Search in This Blog

WANASAYANSI WAGUNDUA KIFAA CHA KUMUAMRISHA MBWA (REMOTE CONTROL’)


NOOR SHIJA 
Wanasayansi katika kurahisisha shughuli za binadamu wamevumbua kifaa cha kutoa amri kwa masafa ya mbali kwa ajili ya mbwa (remote control) na hasa kwa mbwa wanaotumika kwenye shughuli za uokoaji yanapotokea majanga ya asili na wale wanaotumwa kusaka vitu haramu vilivyofichwa kwenye maeneo yasiyofika kwa urahisi na binadamu.
Mbwa hutumiwa na binadamu kwa shughuli mbalimbali, zikiwamo za kiaskari ambapo vyombo vya usalama hutumia mbwa kubaini vitu vya hatari, uokoaji hasa panapotokea tetemeko la ardhi na watu kufukiwa na kifusi, ulinzi na wengine humtumia kama rafiki kwa kuzurura nao mitaani.
Kifaa hicho kilichowekwa mfumo wa GPS (Global Positioning System) unaotumia mawasiliano ya satellite, huvikwa mgongoni mwa mbwa na kumwezesha mmiliki wake kutoa amri akiwa masafa ya mbali.
Wanasayansi wa Chuo Kikuu cha Auburn kilichopo Alabama, Marekani, wamefanya utafiti huo na kuvumbua kifaa hicho kwa ajili ya kuwasaidia polisi wa kikosi cha mbwa kufanya kazi zao kwa urahisi na bila kulazimika kuongozana na mbwa wao kila mahali.
Kifaa hicho kilichojengwa kwa kuwekwa GPS, kinafungwa mgongoni mwa mbwa na kinaelekeza kwa kutoa ishara mbili ambazo ni kutikisika na kutoa sauti, na zote hizo mbwa anakuwa amefundishwa namna ya kuzitii.
Wanasayansi wametengeneza kifaa hiki hasa kwa matumizi ya vyombo vya usalama, ambao mbwa kwao ni askari mwenza. Kwa Marekani, GPS ilitengenezwa kwa madhumuni ya kijeshi, lakini kwa miaka 1980 ilianza kutumika kwa shughuli za kiraia.
Mbwa anapofungwa kifaa hicho ambacho kinatumia mawimbi kama yale ya simu za mkononi au redio, hupokea amri kutoka kwa bosi wake ambapo wanasayansi wamethibitisha kuwa utendaji kazi wa kifaa hicho uko kwa asilimia 97.
Wanasayansi wamesema kifaa hicho licha ya kuwasaidia wanausalama, pia kina uwezo wa kutumiwa na mtu mwenye mbwa wake nyumbani, ambapo anaweza kumuachia akazurure mitaani na anaweza kumwamuru arejee nyumbani wakati wowote anapotaka.
Kwa mujibu wa watafiti wa Chuo Kikuu cha Auburn, kifaa hicho kinatoa sauti maalumu ambayo hufunzwa mbwa namna ya kuitii. Kimetengenezwa maalumu kwa polisi wa kikosi cha mbwa, waongozaji na kikosi cha uokoaji na kwa vitendo vyote hivyo usahihi wa utii ni asilimia 97.
Wanasayansi Jeff Miller na David Bevly ambao ndiyo wavumbuzi wa kifaa hicho, walikuwa na mawazo tangu mwanzo kusaidia namna ya kuongoza mbwa kwa masafa marefu bila mmiliki kulazimika kuwa jirani naye.
Kwa mujibu wa wanasayansi Miller na Bevly kifaa hicho si cha kumwelekeza tu mbwa eneo la kwenda, pia kinatuma ujumbe kumweleza muongoza mbwa kama kuna kitu kimegunduliwa.
Wanasayansi hao wanasema kina uwezo wa kupiga na kutuma picha na kumwezesha mmiliki kujua kilichogunduliwa na mbwa.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger