Maofisa wakuu wa jeshi hilo Mkoa wa
Kipolisi wa Temeke, walikutana jana katika kikao cha kutafuta njia ya
kumpata polisi huyo kwa kile kinachoelezwa kuwa baadhi ya maofisa wakuu
wa jeshi hilo kupakwa matope katika kashfa hiyo.
Akizungumza na mwandishi wetu, Kamanda
wa Mkoa wa kipolisi wa Temeke Engelbert Kiondo, alithibitisha kuwapo kwa
kikao hicho, na kueleza mkutano huo ni mwanzo wa mchakato mzito wa
kuchunguza jambo hilo na kumbaini Ofisa huyo anayetuhumiwa kwa wizi huo.
Alisema kuwapo kwa taarifa ya ofisa wa
polisi kuhusika na kashfa hiyo kubwa, imewafanya kuwa na tahadhari kubwa
katika kazi ya upelelezi, ambapo kwenye kikao hicho waliangalia hatua
mbalimbali za kuzichukua ili kumtia mikononi polisi huyo.
"Tupo kwenye kikao na maofisa mbalimbali
wa polisi kujadili suala hilo, jambo muhimu tunataka kumpata huyo polisi
anayetuhumiwa kuhusika na wizi wa shaba pamoja na watuhumiwa wengine,"
alisema Kamanda Kiondo.
Polisi huyo mwenye cheo cha Mrakibu wa
Polisi anadaiwa kushirikiana na askari mwenzake mwenye cheo cha koplo,
baada ya kutuhumiwa kuonekana wakisindikiza lori lenye shehena hiyo ya
shaba lililoibwa wakati likienda bandarini kwa ajili ya kusafirisha
madini hayo kwenda nchi moja ya Ulaya.
Imeelezwa shaba hiyo ilikuwa ikitokea
nchini Zambia na ilipakiwa kwenye makontena mawili kwenye lori namba T
755 BKZ na tela namba T 117 BMF mali ya kampuni ya Dhadho.
Aidha, shehena hiyo ya shaba ikiwa katika
hali ya vipande 638, ilikamatwa na polisi ikiwa kwenye nyumba moja eneo
la Mtoni Bank Club, huku baadhi ya vipande hivyo vikiwa katika mchakato
wa kuhamishwa kwenda kwa wateja.
Hata hivyo, Kamanda Kiondo aliwataka
wananchi kuwa na subira wakati wanachunguza tukio hilo, kwa kile
alichosema kuna kila dalili watu waliohusika na wizi huo wana mtandao
mkubwa hapa nchini na nje ya nchi.
"Kazi hii ni nzito, watu wanaohusika na
wizi wana mtandao mkubwa kuanzia nchini Zambia hadi hapa nchini,
tunatakiwa kuchunguza kwa makini ili watu wote wajulikane," alisema
Kiondo.
Alisema kwa sasa wanawashikilia watu
watatu wakihusishwa na tukio hilo,na alitaja majina yao kuwa ni
Reginald Fabian Nyamilaga (38), Kassim Yusufu (23) na Dotto Juma Maloda
(20).
DEREVA WA LORI ALIOKOTWA
Kamanda Kiondo alisema katika kitu
kinachotia ugumu kwenye sakata hilo, ni baada ya kugundulika dereva wa
lori hilo Goodluck Makundi hakuwa na nyaraka zinazoweza kumtambua.
Alisema kampuni ya Dhadho ambayo
ilimuajiri, haikuwa na kumbukumbu kama inavyotakiwa katika sheria za
ajira, kitu ambacho ni kigumu kutambua makazi yake na sehemu
alipozaliwa.
Alisema pamoja na udhaifu huo, jeshi hilo linaendelea kumtafuta pamoja na mmliki wa yadi ya magari ilikohifadhiwa shaba hizo.
Jana jioni mwandishi wetu alipompigia
simu Kamanda Kiondo baada ya kuzagaa uvumi kuwa, kigogo huyo (cheo na
jina tunalo) na askari walioshiriki kwenye tukio hilo wanashikiliwa
kituoni hapo, alisema kwa sasa ni mapema kulizungumzia.
Alisema hawezi kuthibitisha hilo kwa
sababu habari wamezisoma kwenye moja ya magazeti nchini
na kwamba wanaendelea kuzifanyia kazi.
No comments:
Post a Comment