Search in This Blog

MBUNGE ADAI ETI UDOM YAENDESHWA KIDINI, AJIBIWA NA MBUNGE MWENZAKE HAPOHAPO

MBUNGE wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema) amewasilisha bungeni CD za video zenye ushahidi wa namna baadhi ya taasisi za kiserikali nchini zinavyokumbatia na kuchochea suala la udini kikiwemo Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).

Selasini alisema CD hizo mbili zina ushahidi wa namna polisi wanavyoshindwa kuwakamata baadhi ya watu ambao wanazungumza kwa uwazi kuwa ukiona mtu wa dini fulani chinja jambo ambalo alisema ni hatari kwa ustawi wa amani nchini.

Kuhusu Chuo Kikuu cha Dodoma, Selasini alisema CD hiyo inaonesha chuo hicho kinavyoendeshwa kidini kwani wanaonekana baadhi ya wahadhiri wakiwa wamewakusanya wanafunzi wa dini moja na kuwalisha maneno ya chuki dhidi ya wanafunzi wa dini nyingine.

“Baada ya wanafunzi hao kulishwa maneno ya chuki na wahadhiri hao wa dini fulani, wakahoji huko vyumbani tunakaa na wanafunzi wa vyuo vingine tuwafanyeje?

Lakini licha ya kuwepo ushahidi wa mikanda hiyo, Selasini alisema hakuna mtu ambaye ameshakamatwa kutoka katika taasisi hiyo ya Serikali inayoongozwa na Mkuu wa Chuo, Benjamin Mkapa na Makamu wake ni Profesa Idris Kikula.

Mbunge huyo pia alisema jijini Dar es Salaam katika baadhi ya shule kuna walimu wa dini moja wanawachukua wanafunzi wa dini yao na kwenda kuwafundisha na viongozi wanaohusika na kulinda amani ya nchi wamekaa kimya.

“Tusiwe wanafiki wa kukemea udini kwa nje wakati ndani ya mioyo yetu kuna chuki kubwa dhidi ya watu wa dini nyingine,” alisema Selasini.

Alitoa mfano kuwa katika Jiji la Dar es Salaam ipo mikanda imesambazwa mitaani na watu wa dini moja ambayo inawataka waumini wake kuwaua viongozi na waumini wa dini nyingine na polisi haijachukua hatua yoyote.

“Wako wapi polisi wetu wanaosifiwa, kwa nini wameshindwa kuchukua hatua dhidi ya mikanda hii inayouzwa kama njugu pale Dar es Salaam?Alihoji mbunge huyo. Mbunge huyo alieleza kusitikishwa na taifa hili kuacha misingi aliyoiacha mwasisi wa taifa letu Mwalimu Julius Nyerere ambaye katika kipindi chake hakukuwa na suala la udini kutokana na watu kuoleana na kuishi pamoja kama ndugu. Baada ya kutoa hoja hiyo, Mbunge wa Kondoa Kusini Juma Nkamia (CCM) alidai chuo kikuu cha Dodoma kimetulia na hayo mambo yanayosemwa na Selasini hayapo.

“Nadhani tatizo la pale UDOM ni Profesa Kikula na Profesa Mlacha (Shaban ) wanahukumiwa kwa dini zao, leo hii kungekuwa na Lyimo pale haya yasingezungumzwa humu bungeni,” alisema Nkamia ambaye alidai anasoma hapo kwa sasa. Nkamia alisema yeye akiwa mwanafunzi hapo hajasikia suala la udini .

“Hii mikanda ya mbunge aliyoiwasilisha hapa bungeni ni za mitaani tu zisitiliwe maanani, Udom kwa sasa kumetulia.”
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger