KWELI huu ni unyama wa wanaume hata kama si
wote! Wanawake wawili wakazi wa maeneo tofauti jijini Dar es Salaam, wamepoteza
maisha kufuatia madai ya kuuawa na waume zao. Inauma sana na Uwazi ndilo lenye
mkasa mzima!

Matukio yote mawili yametokea jijini Dar es
Salaam na kuacha vilio kwa ndugu na jamaa wakiwa hawaamini kilichowakumba
wapendwa wao.
WALIOTENDWAWanawake waliojulikana kwa majina ya
Mwanahamisi na mwenzake Waisiko Robert Mtundi ndiyo waliodaiwa kuuawa na waume
zao, kisa kikubwa kikidaiwa ni hofu ya wanaume hao kusalitiwa katika mapenzi.
Juma Shaban, mkazi wa Manzese Kwamfuga Mbwa na Samuel Gesire
Mlimi, mwenye makazi yake Msongola, maeneo yote hayo yapo Dar ndiyo wanaodaiwa
kutekeleza ukatili huo wenye kutoa machozi mpaka basi.
MWANAHAMISI ALIVYOUAWA
Ilikuwa saa tatu usiku, Septemba 21, mwaka huu, kila familia ya
eneo la Kwamfuga Mbwa ilikuwa ndani kwa chakula cha usiku au maandalizi ya
kulala, ndipo waliposikia zogo kutoka ndani ya chumba cha kwa wanandoa hao.
ZOGO NA MANENO
Kwa mujibu wa majirani hao waliozungumza na gazeti hili baada ya
tukio, zogo hilo liliambatana na maneno ya shutuma kutoka kwa Juma kwamba mkewe
huyo si mwaminifu ndani ya uhusiano wao.
Majirani walisema shutuma za Juma ziliambatana na kelele za
Mwanahamisi kuomba msaada akisema ‘nauawa jamani! Nauawa mwenzenu!’
Wakasema baada ya kama saa moja ya mzozo ulipita ukimya, ndipo
kila jirani alitoka nje na kuulizana nini kinaendelea ndani ya chumba cha
Mwanahamisi na mumewe!
“Baada ya dakika kumi, tulimwona Juma akitoka chumbani kwake
huku akiwa anabofyabofya simu yake ya mkononi na kutokomea kusikojulikana,”
alisema jirani mmoja huku macho yakiwa yamevimba kwa sababu ya kumlilia
Mwanahamisi ambaye wakati huo alikuwa chini ameshakata roho.
Akaendelea: “Baada ya Juma kuondoka tulipatwa na wasiwasi,
tukaenda kumwangalia Mwanahamisi chumbani na kumkuta hajitambui, amelala
kifudifudi, ana majeraha sehemu mbalimbali za mwili huku akiwa ametapakaa damu.
Alikuwa akipumua kwa mbali.
“Alikuwa hawezi kuongea vizuri, mimi nilimsikia akisema hana uhai
tena, tumwombee mtoto wake. Ndani ya chumba tuliona viroba vya pombe kali na
kisu kikiwa kimelowa damu, nahisi ndicho alichotumia Juma kufanyia ukatili
wake.
“Tuliamua kumwahisha hospitali Mwanahamisi lakini kutokana na
hali yake tuliona ni vizuri kuwasiliana na polisi ambao walifika baada ya muda.
“Lakini siku yake Mwanahamisi ilitimia kwani wakati polisi
wakijiandaa kumchukua kumkimbiza hospitali aliaga dunia.”
KUMBE NI MWEZI MMOJA BAADA YA KUHAMIA
Wengine waliozungumza na gazeti hili siku ya tukio huku wakitoa
machozi, walisema Juma ambaye alitoroka baada ya ukatili huo, alihamia kwenye
nyumba hiyo mwezi mmoja nyuma lakini walipata umaarufu mtaani hapo kutokana na
tabia yao ya kupigana mara kwa mara.
MJUMBE WA MTAA NAYE ANENA
Akizungumza na gazeti hili katika eneo la tukio, Mjumbe wa
Nyumba Kumi, Techla Tesha aliwalaumu majirani na wapangaji wa nyumba hiyo kwa
kushindwa kumpelekea taarifa mapema huku wakijua mtuhumiwa alikuwa na tabia ya
kumpiga mkewe mara kwa mara.
WAISIKO ALIVYOUAWA
Awali ya yote, inadaiwa Waisiko ni mke mkubwa, mke mdogo jina
lake halikupatikana mara moja.
Siku ya tukio, saa tatu usiku inadaiwa Samuel alikwenda nyumbani
kwa Waisiko ambapo si mbali sana na nyumbani kwa mke mdogo na kuangusha
timbwili zito.
“Samuel aliingia ndani na kuanza kumpiga mkewe mkubwa huku
akionya majirani kuwa asiwepo mtu wa kwenda kuamua ugomvi wao.
“Sisi kama majirani tuliogopa kwa sababu Samuel alikuwa
akitishia kuwa atakayeingia atamchoma kisu.
“Licha ya vitisho hivyo, tulisimama nje ya chumba chao huku
vitisho vikiongezeka lakini namna ya kutoa msaada tulishindwa. Hatukujua chanzo
cha ugomvi wao.
“Kauli za mwanamke kila wakati ziliashiria alichokuwa akitendwa
kwa wakati huo, mfano kuna wakati tulimsikia akisema anavunjwa mgongo, akasema
anang’olewa kucha. Pia kuna muda alilalamikia kuvunjwa mkono. Jamani, marehemu
aliteswa sana kabla ya kufariki dunia,” alisema shuhuda mmoja.
NI MATESO YA USIKU KUCHA!!
Shuhuda huyo aliongeza: “Mateso ya mwanamke huyo huenda yalikuwa
ya usiku kucha kwani nakumbuka mpaka alfajiri ndipo tukasikia sauti ya mwisho
ya Waisiko akisema Samuel umeshaniua, nimalizie kabisa basi. Baada ya hapo
hatukusikia tena sauti wala vurugu.
SERIKALI YA MTAA YAZUNGUMZA
Makamu Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Msongola, Juma Chacha
alipohojiwa kuhusiana na mauaji hayo, alisema ana taarifa lakini mtuhumiwa
alikimbia baada ya kutenda unyama huo na anatafutwa na polisi.
UWAZI LABAINI KISA
Uchunguzi wa gazeti hili ulibaini kuwa chanzo cha ugomvi huo ni wivu
wa mapenzi kwani ilidaiwa kuwa Samuel alikuwa akimhisi mkewe huyo kutoka nje ya
ndoa.
Chanzo chetu kilisema siku ya tukio, Samuel aliwachukua baadhi
ya marafiki zake na kwenda nao baa ambako aliwaambia kuwa anahisi mkewe huyo
ana jambo kwani akimuuliza kitu anamjibu jeuri.
Mtoa habari wetu alisema Samuel akiwaambia marafiki hao kwamba
siku hiyo akirudi nyumbani, mwanamke huyo atamtambua.
POLISI WALIVYOIKUTA MAITI
Polisi walipofika na kuichunguza maiti waliikuta imevunjwa mkono
wa kushoto na kung’olewa kucha za miguu huku uti wa mgongo nao ukiwa
umevunjika.
Habari zinasema mara baada ya mtuhumiwa kufanya mauaji hayo,
alikwenda kwa mkewe mdogo na kumtaka akamuone mke mwenzie, alipokwenda yeye
nyuma akatoroka.
Polisi Mkoa wa Ilala tayari wamemfungulia jalada mtuhumiwa huyo
lenye namba STK/RB/10058/2013 MAUAJI.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ilala, ACP Marietha Minangi
amethibitisha kutokea kwa mauaji hayo