AMA KWELI MGANGA HAJIGANGI
WANAFUNZI
wanaosomea udaktari katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi
Muhimbili (Muhas) wanaishi katika mazingira hatarishi kwani wanaweza
kupata magonjwa ya mlipuko na yale ya kuambukizwa wakati wowote.
Uchunguzi uliofanywa na Operesheni Fichua Maovu (OFM) ya Global
Publishers ndani ya majengo ya chuo hicho yaliyo karibu na taasisi ya
mifupa (MOI), umegundua kwamba kwa miezi mingi, vyoo vinavyotumiwa na
wanafunzi hao vimejaa na kuziba kabisa, hali inayowafanya vijana hao,
licha ya kushindwa kupata huduma hiyo muhimu ya kibinadamu, pia kuwa
katika hatari ya kupatwa na magonjwa ya mlipuko.
“Hali ni mbaya sana hapa kwa kweli. Hatuna huduma ya choo kwa miezi
miwili hadi mitatu sasa, tunapobanwa na haja, hasa kubwa, hulazimika
kukimbilia Kariakoo kwenye vyoo vya kulipia, hapa hapafai,” mmoja wa
wanachuo hao aliiambia OFM na kuomba hifadhi ya jina lake.
Wanafunzi hao ambao walitoa ushirikiano wa kutosha kwa makachero
wetu, pia walisema majengo mengi yanayotumiwa kama mabweni yao ya
kulala, yamechakaa na hivyo kuwafanya wawe na hofu kubwa, kwani yanaweza
kuanguka wakati wowote.
OFM ilishuhudia ngazi za kushuka na kupanda, zinazozunguka nje ya
majengo hayo zikiwa zimechakaa vibaya huku vyuma vilivyowekwa pembeni
kwa ajili ya kujishikilia vikiwa vimemongonyoka. Ni hatari kama
likitokea tukio la ghafla, mfano wa moto, litakuwa ni jambo gumu kwao
kuweza kujiokoa kupitia ngazi za nje. Hata baadhi ya milango inayotokeza
nje ya ngazi hizo katika maghorofa hayo, imefungwa kutokana na ubovu.
Licha ya kero hizo, pia wanafunzi hao walilalamikia kitendo cha
kujazana kupita kiasi katika vyumba vyao vya kulala, kwani wamepangwa
hadi wanane katika chumba kimoja.
Baada ya kutoka kwenye chumba cha
madenti hao (majina tunayo) OFM ilitua kwenye jengo moja ambalo liliwahi
kulipuka kwa moto lakini bado limechakaa kutokana na kutofanyiwa
ukarabati.
MSEMAJI WA MUHIMBILI ABANWA, AKISALITI CHUO
Baada ya OFM kunasa uozo huo ndipo ilipoamua kuwasiliana na msemaji wa Muhimbili, Amiela Angelekera.
OFM: Habari za leo kiongozi?
AMINIELA: Salama tuu, za kwako? Samahani naongea na nani?
OFM: Unaongea na Operesheni Fichua Maovu ‘OFM’ ya Global Publishers.
AMINIELA: Ok, nikusaidie nini?
OFM:
Unafahamu kama vyoo vya hosteli ya wanafunzi vyote vimejaa? Je, kuna
mkakati wowote wa kurekebisha maana ni miezi mingi imepita.
AMINIELA: Mmmh..(anaguna kidogo) sijajua ni vyoo vipi, unatakiwa uwe
mwandishi mzuri wa taaluma yako unapozungumzia chuo, njoo twende wote
tukaone hivyo vyoo.
OFM: Taaluma ipi ambayo unadhani hawana OFM?
Tayari tumefika hapo na kujionea ubovu wa miundombinu ambayo
inahatarisha maisha ya wanafunzi na chuo kwa ujumla.
AMINIELA: Nimesema njoo ofisini kwangu, maana sipendi kuzungumza
kwenye simu ishu kama hizi, kwanza mimi sihusiki na chuo maana ni
taasisi nyingine.
OFM: Ok, kwa nini umelizungumzia suala hilo.
AMINIELA: Sihusiki na chuo, hiyo ni taasisi nyingine.
OFM: Ok, sawa kazi njema.