“MSEMO wa wahenga, hujafa Hujaumbika ulikuwa sahihi kabisa.
Wahenga waliona mbali, wanatakiwa kuheshimiwa kwani misemo yao inaishi
mpaka leo. Ni kweli binadamu kamili ni yule anayezikwa, kabla ya hapo
hujakamilika.
“Unaweza kuishi na viungo vyako vyote miaka hamsini, lakini siku ya
mwisho ukapata ajali, ukakatika mikono na kufa, pale ndiyo umeumbika
sasa,” ndivyo anavyoanza kusimulia Nhende Ng’wanandilima (35), mkazi wa
Kwimba, Mwanza ambaye amelazwa Jengo la Sewa Haji, Hospitali ya Taifa
Muhimbili, Dar baada ya sehemu ya uso wake kuliwa na fisi aliyedai ni
mtu aliyejibadili.
Akisimulia kwa majonzi tena akiwa hawezi kuzungumza sawasawa, kijana
huyo alisema tukio hilo lilitokea katika Kijiji cha Kibetelwa,
Nh’ungumalwa, Kwimba usiku wa Mei 10, 2012.
MKASA KAMILI
Akisimulia mkanda mzima wa tukio hilo, Nhende
anasema: “Siku hiyo nilitoka kilabuni kunywa pombe kidogo. Nikiwa njiani
narudi nyumbani sasa, nilipita kwenye pori la kijiji kile, ndipo ghafla
nilianguka na kukumbana na sura ya fisi akiwa mkali sana.
“Yule fisi bila kujali mimi ni binadamu, alianza kunitafuna sura bila
huruma. Alinitafuta sehemu za kuzunguka kinywa kama unavyoniona.
Lilikuwa jambo la ajabu sana kwangu.
“Wakati nikipigania maisha, fisi aliendelea kunila. Nikapiga kelele
za kuomba msaada kutoka kwa wanakijiji ambapo walifika na kunikuta
nikiendelea kupambana na yule fisi huku nikiwa nimelowa damu.
“Alikuwa
fisi mwenye nguvu za ajabu na hata ule woga tunaosema fisi anao
sikuuona. We fikiria, watu wamefika lakini fisi aliendelea kunitafuna
bila kuogopa.
“Ilibidi wanakijiji wafanye kazi ya ziada kunitoa katika miguu na
fisi ambapo sasa alikaribia kabisa kunila sehemu za siri kwani
alishafika huko. Nilikuwa hoi sana. Ndipo wanakijiji wakanichukua na
kunikimbiza Hospitali ya Rufaa Bugando (Mwanza) kwa matibabu zaidi,”
alisema kijana huyo.
IMANI YA FISI MTU
Hata hivyo, Nhende alisema kuwa anaamini fisi
aliyemfanyia kitendo kile ni binadamu aliyejigeuza kuwa mnyama huyo.
Anasema kuwa, si rahisi kwa fisi kumla binadamu, tena mtu mzima.
Alisema
vitendo vya watu kuliwa na fisi katika maeneo hayo vinasababishwa na
mambo ya kishirikina ambayo hayajapatiwa ufumbuzi kutokana na wahusika
kutojulikana.
Alioongeza kuwa, wapo binadamu ambao kama ana chuki au kisasi na mtu
anajigeuza fisi usiku na kumrarua kama alivyofanyiwa yeye na si ajabu
mtu huyo huyo akatokea hospitali kumjulia hali.
KWA MUJIBU WA MADAKTARI
“Nilipofikishwa
Bugando, madaktari mashuhuri wa masuala ya koo na mfumo wote wa ‘ogani’
za fahamu walijitahidi kunitibu lakini bila mafanikio. Nikaletwa hapa
Muhimbili ambapo pia imeshindikana, sasa natakiwa kupelekwa India kwa
matibabu zaidi.
“Wameniambia nikifika kule nitasukwa upya (plastic surgery) sehemu
zote nilizoliwa na fisi. Ninachoweza kusema ni kwamba, yule fisi
ameniharibia sana maisha, nina mke na watoto watano sijui nitawalisha
nini, nimekuwa kilema mimi. Nimekuwa nikipata maumivu makali, sikuwahi
kujua kama fisi anaweza kumla binadamu hivi.
KUHUSU KWENDA INDIA
“Kuhusu safari ya India, nimeahidiwa
kusafirishwa, lakini awali ya yote mimi mwenyewe natakiwa niwe na pesa
zangu zisizopungua shilingi milioni moja ili kukamilisha mipango ya hati
za kusafiria.
KAMA SI POMBE ANGEMSHINDA FISI
Nhende hakusita kuweka wazi kwamba,
ushauri wake kwa vijana ni kuepuka matumizi ya pombe kupita kiasi,
kwani anaamini kama asingekuwa amekunywa pombe angeweza kumshinda yule
fisi.
MSAADA ANAOUOMBA KWA WATANZANIA
Nhende ameomba walioguswa na tukio
lake wamsaidie kwa hali na mali ili aweze kukamilisha taratibu za
usafiri wa kwenda India. Walio tayari wamchangie kupitia namba za simu
+255 763 176454.