BINTI
wa miaka 16 amebakwa na watu wasiojulikana hadi akazirai na
wakamtelekeza katika nyumba mbovu akiwa hana nguo. Tukio hilo lilitokea
Aprili 10, mwaka huu, ambapo binti huyo aligundulika asubuhi ya Aprili
11, mwaka huu na akina mama waliokwenda kutafuta maji ambapo walimwona
binti huyo akiwa amezirai. Chanzo
cha habari kilichoomba jina lake kuhifadhiwa kilisema binti huyo ambaye
ni mkazi wa Muheza, alifika Korogwe takriban mwezi mmoja uliopita kwa
lengo la kuishi na dada yake katika Mtaa wa Habitati, aliyefahamika kwa
jina moja la Mariamu.
Baada
ya kufika kwa dada yake, binti huyo alikuwa akilala katika chumba
kimoja na watoto wenzake wa majirani katika nyumba wanayoishi na
alichukua uamuzi wa kuwatoroka wenzake wakati wakiwa wamelala na kwenda
mitaani alikokumbwa na mkasa huo.
Chanzo hicho kilisema binti huyo aligundulika kutokuwapo katika chumba
alichokuwa amelala na wenzake saa nane usiku wa kuamkia Aprili 11, mwaka
huu, ambapo hata dada yake alipowauliza wenzake asubuhi walimjibu
hawafahamu alikokwenda.
“Wakati wenzake wakiwa wamelala ndipo alipotoka na hakuoenekana na dada
yake alimuulizia asubuhi akitaka aamshwe akidhani amelala, akajibiwa
hajulikani alipo na ndipo baadaye zikapatikana taarifa kuwa kuna binti
ameonekana Mtaa wa Roma Kanisani,” kilisema chanzo hicho.
Habari zaidi zinasema kijana aliyekuwa na binti huyo usiku huo kabla ya
kufanyiwa kitendo hicho amedai kumulikwa na tochi yenye mwanga mkali
usoni, kisha akakabwa shingo na watu wanaodhaniwa kumbaka binti huyo kwa
vile yeye alidai kufanikiwa kukimbia katika sakata hilo.
Mwandishi wa MTANZANIA alifika Hospitali ya Magunga Korogwe na
kufanikiwa kumkuta binti huyo akiwa amelazwa kitanda namba 10 katika
wodi ya wanawake mchanganyiko akiendelea kupatiwa matibabu huku akiwa na
mama yake mzazi, Mwanaharusi Hassan (38).
Naye mama mzazi wa binti huyo, alisema mwanaye tangu kufikishwa
hospitalini hapo amekuwa akipatiwa matibabu yenye kuridhisha, tofauti na
habari zilizozagaa mitaani kwamba hasaidiwi.
Kwa upande wake, Mganga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dk. Rashid Said, alisema
tangu binti huyo afikishwe hospitalini hapo amepatiwa tiba stahili,
huku vipimo vikiwa vimechukuliwa na majibu kupatikana ambapo hakuweza
kukutwa na mbegu za kiume pindi alipopimwa.
“Vipimo vya maabara vinaonyesha kwamba mgonjwa hakukutwa na mbegu za
kiume, sisi kazi yetu hapa tutaandika taarifa zetu na kuzijaza katika
fomu namba tatu ya polisi na kuziwasilisha kwa wenzetu wa polisi kwa
hatua zaidi kwa kuwa wao wanaweza kujua kama amebakwa,” alisema Dk.
Said.
Naye, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Constantine Massawe,
alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na wanaendelea na uchunguzi wa
kuwabaini waliohusika na tukio hilo.
chanzo - mtanzania