MWANAJESHI aliyemuua Rais Abeid Karume kwa risasi Aprili 7, 1972
Luteni Hamud Mohamed Hamud, imeelezwa kuwa baba yake mzazi mzee Mohamed
Hamud alikuwa mpinzani mkubwa wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Mzee Hamud alikamatwa miezi michache baada ya Mapinduzi ya Januari
12, 1964 kwa tuhuma za kutaka kuipindua serikali mpya ya Karume. Alitiwa
kizuizini na hatimaye kuuawa bila ya kushitakiwa.
Imeelezwa kuwa Luteni Hamud alifahamu juu ya kuuawa kwa baba yake
miaka michache baadaye akiwa katika mafunzo ya kijeshi huko Tashkent,
Urusi ya zamani. Inasemekana alitamka kwa kuapa kwamba, punde
atakaporejea Zanzibar, angemuua Karume kulipiza kisasi cha kifo cha baba
yake.
Kwa kupitia majasusi waliokuwa wanasoma na Hamud huko masomoni, yapo
madai kuwa serikali ya Karume ilijulishwa juu ya kusudio la Hamud la
kumuua Rais Karume, lakini haikuchukua hatua hata baada ya mwanajeshi
huyo kurejea Zanzibar.
Badala yake, Karume alimpandisha cheo kuwa luteni katika sherehe
iliyohudhuriwa na wakuu wa vikosi vyote vya ulinzi na usalama Zanzibar.
Je, taarifa juu ya ‘tamko’ la Luteni Hamud huko Tashkent juu ya
dhamira yake ya kutaka kumuua Karume zilikuwa za uongo? Kwa
alichokifanya ni dhahiri kwamba kilichosemwa na shushushu juu ya jambo
hilo ni sahihi.
Mara baada ya Karume kuuawa , Hayati Thabiti Kombo Jecha aliyekuwa
Katibu Mkuu wa ASP na mmoja wa waliojeruhiwa vibaya katika shambulio la
kumuua kiongozi huyo wa nchi amenukuliwa na Minael Hossana Mdundo
katika kitabu chake cha Masimulizi ya Sheikh Thabit Kombo Jecha (Uk.
157/8) akieleza: “Mara ikapigwa risasi kutoka mlangoni, ikampiga
Mheshimiwa Sheikh Karume shingoni. Hapo hapo akaanguka akisema;
“Hamad”… bahati mbaya risasi zote alizopigwa zilimpiga sehemu mbaya”.
