MMOJA wa mawaziri wa Serikali ya Awamu
ya Tatu na mbunge anayetoka Mkoa wa Tabora, anatuhumiwa kumbaka na kisha
kutishia kumuua msichana yatima mwenye umri wa miaka 16 (jina
limehifadhiwa) anayesoma Shule ya Sekondari Turiani iliyoko Magomeni
jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo (jina lake linahifadhiwa kwa
sasa), ametoa tishio hilo la mauaji kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia
namba iliyosajiliwa kwa jina lake kwa kile alichodai kukaidi amri ya
kutaka wasifichue uchafu wake kwa waandishi wa habari.
Akizungumza kwa uchungu na mwanafunzi
huyo alisema kuwa waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii
iliyoko jijini Dar es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho
katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012.
Mwanafunzi huyo alisema alifikwa na
ukatili huo alipoitwa na kiongozi huyo kwenda kuchukua fedha za ada na
matumizi mengine, ambapo mara ya kwanza alimpa sh 700,000 na mara ya
pili sh 350,000.
Yatima huyo anayeishi na dada yake,
alikutanishwa na waziri huyo wa zamani na baba wa mwanafunzi mwenzake,
kutokana na msaada mkubwa aliompa akiwa mgonjwa, ili aweze kumsaidia
fedha za ada kama ishara ya shukurani.
Mwanafunzi huyo alisema baada ya
kutambulishwa, aliitwa katika hoteli hiyo ambako baada ya kufika
mapokezi wafanyakazi walimkataza kuingia chumbani kutokana na umri wake
kuwa mdogo (mwaka 2011 alikuwa na miaka 14), lakini waziri huyo wa
zamani aliamrisha aruhusiwe.
Akiwa chumbani, mwanafunzi huyo
alilazimishwa kulala naye kisha kumpa sh 700,000, badala ya shilingi
67,000 alizohitaji kwa ajili ya ada.
Mwanafunzi huyo alisema baada ya muhula
mmoja aliitwa tena na kiongozi huyo katika Jengo la Biashara Complex
lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012, ambapo pia alimlazimisha kulala naye
kwenye zulia la ofisi yake, kisha kumpa sh 350,000.
Mwanafunzi huyo alisimulia kwamba wakati
anatoka kwa huzuni ofisini kwa mbunge huyo, mmoja wa wahudumu
alimuuliza sababu ya huzuni yake na akalazimika kumweleza kisa hicho,
ndipo mhudumu alitokwa machozi huku akimwambia kwamba, atakufa kwa
sababu “baba huyo ni muathirika wa ukimwi”.
Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa vile
alilia na kufanya fujo hapo mapokezi, hadi alipokamatwa na walinzi,
kisha kupelekwa kituo cha polisi kufunguliwa mashitaka.
Hata hivyo, alisema polisi
waliposimuliwa kisa chote, walilazimika kumwita waziri huyo wa zamani na
alipofika alikiri na kuomba mambo yaishie hapo.
“Alikubali na akaahidi kunilipia ada na
pesa za matumizi kiasi cha sh 300,000 kila mwezi, jambo ambalo amekuwa
akilitekeleza kupitia simu yake ya mkononi (namba za simu tunazo),”
alisema.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, Januari
24, mwaka huu walitishiwa maisha na kiongozi huyo, lakini mwezi
uliofuata, mtu asiyefahamika alienda nyumbani kwao na kuacha gari (namba
tunazo) aina ya Mercedes Benz yenye rangi ya bluu wakati akiwa shuleni,
kisha kuacha ufunguo kwa jirani yao kwa maelekezo kuwa akifika apewe.
Wamesema baadaye kiongozi huyo
aliwapigia simu kuwaarifu kuwa amempa zawadi ya gari kwa ajili ya
matumizi, na wanaruhusiwa kuliuza ili wapate pesa za mahitaji yake siku
zilizosalia, kwani baada ya uchaguzi mkuu 2015, atakuwa Waziri Mkuu,
hivyo itakuwa ngumu yeye kumtumia huyo binti pesa kama alivyoelekezwa na
Jeshi la Polisi kituo cha Oysterbay.
Hata hivyo, wasichana hao walishindwa kulitumia gari hilo hivyo kutoa taarifa polisi ili kesi ipelekwe mahakamani.
Wamedai kuwa polisi walikubali
kulipeleka tatizo hilo kwa katibu wa Bunge, ambaye alimwita mwanafunzi
huyo na nduguye Dodoma kukutana na Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge.
Hata hivyo, walipofika Dodoma hawakuweza
kupata ufumbuzi kwa maelezo kuwa waziri huyo wa zamani hakuwepo hadi
Bunge lilipoisha. Kwa muda wote, wasichana hao walisema waligharimiwa
kila kitu na Ofisi ya Bunge.
Kabla ya kurudi Dar es Salaam, mabinti
hao walisema waliitwa na kiongozi mmoja wa juu wa CCM aliyewalekeza
kwenda kumwona Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Kwa mujibu wa mawasiliano, kiongozi
mwingine (jina tunalo) alimpigia binti huyo simu majira ya asubuhi,
akimtaka aende ofisi za CCM, lakini hakupata msaada wowote zaidi ya
kuombwa asubiri hadi wakati wa kipindi cha Bunge ili apate msaada kwa
kuwa ni suala binafsi.
Hata hivyo, wakati akiwa njiani kuelekea
katika kituo kimoja cha runinga kwa ajili ya kutoa kilio chake,
mwanafunzi huyo na dada yake walifuatiliwa na watu wasiowajua, jambo
lililowalazimisha kuomba msaada wa wapita njia.
Hata alipofika katika ofisi za kituo
hicho cha runinga, watu watatu akiwemo mwanamke mmoja walifika wakidai
kuwa ndugu wa wasichana hao na kuwakataza waandishi wasikubali
kusikiliza neno lolote, wakati sio kweli.
Aidha, walitumiwa ujumbe kutoka katika
namba ya mmoja wa wafanyakazi wa makao makuu ya CCM, akiwasihi kufumba
mdomo kwa kuwa anawapenda na hataki wadhurike.
Baada ya jitihada za kuwanyamazisha
wasichana hao kushindikana, ndipo mwathirika alipoanza kupokea ujumbe wa
kutishia maisha kupitia katika namba ya simu ya 078499….
Ikisema: “Waandishi hawatakusaidia
kamwe, Bunge la Katiba likianza watu watakusahau kama uliuawa.
Mtasahaulika kabisa, subirini mje mzikwe leo usiku kwenu, sitanii,
hakuna wa kunifanya lolote, serikali ndio sisi, salini kabisa.”
Jitihada za kumpata waziri huyo wa
zamani na mbunge wa CCM, ziligonga mwamba. Mara ya kwanza simu yake moja
ilipokelewa na mtu aliyejitambulisha kama dereva wake, na akataka
aambiwe sababu za kumuhitaji kiongozi huyo.
Hata aliposisitizwa kuwa anayehitajika
ni mkubwa wake, alitoa namba nyingine ya kumpata, lakini ilikuwa
ikikatwa mara zote ilipokuwa ikiita.
Mbali ya ujumbe huo wa vitisho, binti
huyo alikuwa akitumiwa ujumbe mbalimbali na watu asiowafahamu, na
wengine kumpigia simu wakimwambia wanajua amejificha wapi na kwamba
hawezi kutoka.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai,
alipoulizwa kuhusiana na tuhuma hizi nzito, alionyesha kushangaa na
kuhoji; “na wewe umeanza kuandika mambo kama haya?”
“Hilo ni jimbo binafsi zaidi na mimi siwezi kuongea lolote,” alisema na akakata simu.
Tanzania Daima Jumatano, liliwasiliana na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, ambaye anadaiwa kulielewa vema suala hilo.
Shelukindo, hata hivyo, licha ya
kukubali kuwa alikuwa anajua tatizo hilo, aliomba asiongee kwa kirefu
kwa madai kuwa alikuwa kwenye kikao.
Kamanda wa zamani wa polisi Mkoa wa
kipolisi wa Kinondoni, Charles Kenyela alipulizwa namna
alivyoshughulikia jambo hilo, alikana kujua chochote kwa madai kwamba,
mambo kama hayo yanashughulikiwa na dawati maalumu.
CHANZO NI TANZANIA DAIMA
