Mripuko mkubwa uliotokea kwenye kiwanda cha mbolea karibu na mji wa Waco
katika jimbo la Texas nchini Marekani, umewajeruhi watu wapatao 200 na
kuuwa wengine ambao bado idadi yao haijatajwa.
Kiwanda cha kutengeneza mbolea kilichojengwa katika mji wa West ulioko
umbali wa kilomita 130 kusini mwa jiji la Dallas kiliripuka na kuwaka
moto saa moja usiku kwa saa ya mahali hapo, na sauti ya mripuko huo
iliweza kisikika kutoka umbali wa km 45.
Akizungumza baadaye usiku, msemaji wa idara ya usalama wa raia katika
jimbo la Texas amethibitisha kuwa watu kadhaa wameuawa katika mripuko
huo, ingawa hakutaja idadi yao. Msemaji huyo ameongeza kuwa itachukua
muda mrefu kabla ya kujua bayana kiwango cha uharibifu uliosababishwa na
mripuko huo.
Vifo vyaripotiwa
Baadhi ya waathiriwa wakipewa msaada wa uokozi
Hata hivyo, mbunge anayewakilisha eneo hilo Bill Flores amesema
kuwa mripuko huo umetokea pale wazima moto walipokuwa wakijaribu kuzima
moto uliokuwa umezuka katika sehemu moja ya kiwanda hicho. Kituo cha
Televisheni cha CNN cha huko Marekani kimewanukuu maafisa wa afya
wakisema kwamba watu wawili walikuwa wamekufa.
Gavana wa jimbo la Texas Rick Perry amesema maafisa wa jimbo lake
wanaifuatilia hali kwa makini. Aidha, gavana huyo ameongeza kuwa ofisi
yake inatoa msaada wa hali na mali kwa mamlaka ya eneo lililoathiriwa,
na kutoa pole kwa wale waliofikwa na maafa.
Kama filamu ya kutisha
Walioshuhudia waliinganisha hali ya mripuko huo na filamu za kutisha
Watu walioshuhudia mripuko huo ukitokea wamesema kwamba ulitoa
sura ya filamu za kutisha. Wengine wameilinganisha hali hiyo na ile ya
wakati wa vita vya Iraq.
Moto uliotokana na mripuko huo umeenea katika mtaa mzima, na miongoni
mwa nyumba zilizoathirika ni makazi ya wazee. Baadhi ya wazee
waliohamishwa kutoka nyumba hiyo walionekana wakipatiwa matibabu katika
kituo cha afya.
Vituo vya matibabu ya dharura vimewekwa karibu, na wakazi wameamriwa
kwenda mbali kwa hofu kwamba moto unaowaka unaweza kusambaza moshi wenye
sumu. Hospitali inayoendeshwa na kanisa la Kibaptisti katika mji wa
Waco imeripoti kupokea majeruhi 66, miongoni mwao wakiwa 38 walio
katika hali mahututi.
Viwango duni
Afisa wa polisi katika mji wa Waco sajenti William Patrick Swanton
amewaambia waandishi wa habari kwamba hana maelezo kamili kuhusu idadi
ya watu wanaofanya kazi katika kiwanda cha mbolea kilichoripuka. Kiwanda
hicho kilitajwa katika ripoti ya tume ya viwango na mazingira ya jimbo
la Texas mwaka 2006, ambayo ilisema hakitimizi wiwango vya kupewa leseni
ya kufanya kazi.
Uchunguzi wa tume hiyo ulifanywa baada ya kupata malalamiko ya kuwepo
kwa harufu kali ya kemikali ya ammonia katika kiwanda hicho.
CHANZO : http://www.dw.de/idhaa-ya-kiswahili