Search in This Blog

MKUU WA JESHI LA POLISI IGP MWEMA KULISHUGHULIKA SWALA LA MH KAPUYA, SAMWELI SITTA NAYE ALONGA




SAKATA la Mbunge wa Urambo Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM) kudaiwa kumbaka mwanafunzi na kumtishia kumuua, linazidi kuchukua sura mpya ambapo Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Said Mwema na Wizara ya Jamii, Jinsia na Watoto wamengilia kati. 
 
Jana gazeti la  Tanzania Dama  liliripoti kauli ya Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa watamchukulia hatua Kapuya mara moja baada ya mtoto huyo kuandikisha maelezo na kuwasilisha vielelezo polisi.
 
Wakati hali ikiwa hivyo, huku chama chake, Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kikijinasua na kutaka Kapuya abebe mzigo wake mwenyewe, Tanzania Daima limedokezwa kuwa IGP Mwema tayari ameingilia kati na kumwagiza Kamishna Kova kuhakikisha suala hilo linashughulikiwa haraka.
 
Chanzo hicho kilidokeza kuwa IGP amelazimika kuingilia kati baada ya kufuatwa na Naibu Waziri wa Jamii, Jinsia na Watoto, Ummy Mwalimu, aliyetaka kujua ni kwanini mtuhumiwa hachukuliwi hatua baada tuhuma hizo kufichuliwa.
 
Taarifa za ndani zilidokeza kuwa serikali sasa inaendelea na utaratibu wa kumwandalia Prof. Kapuya mashitaka ya ubakaji na kutishia kumuua mwanafunzi huyo wa miaka 16.
 
Kwa siku tatu mfululizo Tanzania  Daima  limeripoti madai ya mtoto huyo aliyedaiwa kubakwa na Prof. Kapuya, ambaye pia amewahi kushika nafasi za uwaziri katika wizara mbalimbali.
 
Kwa mujibu wa ujumbe mfupi wa maandishi ya simu (sms) ambao Tanzania Daima  linao, Prof. Kapuya kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina lake alitishia kumuua mtoto huyo na dada yake akitamba kuwa serikali hii ni yao haiwezi kumfanya kitu.
Katika hatua nyingine, Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta, amesema nchi imefika pabaya kama viongozi wanaweza kutoa vitisho na tambo za watoto wao kuuza dawa za kulevya, huku vyombo vya dola vikishindwa kuchukua hatua.
 
Sitta ambaye pia ni spika mstaafu na Mbunge wa Urambo Mashariki, alitoa kauli hiyo mwishoni mwa wiki katika mahafali ya 15 ya kidato cha nne ya Shule ya Sekondari Agape Seminari iliyoko Marangu, wilayani Moshi vijijini.
 
Alisema kuwa nchi imegawanyika kimakundi, ambapo baadhi ya viongozi wamekuwa na kiburi cha kutamba kwamba hawawajibiki kwa vyombo vya kisheria.
 
Sitta alitolea mfano kitendo cha waziri mstaafu ambaye sasa ni mbunge, aliyeripotiwa na vyombo vya habari akidaiwa kumtisha mtoto aliyemtuhumu kuwa alimbaka mara mbili alipoitwa kwake kuchukua ada.
Katika moja ya ujumbe wa maandishi (sms), mbunge huyo ambaye Waziri Sitta alimtolea mfano, anatamba na kumtisha binti huyo kuwa atamuua huku akihoji: “Watato wetu wanauza unga nani anawakamata? Nani atapigana nasi?”
 
Sitta alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi kubwa, hivyo haiwezi kuendeshwa hovyo hovyo, na kwamba lazima iendeshwe kwa viwango vya maadili vitakavyoleta maendeleo.

-Tanzania Daima
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger