Search in This Blog

PATA DONDOO ZILIZOJITOKEZA JANA KATIKA MECHI YA WATANI WA JADI

 Kikosi cha Simba kilichocheza na Yanga
 Kikosi cha Yanga kilichopepetana na SimbaMAAJABU! Ndivyo unavyoweza kulitafsiri pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga, baada ya jana kushuhudiwa wakitoshana nguvu ya mabao 3-3 katika mechi ya Ligi Kuu ya Vodacom huku lango moja likitikiswa mara sita.
Katika pambano hilo lililopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, mabao yote ya timu zote yalifungwa lango la kusini, matatu kipindi cha kwanza na idadi kama hiyo kipindi cha pili.
Walikuwa ni Yanga walioanza kujipatia bao dakika ya 15, likifungwa na Mrisho Ngasa ambaye alikuwa amenuia kuifunga Simba, akimalizia krosi ya Hamis Kiiza.
Dakika kadhaa baada ya bao hilo, shabiki mmoja wa Yanga alianguka jukwaani na kuzimia, ambako wafanyakazi wa huduma ya kwanza, walipata wakati mgumu kumfikia na kuwalazimu kuagiza machela kupitia kwa mashabiki ili kusaidia kumbeba.
Hamis Kiiza, aliiandikia Yanga bao la pili dakika ya 35, akimalizia mpira wa kurushwa wa Mbuyu Twitte uliongezewa nguvu kwa kichwa na Didier Kavumbagu.
Kama utani, dakika ya 44 Kiiza alipachika bao la tatu baada ya mabeki wa Simba kukosa umakini na kukatika.
Bao hilo nalo lilimzimisha shabiki wa kike wa Yanga na kulazimu machela kupelekwa jukwaani, kumbeba. Matokeo hayo yalidumu hadi dakika 45 zinamalizika.
Dakika 45 za kwanza, Yanga ilionekana kutawala mchezo huku baadhi ya wachezaji kama Ngasa na Haruna Niyonzima wakionesha madoido yasiyo ya msingi.
Kipindi cha pili, Simba ilibadilika baada ya kuwatoa Haruna Chanongo na kuingia Saidi Ndemla huku Abdulhalim Humud akimpisha William Lucian.
Alikuwa ni Betram Mombeki dakika ya 54 aliyeanza kumtungua Ali Mustafa ‘Barthez’ kwa shuti baada ya kuwatoka mabeki wa Yanga.
Simba iliendelea kusaka mabao ya kusawazisha, ambako dakika ya 57 Mganda Joseph Owino alifunga bao la pili kwa kichwa, akimalizia kona ya Ramadhan Singano ‘Messi’. Jinamizi la mashabiki kuzimia liliendelea, safari hii kwa upande wa Simba ambako mashabiki kadhaa walianguka na kuzimia baada ya mabao hayo mawili ya haraka haraka.
Wakati Yanga wakijiuliza, Simba ilifanikiwa kuchomoa dakika ya 80 kwa bao la Mrundi Gilbert Kaze kwa kichwa na kuibua shangwe za Wanamsimbazi.
Hadi mwamuzi Israel Nkongo akipuliza filimbi kuashiria dakika 90 kukamilika, Simba 3, Yanga 3.
Katika pambano hilo, licha ya tambo za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), na Wizara ya Mambo ya Ndani, lakini makundi kadhaa ya polisi yaliyokuweko uwanjani, yalionekana yakitingwa kuangalia mpira.
Awali, pambano hilo lilitanguliwa na mechi ya vikosi vya U-20 vya timu hizo; mechi ambayo ilimalizika kwa sare ya 1-1.
Baada ya mechi, makinda hao wa Simba na Yanga walijikusanya pamoja na kusali kisha kuwapungia mikono mashabiki kwa pamoja na kuingia vyumbani.
Simba: Abel Dhaira, Nassor Masoud ‘Cholo’, Haruna Shamte, Gilbert Kaze, Joseph Owino, Jonas Mkude, Ramadhan Siongano ‘Messi’, Abdulhalim Humud/William Lucian, Betram Mombeki, Amis Tambwe, Haruna Chanongo/Saidi Ndemla.
Yanga: Ally Mustafa ‘Barthez’, Mbuyu Twite, David Luhende, Nadir Haroub ‘Canavaro’, Kelvin Yondani, Haruna Niyonzima, Frank Domayo, Didier Kavumbagu, Mrisho Ngasa, Hamis Kiiza.
Kwa matokeo hayo, Simba imefikisha pointi 19 ndani ya mechi tisa na kubaki nafasi ya tatu nyuma ya Azam FC na Mbeya City zenye pointi 20 zikiwa zimeshuka dimbani mara 10.
Yanga yenye mechi tisa imefikisha pointi 16 na kusogea nafasi ya nne ikizishusha Mtibwa Sugar na Ruvu Shooting.
DONDOO KABLA YA MECHI
Saa 8:35: Basi la wachezaji wa Yanga likioneshwa ‘live’ kwenye runinga kubwa iliyoko ndani uwanjani. Mashabiki Yanga wanalipuka kwa shangwe.
Dakika 2 baadaye, basi la Simba nalo linaingia lango kuu na kuibua shangwe za mashabiki wao.
Saa 8:40: Wachezaji wa Yanga wakaingia vyumbani kupitia lango kuu huku Simba wakilisusia na kutumia mlango mdogo hadi uwanjani kisha vyumbani, kama vile wanakwenda mapumziko.
Saa 8:50: Upande wa mashabiki wa Yanga umejaa huku upande wa Simba ukiwa nusu kwa nusu.
Saa 9:15: Mwenyekiti wa Yanga anaibukia VIP na kuwapungia mashabiki wake huku akiwa amemshika mkono Makamu wake, Clement Sanga, na kuibua shangwe.
Dakika mbili baadaye, kigogo wa Simba, Zakaria Hans Pope, anajibu mapigo akiwa peke yake kwa kufanya hivyo.
Karibu kila kitu kabla ya pambano kuanza, Yanga walitangulia kufanya uwanjani.
Saa 9:18: Wachezaji wa Yanga wanaingia uwanjani kupasha na kushangiliwa wakifuatiwa na Simba dakika mbili baadaye na uwanja unalipuka kwa shangwe.
Hadi saa 9:30: Jukwaa la Simba upande wa mashariki bado halijajaa huku kwa Yanga kukiwa kumejaa hadi sehemu za kutembelea, wakati wafanyakazi wa huduma ya kwanza, wakiwa wametingwa kuhudumia mashabiki wanaoshikwa na presha kabla ya mechi kuanza.
Jezi gumzo. Jezi namba 17, 23 na 24 zilizua mjadala uwanjani kwa sababu tofauti. Namba 17 kwa mfano, zimevaliwa na Tambwe na Ngasa ambao walikuwa wanatazamwa na wengi kuzibeba timu zao, jezi namba 23 ilivaliwa na Mombeki na Canavaro ambao walibashiriwa kuwa kibaruani katika boksi la Yanga huku namba 17 ikivaliwa na Athuman Idd ‘Chuji’ na Abdulhalim Humud, viungo ambao walitazamwa kuwa injini za timu zao.
Saa 9:45: Timu zote zinamaliza kupasha na kurejea vyumbani kupumzika muda mfupi kabla ya kuanza kwa pambano, huku waamuzi nao wakijifua kwa mazoezi ya aina yake, ikiwamo yale ya kukimbia na kuwahi ‘offside’.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger