Dk Msafiri alisema hayo akizungumza na waandishi wa habari waliotaka kupata maelezo zaidi kuhusu matumizi ya kituo hicho ambacho kimewekwa kwa ajili ya kutoa huduma za haraka kwa wanawake wanaopata matatizo ya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo kubakwa au kulawitiwa.
Alisema kituo hicho kinatumika vibaya kinyume na malengo yake ambapo wazazi wanawalazimisha watoto wa kike kuchunguzwa bikira yao baada ya kuwatilia shaka kwamba wanayo mahusiano ya kimapenzi na wanaume.
“Kituo hiki Mkono kwa Mkono malengo yake ni kutoa huduma za dharura kwa wanawake wanaokabiliwa na matukio ya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo kubakwa.....sasa wazazi wanawaleta watoto wao hapa baada ya kuwatilia shaka kwamba wanamahusiano ya kimapenzi na wanaume kwa ajili ya kuchunguzwa kujua ubikira wao,” alisema.
Alisema huo ni aina mpya ya udhalilishaji wa kijinsia kwa sababu wanawake wengi wanapinga kuchunguzwa ubikra huo ambapo kazi hiyo inafanyika kwa nguvu kwa maelekezo ya wazazi tu.
Aidha alisema kituo hicho kinakabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo ukosefu wa madaktari wa kufanya vipimo na kuchunguza matukio ya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo kubakwa au kuchunguza ubikra ambapo kazi hizo hufanywa na madaktari wanaume.
Kituo cha Mkono kwa Mkono kilifunguliwa miaka miwili iliyopita ambapo lengo lake kubwa ni kurahisisha kupatikana kwa huduma zote katika kituo kimoja za matukio ya udhalilishaji wa kijinsia ikiwemo matukio ya ubakaji.
Kituo hicho kinachotoa huduma zake katika Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja mjini hapa kinatoa huduma zake kwa ushirikiano mkubwa wa mashirika ya kimataifa yanayoshughulikia afya na maendeleo ya mtoto na mwanamke ikiwemo UNFPA na UNICEF.