Search in This Blog

UKATILI: MAITI YA MTOTO WA MIEZI KUMI YACHUNWA NGOZI

MAMIA ya wananchi mjini Bunda na vitongoji vyake, juzi walifurika kushuhudia mwili wa mtoto mwenye umri wa miezi 10 aliyefariki dunia kwa ugonjwa wa malaria, lakini baadaye watu wasiofahamika wakachuna ngozi ya kichwa chake.
Tukio hilo ambalo limehusishwa na imani za ushirikina, lilitokea usiku wa kuamkia juzi katika mtaa wa Nyasura B Tarafa ya Serengeti katika mamlaka ya mji mdogo wa Bunda, wilayani hapa.
Ofisa Tarafa ya Serengeti, Justine Rukaka, alisema kuwa mtoto huyo alifariki dunia usiku katika hospitali ya DDH Bunda, baada ya kuugua ugonjwa wa malaria na mwili wake ukapelekwa nyumbani kwao kwa ajili ya maziko.
Rukaka alisema kesho yake asubuhi wakati wananchi wanaandaa shughuli za mazishi walishangaa kuona ngozi ya kichwa chake ikiwa imechunwa na watu wasiofahamika.
Ofisa upelelezi wa makosa ya jinai mkoani Mara, Jafari Mohamed, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo. Hili ni tukio la pili kutokea mjini hapa, kwani hivi karibuni mtoto mwenye umri kama huo pia alifariki dunia kwa ugonjwa wa malaria, lakini kesho yake wakati shughuli za mazishi zinaandaliwa walikuta amekatwa mdomo kwa imani za kishirikina.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger