WAKATI
Jeshi la Polisi likiendelea kukwepa kumkamata Mbunge wa Urambo
Magharibi, Prof. Juma Kapuya (CCM) anayekabiliwa na tuhuma za kumbaka
mwanafunzi na kutishia kumuua, uongozi wa Bunge umeingilia kati ukitaka
achukuliwe hatua.
Chama Cha Mapinduzi (CCM) nacho kimeibuka na kueleza kushangazwa na
kitendo cha mbunge huyo kuikana namba yake ya simu 0784 993 930 wakati
ipo hata kwenye kitabu cha wageni cha chama hicho alichokisaini mwenyewe
mkoani Dodoma.
Prof. Kapuya ambaye amewahi kushika nyadhifa kadhaa za uwaziri katika
Serikali ya Awamu ya Tatu na Nne, tayari amefunguliwa jalada namba
OB/RB/21124/13 katika Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Salaam,
tangu Novemba 24 mwaka huu.
Jalada hilo lilifunguliwa na mwanafunzi huyo anayedaiwa kubakwa na
kutishiwa kuuawa, lakini Jeshi la Polisi limekuwa likishughulikia suala
hilo katika namna ya kumlinda mtuhumiwa.
Siku moja baada ya jalada hilo kufunguliwa, Kapuya alidaiwa kutimkia
nchini Sweden, lakini taarifa za uhakika zinasema kuwa alirejea nchini
Alhamisi na amekuwa akiishi kwa kujificha huku polisi wakidai kuendelea
kumsaka.
Ni katika danadana hizo, uongozi wa Bunge umesisitiza kuwa suala hilo ni jinai na linapaswa liende katika mkondo wa kisheria.
Akizungumza na gazeti hili wiki hii, Katibu wa Bunge, Dk. Thomas
Kashililah, alikiri kulifahamu jambo hilo akisema kuwa walipomsikiliza
mtoto huyo waliona ni suala ambalo linahitaji kushughulikiwa kisheria
kwa kuwa ni jinai.
“Suala la binti huyo lilifikishwa kwangu kupitia msaidizi wangu
ambaye alisikiliza hoja na rai yake na kushauriwa kuwa hilo ni suala la
jinai na linapaswa liende katika mkondo huo.
“Hata hivyo, binti huyo alitambulishwa kwa spika kama kiongozi wa
wabunge na kuelekeza kuwa tumshauri alifikishe katika mamlaka husika,”
alisema Dk. Kashililah.
Chanzo chetu cha habari kilithibitisha kuwa binti huyo alikutana na
Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Oysterbay (OCD) na OC-CID wake na
kutoa maelezo ya awali kabla ya viongozi hao kumruhusu ayaweke
malalamiko yake katika maandishi kwa ajili ya kufunguliwa mashtaka.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alikiri polisi
kufungua jalada hilo na kuongeza kwamba hivi sasa wanafanya uchunguzi
kubaini kama ujumbe ulio katika simu ya binti anayedai kubakwa na
kutishiwa maisha unatoka katika simu ya mbunge huyo.
Lakini tangu kufunguliwa kwa jalada hilo, mtuhumiwa huyo ameendelea
kubaki uraiani bila kuhojiwa, huku akiendelea kuwapa vitisho watoto hao,
kusafiri nje ya nchi na kurejea kupitia Uwanja wa Ndege wa Julius
Nyerere bila kukamatwa.
Awali Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
alipoulizwa kuhusu suala hilo, alisema hawana shamba mjini, kazi yao ni
kukamata wahalifu na kuwa wangemsaka popote mtuhumiwa huyo ikiwa
taarifa itafikishwa rasmi polisi.
Kwa siku tatu sasa jeshi hilo limekuwa likitupiana mpira kuhusu kumkamata na kumhoji mtuhumiwa huyo.
Wakati Kamanda Wambura akijitetea kuwa yuko mkoani Arusha, Kamishna
Kova naye anadaiwa yupo nchini China, huku Kaimu Mkurugenzi wa Makosa ya
Jinai nchini, Isaya Mungulu akisema hadi jana alikuwa hana taarifa,
hivyo kuomba muda zaidi ili leo aweze kutolea ufafanuzi.
Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kuwa Mungulu alikuwa na taarifa
tangu Kapuya anarejea nchini akitokea nje kwa ndege ya Shirika la Qatar
ingawa yeye hakuwa tayari kufafanua suala hilo.
CCM wamuumbua
Kada wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Mkoa wa Dodoma ambaye aliomba
kuhifadhiwa jina, amemuumbua Prof. Kapuya akisema namba ya simu
aliyoikana na kudai kuwa alishaigawa miezi sita iliyopita ndiyo hiyo
aliiandika mwenyewe kwenye kitabu cha wageni.
Akiwa mjini Dodoma kama kamanda wa UVCCM, Kapuya alitembelea tawi
moja na kusaini kitabu cha wageni ambapo mwisho wa saini yake aliandika
namba hiyo ya simu ambayo pia imeandikwa kwenye kitabu cha orodha ya
wabunge.
Kada huyo alisema kuwa alishitushwa kusikia Prof. Kapuya anaikana
namba 0784 993 930 ambayo imekuwa ikiandikwa na gazeti hili kuwa ndiyo
imekuwa ikitumika kutuma ujumbe wa vitisho kwa binti anayedaiwa kumbaka.
Alisema kuwa anampa ushauri wa bure Prof. Kapuya asijaribu
kujiaibisha kwa kuikana namba hiyo kwa sababu hata kwenye moja ya vitabu
vya wageni aliiandika na kusaini kwa mkono wake.
“25.6.2013 Alhaj Prof. Juma Athuman Kapuya, Mbunge wa Urambo
Magharibi, Mjumbe wa NEC-CCM Taifa, Kamanda wa UVCCM (M) Tabora, Makamu
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Juhudi zako
zibarikiwe na Mungu 0784993930 CCM Oyee,” aliandika Kapuya katika kitabu
kile.