikao hicho zimebainisha kuwapo kwa
maamuzi hayo pasipo shaka.
“Kikao hicho kimemsimamisha Uongozi
kupisha uchunguzi dhidi ya tuhuma zinazomkabili, hivyo kuanzia sasa
mwigamba siyo kiongozi, nadhani tamko litatolewa baadaye,” alieleza
mmoja wa wajumbe wa kikao hicho kilichofanyika Arusha na kuongeza kuwa
katika Kompyuta yake baadhi ya maandiko ambayo yamekuwa yakikikashfu
chama yamekutwa ikiwa ni pamoja IP address ya Jina na Maskini Mkulima
ambalo limekuwa likituma post ndani ya Jamiiforums kukuta zinafanana.
Jina la ‘Maskini Mkulima’ lilijiunga
na mtandao wa jamiiforums mnamo Desemba 27, 2011 na mpaka jana
inaonyesha alikuwa ametuma zaidi ya Post 27 ikiwamo hii iliyokuwa na
kicha cha habari: Wito kwa wana CHADEMA wote.
Makala hiyo ambayo ndiyo imefanikisha
kumbaini ilitumwa Jamiiforums Oktoba 19 Mwaka huu chini ya kichwa cha
habari cha ‘Wito kwa wana CHADEMA wote!’,
SOMA MAKALA HIYO HAPA
Kufuatia malumbano
yanayoendelea kwenye vyombo vya habari na madhaifu mengi ambayo
tumeshayashuhudia kwenye chama kwa sasa, natoa wito kwa wana CHADEMA
wote nchini kwamba wakati umefika tubadilishe uongozi wa juu wachama.
Kihistoria, CHADEMA
kati ya mwaka 2005 na 2010, agenda zetu kwa wananchi zilikuwa mbili.
Kupiga vita ufisadi, iliyosukumwa sana na Dr. Slaa na ile ya utetezi wa
raslimali zetu iliyobebwa na Zitto. Lakini sasa hivi chama kinaenda kwa
matukio.
Naandika nikiwa mwana
CHADEMA safi na nataka kila mwanachama atakayesoma atulie na
kutafakari. Hili siyo jambo la ushabiki. Nimawasiliano baina yetu wana
chadema na tunahitaji tutulie na kutafakari.
Nimekuwa mwanachama
wa siku nyingi na nimebahatika pia kuwa kiongozi ndani ya chama kwa
nyakati tofauti kwahiyo naelewa ninachokiandika.
Nadriki kusema
kwamba kwa sasa chama kinakwenda kwa matukio na ni bahati tu kwamba CCM
inaendelea kutupatia matukio lakini CCM na serikali yake wakitunyima
matukio, CHADEMA chini ya Mkt Mbowe, Katibu mkuu Slaa na Naibu Zitto
utakuwa ndo mwisho wake.
CHADEMA iliyopiga
kelele sana dhidi ya ufisadi, CHADEMA iliyopiga kelele mpaka sheria ya
vyama vya siasa ikabadilishwa na vyama kutakiwa kukaguliwa na Mkaguzi na
Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), eti leo inaungana na CCM
kumshambulia mwenyekiti wakamati ya bunge ya hesabu za serikali (PAC)
kwa kutamka kwamba vyama havijawasilisha ripoti zake za fedha
zilizokaguliwa. Kwa nini? Muungano huu wa CHADEMA na CCM maana yake
nini?
Kama chama
kinajiamini ni kisafi kwenye hesabu zake hofu ni ya nini? Si wasubiri
kikao na kamati ya bunge katibu mkuu aende na hizo ripoti na nyaraka
zinazoonyesha kweli wamewasilisha hesabu hizo?
Napenda kabla
sijaendelea mbele kuwapongeza wenyeviti wetu wawili wa kwanza ambao
kimsingi waliweka msingi mzuri sana wakutong’ang’ania madaraka na badala
yake kuachia mapema na kumwachia mwingine kidemokrasia bila vurugu.
Hawakuwa madikteta na
nawapongeza sana. Walijitahidi sana kutokuwa wapenda madaraka na
kimsingi walituwekea utamaduni ambao walitaka wote tuufuate na kujenga
taasisi imara inayojali demokrasia na haki ya kila mwanachama.
Ni kwa msingi huo
waliamua kuandika kabisa katika katiba yetu kwamba kiongozi yeyote
katika ngazi yoyote ya kuchaguliwa atakapogombea na kushinda ataongoza
kwa kipindi kimoja cha miaka mitano na kisha ataweza kugombea nakuongoza
kwa kipindi cha pili cha miaka mitano baada ya hapo hawezi kugombea
tena katika nafasi ile ile aliyoitumikia kwa vipindi viwili.
Ili kuonyesha kwamba
walimaanisha kile walichokisema, wote wawili hawakuwahi kukaa
madarakani kwa vipindi viwili vilivyoruhusiwa katika katiba bali wote
wawili walikaa kipindi kimoja kimoja tu.
Napenda pia
kumpongeza mwenyekiti aliyepo madarakani, Mbowe. Kuna mengi kakifanyia
chama. Kakitoa kutoka kwenye chama cha tatu ama nne kwa upinzani hadi
kuwa cha kwanza na kustahili kuitwa chama kikuu cha upinzani.
Kakichukua kikiwa na wabunge 5 bungeni na leo katika kipindi chake cha miaka 10 kina wabunge 49.
Ni achievement
kubwa! Si hivyo tu, ni wakati wake CHADEMA imebeba agenda nzito za
kitaifa kama vile vita dhidi ya ufisadi, utetezi wa raslimali, katiba
mpya,nk.
Lakini kuna matatizo
yameanza kujitokeza na tusipochukua hatua haraka huko mbele tunaweza
kupata shida kubwa. Ni muhimu kwa Mbowe kuelewa kwamba uwezo wake
umefikia hapo asitake kulazimisha kusonga mbele akidhani bila yeye
hakuna CHADEMA.
Akiache chama kikiwa
salama, abaki kama mwenyekiti mstaafu na awaachie wengine awamu
inayofuata ya kuingia madarakani. Kama hataki kuwa mwelewa na kuachia
ngazi, wanachama tumsaidie kwa kumpiga chini uchaguzi ujao.
Leo nitaainisha mambo
machache tu yanayohusiana na fedha za chama na uaminifu ili wanachadema
muelewe kwa nini viongozi wakuu wa chama wamehamaki sana kusikia
wanatakiwa kuwasilisha ripoti za fedha wakajikuta wanapambana na
mwenyekiti wa kamati ya bunge badala ya kamati na hata kufikia kusahau
kwamba huyo mwenyekiti wa kamati ya bunge ni mwenzao, ni naibu katibu
mkuu wa chama. Mengine nitaendelea kuyadondoa siku nyingine nitakapopata
fursa:
1. Wakati tukifanya
mabadiliko ya katiba mwaka 2006 hatukugusa kipengele kinachomzuia
kiongozi kuongoza kwenye nafasi moja kwa zaidi ya vipindi viwili vya
miaka mitano mitano.
Lakini wakati katiba
inachapwa chini ya uongozi uliopo, kipengele hicho kiliondolewa
kinyemela. Mambo yanayotokea hivi leo yanaonyesha dhahiri kipengele
hicho kiliondolewa kwa makusudi kwa maslahi na kwa faida ya viongozi
waliopo madarakani kwa sasa.
Hiki kinaweza
kuchukuliwa kama kitendo kidogo lakini kama viongozi wetu wanaweza
kutokuwa waaminifu katika jambo kama hili, ni dhahiri hawawezi kuaminika
na wanaweza kufanya mambo mengine makubwa nayenye athari
zisizomithirika kwa chama.
Ni muhimu wanachadema
mkafahamu kwamba kitendo cha kuondolewa kwa kipengele hicho ndicho
kinacholeta mpasuko leo kwenye chama unaotokana na Mbowe na Zitto
kupigania uenyekiti.
Kama kingekuwepo leo
Mbowe alikuwa anakatazwa na katiba kugombea kipindi cha tatu na hivyo
vita iliyopo kati yake na Zitto isingekuwepo na chama kingekuwa imara
zaidi.
Ni dhahiri Mbowe
aliondoa kipengele hicho kwa makusudi ili aweze kuendelea kugombea bila
mwisho na huu ni udikteta kama ule tu wa akina Lyatonga Mrema, John
Cheyo na wengineo, na wanachadema hatupaswi kuuruhusu si kwa Mbowe,
bali kwa yeyote atakayepata nafasi ya kuwa mwenyekiti wa chama chetu.
2. Matumizi ya fedha za chama:
Hakuna mtu anayejua
hivi sasa fedha za chama zinatumikaje zaidi ya kakikundi ka watu watatu
yaani Mwenyekiti Taifa, katibu Mkuu na Mkurugenzi wa Fedha.
Maamuzi ya vikao
hayaheshimiki tena na mabwana hawa. Baada ya uchaguzi wa 2010 vikao
halali vilielekeza kiasi na aina ya fedha ambazo hazitaguswa bali
zitunzwe kwenye akaunti maalum kwa ajili ya uchaguzi wa 2015. Lakini leo
si tu akaunti hiyo haina fedha bali hakuna akaunti yoyote yenye fedha.
Watu watatu ndo
wanaamua fedha zitumikeje. Mfano mwingine ni maamuzi ya kikao cha Baraza
kuu cha mwezi January kilichoamua kwamba kiasi cha fedha inayotoka
serikalini kipelekwe kwenye mikoa, wilaya namajimbo na kiasi kingine
kipelekwe kwenye kanda. Leo ni mwezi wa 10 maamuzi hayo hayajatekelezwa
ipasavyo.
Nyinyi viongozi wa
kanda,mikoa, wilaya na majimbo ni mashahidi wa hili . Lakini kuna
michango ya watu binafsi kama Mzee Sabodo, hizo nazo hazijulikani
zimechukuliwa lini kwa mfumo gani, zikatunzwa wapi na hatimaye
zimetumikaje.
Hapo sijataja fedha
zinazopatikana kutoka kwenye fundraising events mbalimbali kama ile ya
Dar es Salaam na Mwanza. Hizo nazo hazijawahi kuonekana na walioendesha
hizo fundraising, uaminifu wao kwenye masuala ya fedha ni questionable.
3. Taarifa za fedha
Tokea baada ya
uchaguzi wa 2010 mpaka leo, hakuna kikao chochote kilichowahi kupokea na
kujadili hadi mwisho ripoti ya mapato na matumizi ya fedha za chama.
Kila kikao agenda
hiyo inarushwa kiaina. Wanaojua mchezo huo ni watu watatu tu niliowataja
hapo juu na malengo ya kurusha hiyo agenda kila wakati na kukwepesha
isijadiliwe pia wanayajua wao.
Ni dhahiri
tukiendelea na hawa watu tutafika 2015 tukiwa hatuna pesa hata ya kuweka
mawakala kwenye vituo na tutapigwa tukiwa tumesimama.
4. Mipango ya kukipatia chama mapato ya ziada kutoka nje ya chama
Wakuu waliopo hawana
hata ndoto ya namna ya kupata fedha za ziada. Wanachokijua ni kukusanya
‘sadaka’ kwenye mikutano ya hadhara na kuwapatia kazi watu wanaoonekana
kuwa matapeli eti waendeshe harambee za kuchangisha fedha kwa njia ya
matukio.
Mawazo mazuri kama la
kuanzisha kampuni la uwekezaji la chama litakalowekeza kwenye miradi
mbalimbali, halijawahi kufanyiwa kazi, na hivyo uanzishaji wa miradi
mbalimbali ya kuiingizia taasisi fedha imebaki ndoto ya mchana.
Hatuwezi kufika hata
siku moja bila fedha. Hata uchaguzi wa wenzetu wa Kenya juzi juzi wakuu
wetu ingawa walishiriki lakini hawaonekani kama wamejifunza chochote.
5. Matumizi mabaya ya madaraka yanayoweza kuhusishwa na ufisadi
Chama chetu kinayo
kamati ya tenda ambayo iko chini ya sekretariat. Lakini kamati hii
haifanyi kazi imezimwa kimya kimya na wajumbe wote wa kamati ya tenda
kwa kuwa ni wachumia tumbo wanaojigonga kwa wakuu,wamekubali kuzimwa.
Leo ikidaiwa kamati
hiyo ilete nyaraka za mchakato wa manunuzi ya magari, pikipiki, kadi za
uanachama, set ya televisheni iliyofungwa ofisini kwa katibu mkuu,
hawana.
Manunuzi haya yote
yanafanywa na wakuu bila utaratibu wowote jambo ambalo ni hatari na
linarahisisha matendo ya kifisadi. Hivi tunavyoongea, ni mwenyekiti
taifa mwenyewe ndiye aliyenunua magari na pikipiki zote za M4C.
Hivi tunavyoongea
kuna shilingi milioni 80 ambazo mwenyekiti taifa alizichukua na kuagiza
kadi za uanachama tangu mwaka jana mpaka leo hizo kadi hazijawahi
kuonekana.
Na mwenyekiti
anafanya mambo hayo yote akitambua kwamba yeye ni mwenyekiti na hayo ni
masuala ya kiutendaji ambayo yako chini ya katibu mkuu kama mtendaji
mkuu wa chama na kamati yake ya tenda. Huu si ufisadi ni nini?
6. Makubaliano ya kifisadi na mtu binafsi anayeuza vifaa vya uenezi vya chama
Hakuna kikao chochote
cha juu kilichojadili ama kilichowahi hata kupewa taarifa tu kwamba
sasa kuna mtu binafsi kapewa tenda ya kuuza vifaa vya chama na chama
kinanufaika vipi na mauzo hayo na kwa nini vifaa muhimu vya chama kama
bendera vinauzwa na mtu binafsi. Jambo hili linajulikana kwa Mwenyekiti
Taifa na Katibu Mkuu wake tu.
Napenda kwanza kuipongeza kamati ya bunge kwa kuvikomalia vyama vinavyopokea ruzuku bila kujali ni chama tawala ama pinzani.
Pili namshauri CAG
unaweza kutumia kampuni binafsi kwenye wizara, idara, taasisi, wakala,
na asasi zote za kiserikali na serikali za mitaa kwenye ukaguzi lakini
kamwe usiruhusu vyama vya siasa vikaguliwe na kampuni hizo.
Hapo nenda mwenyewe
ndo utajionea mwenyewe. Kampuni binafsi kwenye vyama huko zinafundishwa
ziandikeje maoni yao. Nenda mwenyewe ujionee.
Pia kuna mkakati
unaendeshwa na CHADEMA Makao Makuu kwa sasa wa kuwapigia simu viongozi
wa mikoa hasa hapa Dar es Salaam na mikoa mikubwa kama Mwanza, Arusha,
Mbeya, nk, wakiwataka viongozi wa mikoani mtoe matamko kumpinga Zitto.
Kataeni ushenzi huu. Hili si jambo la Zitto ni la kamati ya bunge na
kimsingi ni la uadilifu ndani ya serikali na vyama.
Hata kama jambo
lenyewe lingekuwa limeagizwa na Mwigulu Nchemba msingetoa matamko ya
kupinga zaidi ya kuwaacha viongozi wetu wakuu watoe ripoti kuthibitisha
uadilifu wao japo kidogo maana ni ukweli pia kwamba kwenye ripoti
wanaweza kuzuga zikawa safi lakini ufisadi umefanyika.
Kama ni matamko toeni
matamko ya kuutaka uongozi wetu utoe hizo ripoti, na hapo ndipo mtakapo
jua kwanini hampati ruzuku. Kuna matumizi mengi sana ya hovyo na
ufisadi mkubwa unafanyika hapo Makao Makuu.
Nitaendelea kuwadondolea ili muone kwa nini napendekeza tuung'oe uongozi huu chini ya Mbowe.
Ahsanteni kwakunisoma!
Masikini Mkulima