UTAMADUNI mbovu ulioanza kujitokeza kwa baadhi ya wabunge kuonesha
kukosa nidhamu, umeandaliwa kanuni mpya ambazo pamoja na mambo mengine,
zitadhibiti matukio hayo na kuadhibu wahusika.
Taarifa zilizofikia
gazeti hili zimeeleza kuwa Rasimu ya Mwongozo wa Kanuni za Maadili ya
Wabunge wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyotoka mwishoni mwa wiki,
imebainisha namna Bunge litakavyodhibiti matukio hayo.
Udhibiti Kwa mujibu wa mtoa habari wetu kutoka miongoni mwa wabunge,
rasimu hiyo imewabana wabunge kutofanya vurugu kwa kuzomea au vinginevyo
kunakoweza kusababisha shughuli za Bunge kusitishwa.
Ili kudhibiti kutokea vurugu bungeni, mtoa habari wetu ameeleza kuwa
Spika amepewa madaraka ya kuahirisha shughuli za Bunge bila hoja yoyote
kutolewa ili kupisha muda wa kudhibiti vurugu hizo.
Ingawa rasimu
hiyo haikutamka adhabu kwa wabunge watakaokutwa na hatia, mtoa habari
wetu amesema Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, imepewa nguvu
ya kujadili watuhumiwa na kutoa ushauri kwa Spika kuhusu hatua zaidi.
Kuwepo
kwa rasimu hiyo kumetokana na mapendekezo ya Kamati ya Haki, Maadili na
Madaraka ya Bunge, ambayo mwaka jana ilipendekeza wabunge watungiwe
kanuni zinahohusu maadili.
Katika mapendekezo ya kamati hiyo, waliomba uwepo wa kanuni
zitakazoweka viwango kwa mienendo ya wabunge pale watakapokuwa
wakitekeleza majukumu yao ya kibunge wawapo nje na ndani ya eneo la
Bunge.
Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mbunge wa Mlalo, Brigedia mstaafu Hassan
Ngwilizi (CCM), alisema katika taarifa ya mapendekezo hayo kuwa uzoefu
unaonesha baadhi ya mabunge katika Jumuiya ya Madola, tayari wana kanuni
za maadili na mwenendo wa wabunge.
Alisema pia kuna utafiti umefanyika ulioonesha kwa kiasi fulani
kuwepo kwa kanuni hizo, kunaongeza imani ya wananchi kwa mabunge yao.
Hivi sasa maadili ya wabunge yanasimamiwa na Sheria ya Maadili ya
Viongozi wa Umma, ambayo imeelezwa kwamba kwa madhumuni ya usimamizi
bora wa maadili ya wabunge, sheria hiyo haikidhi mahitaji kama ikiachwa
itumike peke yake.
Kamati hiyo ilieleza kuwa kuwepo kwa mwongozo wa
kanuni za maadili kwa wabunge, kutawafanya wabunge hao kuonesha viwango
vya juu vya maadili, katika kutekeleza majukumu yao kwa umma hususani
wanapokuwa wakiisimamia Serikali.
Hata hivyo, mtoa habari wetu
alisema kanuni hizo hazitahusisha maisha binafsi ya mbunge, familia yake
au pale anapotoa maoni yake ya kisiasa kwa kuzingatia kuwa yeye ni
mwanachama wa chama cha siasa.
Kwa mujibu wa mtoa habari wetu, kanuni hizo pia hazitawahusu wabunge ambao ni mawaziri wanapotekeleza majukumu yao.
Chanzo
kingine cha habari kimebainisha kuwa huenda rasimu hiyo ikajadiliwa
wiki hii, kama Kamati ya Uongozi ya Bunge ambayo ndiyo yenye mamlaka ya
kupanga shughuli za Bunge, ikiamua hivyo.
“Rasimu imetoka ni kweli na inaweza kujadiliwa bungeni iwapo Kamati
ya Uongozi itaona inafaa kwenye bunge hili, wabunge wanachopaswa kufanya
ni kutoa maoni na mapendekezo yao au kuongeza jambo, lakini hawawezi
kukataa kuipitisha. “Mwongozo huo ni mzuri … wabunge wanaofuata maadili
watafurahi uwepo wa kanuni hizo za wabunge, lakini kwa wale wasiofuata
maadili wanaweza kuona ni kero kwako, lakini rasimu ni nzuri,” alieleza
mtoa habari huyo.