Search in This Blog

HATARI: VIJANA WAUZA DAMU ZAO MITAANI KATI YA SHILINGI 10,000 HADI 30,000


Damu salama ikiwa imehifadhiwa kwenye mfuko maalumu wa kutunzi damu. Picha na Maktaba 

Dar es Salaam na mikoani. Wakati Serikali ikisisitiza kuwa huduma ya kumwongezea mgonjwa damu hospitalini ni bure, imebainika kwamba baadhi ya watu mitaani wakiwamo wabeba mizigo sokoni wanauza damu zao kwa watu wanaohitaji.
Mbali ya watu kuuza damu zao, majimaji hayo mekundu muhimu mwilini yamegeuka bidhaa adimu baada ya baadhi ya wauguzi na madaktari nao kugeuza huduma hiyo kuwa kitegauchumi chao.
Kwa mujibu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ni kosa kwa mtumishi yeyote wa afya nchini kumuuzia mgonjwa damu na wala hakuna biashara ya kuuza damu kwa kuwa hutolewa bure na watu wanachangia kwa hiari.
Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili katika hospitali mbalimbali nchini, umebaini hospitali nyingi hazina damu za kutosha na hivyo kusababisha baadhi ya wagonjwa kuwalipa watu mitaani, ili kuwatolea damu au kuinunua kwa wauguzi na madakari.
Hata hivyo, Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk Seif Rashid alisema kuwa wahudumu wa afya wanaoendesha vitendo hivyo ni watu wanaojaribu kuizidi maarifa Serikali na kwamba wananchi wamepewa taarifa za kutosha kuwa damu haiuzwi.
“Kuna watu wanajaribu kutuzidi maarifa, hiyo ni tabia inayopaswa kupigwa vita. Mtu yeyote atakayetakiwa kununua damu, atoe taarifa kwa mganga mkuu au kituo chochote cha polisi,” alisema.
Mkoani Dodoma
Wabeba mizigo wa soko la Majengo Mjini Dodoma, wamekuwa mkombozi kwa wagonjwa wanaofika katika hospitali ya mkoa huo baada ya kugeuza miili yao kuwa sehemu ya kuvuna damu na kuiuza kwa ndugu wa wagonjwa hao.
Gharama za kuuza damu hiyo ni kati ya Sh10,000 hadi Sh30,000 kwa chupa moja, kutegemea na uwezo wa ndugu wa mgonjwa huyo, lakini baadhi wamekuwa wakitoa zaidi kama sehemu ya shukurani.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Dodoma na kuthibitishwa na baadhi ya wabeba mizigo hao, imebainika kuwa kitendo cha kutoa damu kwa wabeba mizigo ni cha kawaida na kwamba utaratibu huo ulianza muda mrefu.
Enock Ayub ambaye ni mmoja wa watu ambao wamechangia damu zaidi ya mara tatu kwa nyakati tofauti, alilimbia gazeti hili kuwa biashara ya kutoa damu anaipenda na kwamba inampa matumaini ya kuishi kwa kuamini kuwa bado ni mzima.
“Mimi nimechangia damu zaidi ya mara tatu, lakini tukifika kule tunabadilisha majina maana madaktari wanataka mtu ukae muda za miezi sita bila ya kutoa, sisi tunataka fedha ‘mkwanja’, hatuna jinsi,” alisema Ayubu na kuongeza:
“Hata hivyo, napenda kutoa damu kwani ukiona wanakutoa ujue afya yako ni nzuri na huna Ukimwi na magonjwa mengine.”
Alipoelezwa hatari za kutoa damu mara kwa mara bila kuzingatia ushauri wa daktari alisema, “Sioni tatizo maana fedha tunazolipwa tunazitumia kunywa bia na matunda, hivyo afya zetu hurejea kama kawaida, tena baada ya muda mfupi.”
Baadhi ya wodi ambazo gazeti hili lilitembelea na kuzungumza na baadhi ya wagonjwa, lilibaini kuwa tatizo la damu katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma limekuwa sugu, huku ndugu wa wagonjwa wakilalamika kuwa wanauziwa damu kwa bei ya kati ya Sh40,000 hadi 60,000 kwa chupa moja.
“Mimi sitaki uniandike jina langu gazetini, lakini ukweli ni kuwa madaktari walimpokea mgonjwa vizuri na damu aliwekewa haraka sana tatizo likaja kwenye kuirudisha niliambiwa nitoe Sh60,000 au mimi nitolewe damu, nilipogoma nikaonyeshwa Soko la Majengo kwa wabeba mizigo,” anasema ndugu huyo.
Anasema kuwa alipofika kwa wabeba mizigo walimuuliza daraja la damu aliyotoa na alipowatajia walijitokeza wawili wenye daraja hilo wakaanza kupatana bei kabla ya kukubaliana na mmojawao kwa kiasi cha Sh 25,000.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Dk Nasoro Mzee, alikiri tatizo la damu ni kubwa katika hospitali hiyo na kwamba linatokana na mwitikio mdogo wa wananchi katika kuchangia katika benki ya damu.
Dk Mzee alisema hadi sasa kitengo hicho kina upungufu wa damu na kwamba ni wanafunzi na askari tu ndio wanaochangia damu kwa kiwango kikubwa.
“Wakifika watu ambao wana mahitaji ya haraka tunachukua damu na kuwawekea, wengine ni kweli tunawaambia wachangiwe na ndugu zao, na kwa wale waoga kutoa huwa wanakwenda kutafuta kwa wanaojitolea kutoa damu,” alisema Mzee.
Alifafanua kuwa siyo kila damu inayotoka kwa mtu inakuwa salama kutumika, ni lazima ipimwe.
-mwananchi
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger