SERIKALI inatarajia kutoa ajira 800,000 kwa vijana kuanzia mwakani
kuliwezesha kundi hilo kuondokana na utegemezi katika jamii na kuchangia
uchumi wa nchi.
Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kongamano la
taifa la ajira, Makamu wa Rais, Dk. Gharib Mohamed Bilal alisema
programu hiyo itatekelezwa kwa awamu na awamu ya kwanza ya miaka mitatu
itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015.
Licha ya uchumi kukua kwa kiwango cha kuridhisha cha asilimia 6.5
kwa mwaka, bado kasi hiyo haijaweza kuzalisha ajira ya kutosha
ikilinganishwa na idadi ya wanaoingia katika soko la ajira, alisema.
Alisema
soko la ajira nchini lina uwezo wa kuzalisha ajira 300,000 kwa mwaka
katika sekta rasmi ikilinganishwa na wastani wa wahitimu 600,000 hadi
800,000 wanaoingia katika soko la ajira nchini.
“Vijana
wasiofanya kazi wanaongeza utegemezi katika jamii na familia na kuathiri
uchumi na wengine wanajiunga na makundi ya uchochezi na uvunjifu wa
amani.
“Wengine wanaweza kujiingiza kwenye vitendo vya wizi,
kutumia madawa ya kulevya na biashara ya ngono hivyo ni muhimu kwa
serikali na jamii kwa ujumla kuchukua hatua zitakazowezesha kuongeza
fursa za ajira kwa vijana kujiajiri au kuajiriwa,”alisema Dk. Bilal.
Hata
hivyo, alisema kati ya mwaka 2010 hadi 2013 ajira 610,285 zimepatikana
na kwamba kati ya hizo ajira 185,929 zilizalishwa kupitia miradi ya
uwekezaji 1,845 iliyosajiliwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).
Alisema
tatizo jingine linaloikabili sekta ya ajira nchini ni vijana kutoweza
kubaini fursa zilizopo na kuzitumia katika kujiajiri katika sekta
mbalimbali nchini na kuondokana na dhana ya kuwa ajira ni kuajiriwa.
Naye
Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema umeanzishwa a mtandao
utakaosaidia vijana kujifunza ni taaluma ipi inahitajika kwenye soko la
ajira.
-MTANZANIA