Baada ya tishio la kupelekwa kwenye Mahakama ya Kimataifa ya ICC, watu
watano wakiwemo wabunge watatu wa CCM wanaodaiwa kujihusisha na biashara
ya dawa za kulevya wamejisalimisha kwenye kamati ya kidini
inayojihusisha na maadili nje na ndani ya makanisa.
Katika mahojiano maalum na NIPASHE Mwenyekiti wa Kamati ya maadili na
haki za binadamu kwa jamii nje na ndani ya madhehebu ya dini, Mchungaji
wa Kanisa la Kiinjili la Kipentekoste, William Mwamalanga, alitoa
taarifa hizo.
Alieleza kuwa wabunge hao (majina yanahifadhiwa) ni wa viti maalum kutoka mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam na Mara.
Alisema mbali ya wabunge wamo viongozi wa dini na mfanyabiashara maarufu ambaye alikuwa akisafirisha mihadarati mkoani Mbeya.
Mchungaji huyo alisema kujisalimisha huko kunatokana na kamati hiyo
mwezi Oktoba mwaka huu kuwataka vinara 61 wakiwemo wabunge hao
kujisalimisha kwa ridhaa zao kwa Rais Jakaya Kikwete kama njia ya kutubu
makosa yao.
Kinyume na hapo kamati hiyo iliweka wazi uamuzi uliofikiwa kuwa ni
kuwapeleka watu hao katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) iliyoko
jijini Hague nchini Uholanzi ili sheria kuchukua mkondo wake.
Mchungaji Mwamalanga alisema kamati ilitoa muda wa miezi miwili ambayo inaisha mwezi huu.
Alisema kutokana na ukaidi huo majina ya watu 56 ya wale ambao
hawajajisalimisha ifikapo Januari 15 mwakani yatakabidhiwa rasmi kwenye
taasisi za kupambana na dawa za kulevya Umoja wa Mataifa ili wafikishwe
ICC.
“Novemba 15, mwaka huu tuliyaingiza majina 61 kwenye mtandao wa
taasisi hizo, baada ya hawa watano kuja kwetu, tulipeleka mrejesho kwa
taasisi hizi kuwa tumewatoa ingawa nao hawakuenda kwa Rais,” alisema na
kuongeza:
“Baada ya kuyaingiza majina haya kwenye taasisi hizi, uchunguzi wa
taasisi hizi ulibaini watu hawa ni kweli wanajihusisha na biashara hii,
sasa tunachofanya hivi sasa ni kuyakabidhi majina ya wale waliokaidi ili
hatua zaidi ziweze kuchuliwa,” alisema.
Alisema kwa sasa kamati ipo katika hatua ya mwisho ya kufanya kazi ya
kukusanya majina ya watu waliofariki kwa dawa za kulevya nchini kama
ushahidi kwenye kesi hiyo.
Alisema majina hayo wanayakusanya kupitia kwenye hospitali na kwa ndugu wa marehemu waliofariki kutokana na dawa ya kulevya.
Alitaja baadhi ya takwimu walizokusanya za vifo vya baadhi ya watu
waliofariki na dawa hizo kwenye mikoa na wilaya kuwa ni Mbeya 38,
Kinondoni 67, Dodoma 19, Tanga 41, Lindi saba.
Mchungaji Mwamalanga alisema baadhi ya takwimu hizo ni za mwaka mmoja na nyingine miaka mitatu iliyopita.
Aliongeza kuwa wanaendelea na zoezi la kukusanya takwimu hizo kwenye maeneo mengine.
Kuhusu wale waliojisalimisha kwao ambao gazeti hili inayo majina yao,
Mchungaji huyo alisema kamati imewawekea ulinzi wa siri wa kuifuatilia
mienendo yao ili kubaini kama wameacha au la kama walivyokiri kwao.
Mchungaji Mwamalanga, alisema moja ya masharti waliyotoa kwa watu hao
watano ni kutoa ushirikiano utakaowezesha kukamatwa wale wanaoendelea
na kuingiza au kusafirisha nje ya nchi dawa hizo.
Alisema tayari watu hao wameshatoa ushirikiano na kuwezesha kukamatwa
watu kadhaa waliokuwa wakisafirisha dawa hizo kwenda nchi nyingine
duniani.
Alisema watu hao waliwatajia mbinu ambazo hutumika kusafirisha dawa
hizo kuwa ni baadhi wamekuwa wakizihifadhi kwenye ‘uume bandia’ na
kwenye midoli.
“ Walitueleza kuwa baadhi ya nchi za Afrika Mashariki na zile za
Maziwa Makuu, wafanyabiashara wamebadilisha mbinu za usambazaji wa dawa
hizi ambapo njia hizo ndizo hutumika, ukimuona mwanamke kabeba mdoli
wengine huwa wamebeba dawa hizi,” alisema.
Pia alisema watu hao waliwaeleza mbinu nyingine ni dawa kusafirishwa
kupitia kwa baadhi ya wafadhili wanaoshughulika na mambo ya afya.
Mchungaji Mwamalanga amewaasa vinara hao kuzitumia sikukuu za mwisho
wa mwaka huu kujisalimisha wenyewe ili ifikapo mwakani taifa liache
kuzungumzia suala hilo.
“Tunawaomba wajisalimishe wenyewe, wanadhani sisi tunafanya mzaa
lakini tunawaambia kuwa, watekeleze yale tuliyowataka,” alisema.
Mkutano ambao uliibuka na maamuzi ya kuwafikisha vinara hao ICC
ulifanyika siku mbili kuanzia 21 Oktoba mwaka huu na kuhudhuriwa na
viongozi wa dini wa madhehebu ya Kiislam na Kikristo 134 kutoka Bara na
Visiwani.
CHANZO: NIPASHE
Wamejisalimisha kwenye tume ya kidini iliyoundwa baada ya kuambiwa
watapelekwa ICC The Hague. Hawajatajwa kwa majina lakini wote ni wabunge
wa viti maalum kutoka CCM mikoa ya Mbeya, Dar es Salaam na Mara.