Ni baada ya umeme kukatika
Hospitali
ya Sinza Palestina iliyoko Jijini Dar es Salaam, juzi usiku ililazimika
kuwakimbiza haraka kinamama wajawazito kwenda Hospitali ya Mwananyamala
kwa huduma ya upasuaji, baada ya umeme kukatika ghafla huku hospitali
hiyo ikiwa haina jenereta.
Mwandishi wetu alifuatilia kituko hicho
baada ya kupata taarifa kutoka kwa mmoja wa ndugu wa waliolazwa katika
hospitali hiyo kwa ajili ya kujifungua.
Mtoa taarifa huyo ambaye hakutaka jina
lake liandikwe gazetini, alisema juzi katika hospitali hiyo hapakuwa na
umeme hali iliyosababisha mgonjwa wao kutokufanyiwa upasuaji kutokana
na hospitali hiyo kukosa jenereta.
Alisema ameshangazwa na hali hiyo kwa hospitali ya kisasa kama hiyo kukosa jenereta inapotokea suala la dharura kama hilo.
Alisema wakati walipokwenda kumuangalia
mgonjwa wao, walishtuka kujulishwa kuwa amehamishiwa hospitali ya
Mwananyama kwa ajili ya upasuaji baada ya hospitali hiyo kushindwa
kumfanyia kutokana na kukatika kwa umeme.
"Nilivyofika hospitali nikamkuta mume wa
mgonjwa analia kwani alikuwa hajamuona mkewe akidhani atakuwa amefariki.
Na tulipokuwa tunafuatilia tukaambiwa kahamishiwa hospitali ya
Mwananyamala ili akafanyiwe operesheni kwani tatizo la umeme ndilo
limesababisha upasuaji kutokufanyika," alisema.
Alisema kitendo cha kutokuwapo kwa
jenereta katika hospitali hiyo ya Sinza, kunahatarisha afya za kinamama
wajawazito. "Hivi kwa mfano ndio mtu anafanyiwa upasuaji halafu umeme
unakatika ghafla hapo itakuwaje… kwa hiyo watamkimbizia Mwananyamala
wakammalizie? Ni kwanini pasiwepo na jenereta umeme ukikatika kwani hata
wagonjwa wanakuwa katika mazingira magumu," aliuliza.
Akiongea na gazeti hili, Mganga Mkuu wa
Hospitali ya Sinza, Dk. Benedict Luoga, alikiri kuwapo kwa tukio hilo na
kudai kuwa pamoja na kukosa jenereta pia ina uhaba wa watumishi.
Alisema juzi umeme ulikatika eneo lote la Sinza na hadi sasa (jana) haujarudi.
Dk. Luoga alikiri wagonjwa kutoka hospitali hiyo kupewa rufaa kwenda hospitali ya Mwananyamala kwa ajili ya huduma ya upasuaji.
Hata hivyo, alisema hospitali yake haitoi huduma ya upasuaji wakati wa usiku kutokana pia kukabiliwa na uhaba wa watumishi.
Alisema huo ndio utaratibu waliokubaliana
na hospitali ya Mwananyama pale inapohitajika mama anapotakiwa
kujifungua kwa upasuaji.
"Muda wa usiku kuanzia saa 2 huwa
hatufanyi upasuaji kama atatokea mama anatakiwa kujifungua kwa njia ya
operesheni basi tunampeleka Mwananyama na sio kwamba kukosekana kwa
umeme ndio kumetufanya tuwapeleke wagonjwa katika hospitali hiyo,"
alisema.
Dk. Luoga alisema jenereta walilokuwa wakilitumia limeharibika na liko kwenye matengenezo.
Alisema wanahitaji jenereta kubwa ambalo litakuwa linatosheleza mahitaji ya jengo zima ambalo gharama zake ni Sh. mil 80.
Alisema suala hilo limewasilishwa katika
ngazi ya Manispaa ya Kinondoni ili waweze kulifanyia kazi kwani jambo
hilo lipo juu ya uwezo wake.
Mwandishi wetu hakuchoka bali ilimtafuta Mganga Mkuu wa
Manispaa ya Kinondoni, Dk. Gunini Kamba ili aweze kulizungumzia suala
hilo ambapo alisema kuwa tayari tatizo la jenereta ameliwasilisha kwa
Mkurugenzi na kwamba linashughulikiwa.
Dk. Kamba alisema tatizo la uhaba wa
wafanyakazi katika hospitali hiyo imetokana na ongezeko la wagonjwa
kwani awali walikuwa wahudumu wachache na kwamba kwa sasa wanasubiri
kibali cha ajira mpya.
Alisema katika hospitali hiyo inatakiwa kupelekwa jenereta jipya lenye ukubwa wa kukidhi mahitaji .
No comments:
Post a Comment