"HAYA YOTE NI KWA SABABU YA URAISI NA MABILIONI YA USWIZI" MANENO YA ZITTO
Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe amesema tuhuma alizosomewa na uongozi wa Chadema katika kikao cha Kamati Kuu sizo zilizoelezwa na chama hicho mbele ya waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho.
Aidha, amesema kuwa vita aliyopo siyo kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi, akitaja magenge ya watu wanaotaka urais 2015 na walioficha fedha nje ya nchi walioungana wakiona tatizo lao ni yeye hivyo kutaka kumwondoa bungeni.
Akizungumza katika mahojiano maalumu na gazeti hili kwa njia ya simu, Zitto alisema kuwa hadi sasa bado hajapokea tuhuma 11 anazokabiliwa nazo, hivyo hajui makosa hayo na bado anasubiri akabidhiwe kwa maandishi.
Ana ugomvi gani na viongozi wenzake?
Alipotakiwa kueleza iwapo ana ugomvi na watu ndani ya Chadema, Zitto alisema kuwa huenda mambo hayo yanatokea kwa sababu mahasimu wake wa kisiasa wa ndani na nje wameamua kuungana na kupambana naye ili kumdhoofisha kisiasa kwa masilahi yao.(P.T)
"Matatizo yaliyopo ni mafanikio yangu, .... nadhani hii siyo vita kati ya Chadema na Zitto, bali ni vita ya watu wengi, pengine magenge ya watu wanaotaka urais na wale walioficha fedha zao nje wamekaa pamoja wanaona tatizo lao ni Zitto... wanajua siwezi kusemea nje maana sina kinga..., hivyo wanataka kuniondoa bungeni..." alisema.
Aliongeza kuwa kwenye siasa kinachohitajika ni kusimamia misingi, jambo alilosema binafsi amekuwa akilifanya katika kipindi chake chote cha kisiasa.
Zitto alisema kuwa ni vyema wananchi wakawapima wabunge wao kwa kazi wanazozifanya bungeni akibainisha kuwa kati ya mwaka 2011 hadi 2013, yeye amewasilisha hoja nyingi nzuri zilizo na mashiko ikilinganishwa na wabunge wenzake wanaomtuhumu kutumiwa na CCM.
"Je, mbunge anayetumika na Chama Cha Mapinduzi anaweza kupeleka hoja ya kumng'oa Waziri Mkuu na kumshinikiza Rais mpaka akasimamisha kazi mawaziri wanane? Je, mbunge anayetumika anaweza kushikia bango watu wanaotorosha fedha nje ya nchi?" alihoji Zitto.
Tuhuma za usaliti
"Sizijui hizo tuhuma 11 kwa sababu nilichoelezwa kwenye kikao cha Kamati Kuu sicho kilichoelezwa na chama kwenye mkutano wake na waandishi wa habari... hivyo sijui kabisa hizo tuhuma zangu ni zipi mpaka sasa," alisema.
Alisema kuwa kwenye Kamati Kuu alilaumiwa kwa masuala matatu. Akizitaja: "Nililaumiwa kuwa sifanyi kazi za chama, la pili kuwa nimemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali akague vyama kutokana na kuwa na nia mbaya na chama hicho. Tuhuma ya tatu ni ile ya kukataa kupokea posho bungeni ambapo nadaiwa kulenga kuwadhalilisha wabunge wenzangu."
Zitto alisema kuwa baada ya kuzijibu tuhuma hizo mbele ya wajumbe wa kikao cha Kamati Kuu na katika mkutano wake na waandishi wa habari, akashangazwa na tuhuma alizoziita mpya kuwa anatuhumiwa kutokana na waraka ambao yeye hahusiki nao, licha ya kutajwa kuwa mfaidika tu.
"Mimi sihusiki na waraka wowote, huo unaodaiwa kusambazwa kwenye mitandao wala mwingine wowote... ni wajibu wa chama kueleza mimi nahusikaje na waraka ule," alisema.
Madai ya Mwanasheria wa Chadema kuvunja Katiba
Zitto alisema jambo linalompa shaka kuwa huenda suala lake limelenga kumdhoofisha kisiasa ni kitendo cha mwanasheria wa chama hicho, Tundu Lissu kuamua kuvunja katiba ya chama hicho kwa makusudi.
Alifafanua: "Katiba ya chama (Chadema), inasema kwamba kiongozi wa ngazi fulani ataondolewa kwenye uongozi na ngazi iliyomchagua. Mimi nilichaguliwa na Baraza Kuu la Chama, siyo Kamati Kuu... sasa iweje Kamati Kuu iniondoe?"
Alisema kimsingi Kamati Kuu haina mamlaka ya kumvua uongozi bali ina mamlaka ya kuweza kumsimamisha uongozi kusubiri kikao kilichomchagua kufanya uamuzi wa kumwondoa katika uongozi au kumrejesha.
Zitto alidai kuwa Lissu alisema uongo kuwa hata Dk Wallid Kabourou aliondolewa uongozi na Kamati Kuu na kwamba ukweli ni kuwa Dk Kabourou alijiondoa mwenyewe na kuhamia CCM na kwamba hata Chacha Wangwe hakuondolewa na Kamati Kuu isipokuwa alisimamishwa na kusubiri Baraza Kuu ambapo kabla ya Baraza Kuu kuketi alifikwa na mauti.
Kwa nini hapokei posho?
Alipoulizwa ni kwa nini yeye hapokei posho za wabunge alisema suala la posho siyo lake binafsi bali ni suala la imani na msimamo wa chama hicho, ambao waliuweka wakati wa kampeni na ni miongoni mwa mambo waliyowaahidi wapigakura wakati wa kampeni, hivyo yeye anachofanya ni kutimiza tu ahadi.
Aliongeza kuwa wakati wa kampeni za mwaka 2010, walikuwa wakiwaeleza wananchi kuwa wabunge wanapokea fedha nyingi na kuwa wakichaguliwa watapunguza posho hizo na kwamba Chadema ilipofanikiwa kushinda chama kilikubaliana watekeleze ahadi zile.
Alidokeza kwamba walikubaliana kutekeleza kwa kuanza na mambo mawili moja likiwa kukataa kuchukua posho za vikao, maana ni kinyume cha utaratibu na suala la pili ni kuacha kutumia shangingi la Serikali ambalo linatumika na Kiongozi wa Upinzani Bungeni.
Alisema katika kutekeleza uamuzi huo Mbowe alitangaza hatua ya kurudisha shangingi na yeye (Zitto) kama Waziri Kivuli wa Fedha akatangaza kuacha kupokea posho.
"Tulikubaliana wote tutekeleze hayo... lakini wenzangu wakashindwa kuyatekeleza, na mwenzangu akalirudia gari na analitumia mpaka sasa... kwangu mimi mafunzo niliyofundishwa kisiasa ni kwamba unayoyasema, yatekeleze, wenzangu hiyo 'principal' ya kutekeleza wanayoyasema hawana," alisema.
Kuhusu tuhuma kuwa anakataa posho lakini anapokea rushwa kubwa kubwa, Zitto alisema iwapo kuna mtu aliye na ushahidi na hilo aupeleke vyombo vya dola, wamshtaki na achunguzwe kisha achukuliwe hatua.
Alisema mbali na posho, wabunge wanaongoza kwa kupewa misamaha ya kodi mbalimbali ukiwemo msamaha wa kodi ya uingizaji wa magari.
"Hii nayo tulikubaliana kuikataa... na katika kulitekeleza hili, nilipoagiza gari langu nilikataa msamaha nikalipa kodi hadi nilipoitwa na Kamishna wa Kodi na kuulizwa iweje nilipe kodi wakati nina msamaha wa kodi nikamjibu kuwa ni suala la 'principal' tu," alisema.
Ruzuku
Kuhusu suala la ukaguzi wa ruzuku ya chama, Zitto alisema yeye anapokuwa Mwenyekiti wa PAC anasimamia taifa, hasimamii chama, hivyo kwa nafasi yake ya PAC na kamati nzima waliona siyo halali vyama vya siasa kukaa bila kukaguliwa.
Alisema alipigania suala hilo tangu mwaka 2011 alipomwandikia barua Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali kumuuliza kwa nini hakagui hesabu za vyama vya siasa wakati sheria inataka vikaguliwe.
Je, ana shaka kuhusu matumizi ya ruzuku ndani ya Chadema?
"Nitaweza kusema jambo hilo kwa uhakika baada ya ukaguzi kufanyika. Mpaka sasa hakuna chama ambacho kimekaguliwa, hivyo inawezekana matumizi mabaya ya ruzuku yako CCM, CUF, NCCR-Mageuzi, Chadema au yako katika vyama vyote...
"Haiwezekani kila mwaka sisi (wabunge) tunaipigia kelele Wizara ya Kilimo na Maendeleo ya Mifugo, haiwezekani kila mwaka tunaipigia kelele Bodi ya Korosho, halafu vyama vya siasa ambavyo vinapokea zaidi ya Sh29 bilioni kila mwaka, tukisema, tuonekane wasaliti," alisema Zitto.
Chadema yajibu
Alipotakiwa kuzungumzia madai hayo ya Zitto, jana Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willbroad Slaa alisema kuwa hawezi kulumbana na mtu kwa njia ya magazeti na kwamba kazi yake yeye ni kufafanua Katiba, kanuni na miongozo ya Chadema pindi inapohitajika. Anaripoti Ibrahim Yamola.
Alisema endapo kama kuna vifungu katika Katiba, kanuni au miongozo vilivyokiukwa katika kufanya uamuzi hayo vibainishwe na si kuongea katika magazeti bila kueleza makosa yaliyofanyika.
"Mimi kazi yangu si kulumbana katika magazeti, kama anaona (Zitto), kuna mambo yamekiukwa anatakiwa kuyawasilisha sehemu inayohusika ili hatua zaidi zichukuliwe.
Wewe mwandishi umeoa? (Mwandishi; hapana), ungekuwa umeoa ningekuuliza hivi; unaweza kutoa siri za ndani za mke wako kwa watu wengine?," aliuliza Dk Slaa.
Akizungumzia kuhusu mikutano inayoendelea mikoani, alisema haina lengo la kuwaeleza wananchi juu ya uamuzi wa Kamati Kuu ya kuwavua madaraka Zitto na wenzake, bali ni utekelezaji wa mkutano wa Baraza Kuu la chama hicho uliofikiwa Junuari mwaka huu.
"Mikutano hiyo imeanza tangu Aprili mwaka huu, iko katika ngazi za vijiji na vitongoji vikikijenga chama na wala si kwa dhana yoyote zaidi ya hiyo," alisema Dk Slaa.
Chanzo:Mwananchi