Search in This Blog

NYUMBA YA NIYONZIMA YAUNGUA MOTO

 
KIUNGO wa Yanga, Haruna Niyonzima, amepatwa na tatizo kubwa baada ya nyumba yake kuungua moto jana asubuhi.
Niyonzima ambaye ni raia wa Rwanda, amejikuta katika wakati mgumu baada ya nyumba yake hiyo iliyopo eneo la Magomeni Makuti jijini Dar kuwaka moto ambao ulianza majira ya saa moja asubuhi na kuteketeza vitu vyote vilivyokuwa sebuleni.

Mara baada ya kupata taarifa hizo, Championi Ijumaa lilifika katika eneo la tukio na kumkuta Niyonzima akiwa na majirani zake na mkewe, Nailah, wakiwa katika hali ya majonzi huku vitu ambavyo viliteketea na moto yakiwemo masofa, televisheni aina ya ‘flat screen’ vikiwa nje, vikionekana havitaweza kutumika tena kutokana na kuathiriwa na moto kwa asilimia 90.
Akizungumza na Championi Ijumaa, Niyonzima alisema wakati moto huo ukianza, hakuwa anajua lolote, ambapo majirani zake ndiyo walioanza kuuona na kuamua kumuamsha, lakini tayari ulikuwa umeshateketeza karibu vitu vyote vilivyokuwa sebuleni, zikiwemo kompyuta zake mbili za ‘laptop’, ingawa walifanikiwa kuudhibiti kwa kutoingia katika vyumba vingine.
“Sebuleni hakuna tulichofanikiwa kuokoa, kila kitu kimeteketea na moto, kama mngekuta wakati unawaka, palikuwa hapapitiki kutokana na moto mkubwa ulioambatana na moshi mwingi, nashukuru hakuna aliyeumia zaidi ya hivi vitu vilivyoteketea.
“Nawashukuru sana majirani zangu, leo nimejua umuhimu wa kuishi vizuri na watu, niseme ukweli wamenisaidia sana katika kuudhibiti moto, kama isingekuwa wao, nisingeweza kufanya hivyo nikiwa mimi na mke wangu peke yetu, moto ulikuwa mkubwa sana,” alisema Niyonzima.
Aliongeza kuwa, bado hajajua hasara iliyopatikana na moto huo, ambapo sasa wanatafuta chanzo cha tatizo hilo, ingawa kwa haraka hali inaonyesha ni kutokana na hitilafu ya umeme.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger