SHETANI anazidi kuuatamia ulimwengu! Mama mmoja aliyetajwa kwa jina
moja la Farida mkazi wa Mburahati jijini Dar, amejikuta kwenye wakati
mgumu baada ya kudaiwa kumuua mumewe aliyetajwa kwa jina la Amos Joseph
kwa kumpiga kwa kukombe kichwani, Ijumaa linaidondosha kama ilivyo.
Akisimulia mbele ya gazeti hili mkasa mzima, mtoa habari hii
aliyetajwa kuwa dada wa marehemu anayejulikana kwa jina la Khadija,
alisema siku ya tukio kaka yake aliamka asubuhi na kumuaga kuwa
anakwenda bondeni kwa mkewe (Farida) kwa kuwa walikuwa nyumba tofauti.
Aliongeza kuwa, muda mfupi baada ya kaka yake kuondoka nyumbani hapo,
wifi yake (Farida) alifika nyumbani hapo na kumwambia kuwa kaka yake
ameumia sana aende akamuone.
“Mimi nilimshauri ampeleke hospitali tu nikidhani ameumia kidogo, kwa
sababu wamekuwa na kawaida ya kupigana mara kwa mara na tulishawaonya.
Wifi aliondoka na mimi nikaendelea na shughuli zangu.
“Muda mfupi, uliingia ujumbe kwenye simu yangu ya mkononi ukisomeka
kuwa kaka yangu alikuwa amefariki dunia huku ujumbe huo ukinionya
kutolia ili nisimshitue mama,” alisema Khadija.
Dada mwingine wa marehemu aliyejulikana kwa jila la Christina,
alisema yeye aliwahi kufika nyumbani kwa Farida na kumkuta kaka yake
akiwa amelala chali huku damu zikimvuja, muda mfupi polisi waliwasili na
kufanya taratibu zote muhimu.
Marehemu Amoni alizikwa siku chache baada ya kufariki dunia kwenye
makaburi ya Mburahati City jijini Dar huku Farida akiwa mikononi mwa
polisi kwa upelelezi zaidi.
Gazeti hili linaipa pole familia ya marehemu na linamuomba Mwenyezi Mungu ailaze pema roho ya marehemu Amosi-Amin.