Search in This Blog

MTU MMOJA AFARIKI DUNIA HUKU WATATU WAKIJERUHIWA AKIWEMO TRAFIKI.

Kaimu kamanda wa polisi mkoani Arusha Ibrahimu Kilongo
*********
Mahmoud Ahmad Arusha
Mtu mmoja amefariki dunia baada ya kuvamiwa na majambazi na kupigwa risasi ya shingoni wakati akiendesha gari kwenye maeneo ya barabara ya Makongoro karibu na ofisi za Auwsa jijini hapa na watu watatu ambao ni wanawake wawili na askari wa kikosi cha usalama barabarani kujeruhiwa katika tukio hilo ambapo hadi sasa hawajatambuliwa majina.
Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 6:30 mchana maeneo hayo wakati majambazi hao waliokuwa kwenye usafiri wa pikipiki kulivamia gari hilo na kupora kiasi kikubwa cha fedha majira ya saa 5 na nusu mchana na kukimbia kusikojulikana.

Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye alikataa kulitaja jina lake gazetini alisema kuwa waliona pikipiki mbili zikilifuta gari aina ya Rav4 jekundu na baada ya kulifikia walimpiga risasi ya shingoni dereva wa gari hilo ambapo walipolifikia kwenye gari hilo walifungua mlango na kumtoa nje huku akitapata kabla ya kukata roho.
Alisema kuwa walipiga simu polisi walipofika hapo tukio lilikuwa limekwisha huku majambazi hao wakiwa wameshakimbia kwa kutumia usafiri wa piki piki mbili huku mmoja ambaye alikuwa kwenye piki piki ya pili akiwafata wenzake mmoja alitumia kishoka kupasua kioo cha gari hilo na kufungua mlango wa gari na kubeba begi lililokuwa na fedha na kutokomea kusiko julikana.
Matukio ya ujambazi wa kutumia silaha mkoani hapa ambayo yalikuwa yamekaa kimya kwa muda mrefu bila kuonekana yameonekana kuanza kujirudia kwa kasi sasa na katika tukio hilo pia askari wa usalama bara barani ambaye alikuwa akifuatilia Tukio hilo alipoanza kuwafuatilia majambazi hao alivunjwa mguu kwa silaha ya moto hali ambayo ilileta taharuki kwa wakazi wa jiji hili kwa muda.
Wakinamama hao waliotambuliwa kuwa ni wafanyabiashara walikuwa wamekodi gari hilo wakati wakizipeleka benki ndipo walikutana na kimbembe hicho cha uporaji wa mchana kweupe na maiti ya dereva huyo ilichukuliwa kupelekwa kwenye chumba cha kuhifadhia maiti cha hospitali ya Mount Meru na askari waliofika kupambana na majambazi hao.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo kaimu kamanda wa polisi mkoani hapa Ibrahimu Kilongo alipotafutwa kwa njia ya simu alisema kuwa bado wanalifuatilia tukio hilo na watatoa taarifa baadae kwa vyombo vya habari
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger