RAIS wa Uganda, Yoweri Museveni ametetea
mazungumzo ya kile kinachoitwa ushirika wa hiari unaohusisha nchi tatu
za Uganda, Rwanda na Kenya, huku akiishangaa Tanzania kuhusu madai yake
ya kutengwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). Museveni
alidhihirisha mshangao wake huo jana mjini hapa, wakati akizungumza na
waandishi wa habari baada ya kukamilika kwa mazungumzo yaliyowahusisha
Rais wa Rwanda, Paul Kagame na Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta.
Katika kikao hicho, Museveni alidai
majadiliano hayo ni sahihi kwa kuwa nchi hizo zinachojadili ni miradi ya
miundombinu kwa ajili ya ukanda wa kaskazini.
Museveni alidai Tanzania itahusishwa
wakati majadiliano yatakapohamia ukanda wa kusini, ambako ndiko lilipo
taifa hilo lenye eneo kubwa zaidi miongoni mwa wanachama wa EAC.
Kauli kama ya Museveni pia ilitolewa na
Rais Kenyatta wakati akizungumza na Wakenya waishio nchini Rwanda,
akipuuza hofu iliyojengeka kuwa jumuiya hiyo inaelekea kuvunjika.
Rais Kenyatta alisema utekelezaji wa
miundombinu ya kimaendeleo unaohusisha nchi hizo pamoja na Sudani
Kusini, hauhujumu mtangamano wa jumuiya hiyo.
“Tumedhamiria katika malengo yetu ya
mtangamano wa eneo hili na kulifanya listawi. Kwa sasa tunatarajia kaka
na dada zetu wa Sudan Kusini kuungana nasi muda si mrefu na kuifanya EAC
istawi na kuwa na nguvu zaidi,” alisema.
Aliendelea kueleza kwamba, tofauti na
kinachoelezwa na ‘maadui’ wa mtangamano wa EAC, wanachama wote wa
jumuiya hiyo bado wamedhamiria kuungana.
“Kutokana na wasiwasi wa majirani zetu,
niliamua kuchukua hatua zilizofanikisha kupunguza siku za kusafirisha
bidhaa kutoka Mombasa kwenda Kigali kutoka siku 22 hadi nane,” alisema.
Aidha alisema Serikali yake imeondoa
vikwazo vyote vya usafirishaji mizigo na anatarajia mizigo itasafirishwa
kwa kasi na urahisi zaidi katika nchi zote jirani.
Hata hivyo, viongozi hao walikwepa
kuzungumzia suala nyeti zaidi ambalo nchi hizo katika mikutano miwili ya
nyuma ziligawana majukumu ikiwamo kushughulikia suala la katiba ya
shirikisho la kisiasa, viza moja, ushuru wa forodha na mengineyo ambayo
yamo ndani ya mipango ya EAC.
Hivi karibuni, Waziri wa Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Samuel Sitta alieleza msimamo wa Serikali ya Tanzania
kutokana na kitendo cha nchi hizo kujiundia utatu wa hiari ndani ya EAC.
Akijibu moja ya maswali ya wabunge mjini
Dodoma hivi karibuni kuhusu mwelekeo huo unaotishia mustakabali wa
jumuiya hiyo, Sitta alisema Serikali imeamua kutohudhuria mikutano yenye
ajenda ambazo nchi hizo tatu zimeshaweka msimamo wa peke yao.
Sitta ambaye awali aliwahi kuonya kwamba
kinachofanywa na nchi hizo ni kinyume na makubaliano na mkataba wa EAC,
alienda mbali akisema Serikali imeshaanza mazungumzo na Burundi pamoja
na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ili kuanzisha ushirikiano
wao.
Aidha alifafanua kauli ya hivi karibuni
ya waziri mwenzake wa Mambo ya Nje, Bernard Membe, kwamba Tanzania
inasubiri talaka, akisema yenyewe ndiyo yenye uwezo wa kutoa talaka kwa
jumuiya hiyo kwa kuwa inamiliki asilimia 52 ya eneo lote, huku nchi
zilizobakia zikigawana asilimia 48 iliyobakia.
“Hawa wenzetu wanafanya utoto wa
kutuzunguka, sisi tunatumia hekima ya Mzee Mwinyi aliyesema ‘mwongo,
mwongoze.’ Kama wao wana hila zozote juu yetu, siku si nyingi
tutazibaini, kama ni ndoa ya kwenye jumuiya basi sisi ndiyo tutakuwa
tumeoa. Hivyo tutatoa talaka sisi,” alisema.
Hata hivyo, Rais Museveni alipoulizwa na
mmoja wa wanahabari wakati wa mkutano wake mjini Kigali, alidai kuwa
hana taarifa ya malalamiko yanayotolewa na Tanzania kuhusu utatu wa nchi
zao.
“Hadi nitakapopata barua rasmi kutoka
Serikali ya Tanzania ndipo nitakapoamini, vinginevyo nahesabu kile
ninachoshuhudia katika vyombo vya habari ni uongo,” alisema.
Hata hivyo, wanadiplomasia wa Tanzania
wamekuwa wakieleza wasiwasi wao kuhusu kuachwa katika mipango ya jumuiya
hiyo, wakisema haikualikwa kushiriki na wanatarajia kulifikisha suala
hilo katika kikao cha wakuu wa EAC kitakachofanyika mjini Kampala,
Uganda mwishoni mwa Novemba mwaka huu.
-Mtanzania
