Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na
Teknolojia, January Makamba amesema kuwa anatafakari iwapo awanie urais
katika Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na kuwapo kwa watu wengi hasa
ndani ya CCM, wanaomtaka kugombea nafasi hiyo ya juu ya uongozi wa nchi.
Makamba ambaye pia ni mjumbe wa
Halmashauri Kuu (NEC) ya CCM alisema: “Kwanza ni kweli kwamba kuna
ushawishi kuhusu suala hilo kutoka kwa vijana walioko nje na ndani ya
chama, wanataaluma, baadhi ya wazee na watu wengine iwe kwa makundi au
mtu mmoja mmoja wamekuwa wakinishawishi kugombea kwa muda sasa.”
Aliongeza: “Mwanzoni sikuona uzito sana,
yaani sikuzingatia sana, lakini kwa kadiri siku zinavyokwenda ni kwamba
ushawishi umekuwa mkubwa na hivyo niseme ni jambo ambalo sasa
ninalitafakari kwa kina”.
Alisema ikiwa ataamua kuwania urais,
atafanya hivyo wakati mwafaka kwa kuzingatia utaratibu utakaowekwa na
chama hicho, lakini akasema kwa sasa si wakati wake. Makamba alikuwa
akijibu hoja za gazeti hili lililotaka ufafanuzi wake kutokana na kuwapo
kwa taarifa kwamba ameanza harakati za kuusaka urais katika Uchaguzi
Mkuu wa 2015.
Gazeti hili lilidokezwa kuwa hatua yake
hiyo imemwingiza katika mvutano usio rasmi na wanasiasa ambao tayari
wameonyesha nia ya kuwania nafasi hiyo ya juu ya uongozi nchini,
wakiwamo wale wa kambi ya urais aliyokuwa akidaiwa kuwa mmoja wao.
Awali iliaminika kuwa Makamba alikuwa
katika kambi ya Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, lakini wachambuzi
wa masuala ya kisisa wanasema ‘katika siku za karibuni mwenendo wake
unaashiria kwamba si mmoja wa wanaomuunga mkono kiongozi huyo, bali ni
mtu mwenye mipango yake binafsi ya kisiasa”.
