Search in This Blog

NAFASI YA AJIRA KWA WANAVYUO

Dar es Salaam. Benki ya Exim, imetangaza mpango wa kutoa nafasi za ajira zaidi kwa wahitimu kutoka vyuo vikuu mbalimbali nchini, ukiwa ni mpango wa benki hiyo katika kupanua ajira nchini.
Akizungumza katika maonyesho ya vyuo vikuu yaliyofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Exim, Dinesh Arora, alisema vyuo vikuu vina nafasi kubwa ya kuziba pengo la upungufu wa wafanyakazi katika sekta ya kibenki na fedha nchini.
“Baada ya kuanzishwa kwa kituo chetu cha mafunzo kinachojulikana kama Exim Academy, benki yetu sasa imeamua kuwalenga moja kwa moja wahitimu kutoka vyuoni, uzoefu hautakuwa kipingamizi kwa sababu wahitimu hao watapatiwa mafunzo muhimu mara watakapojiunga na benki yetu,” alinena mkurugenzi huyo.
“Nimebahatika kufanya usaili kwa baadhi ya wahitimu leo (jana) na nimeona wengi wana uwezo mkubwa sana. Baada ya zoezi hili kukamilika, tutachagua baadhi yao ili wajiunge na benki,” alisisitiza Arora.
Meneja Mwandamizi wa Tawi la Exim la Clock Tower, Agnes Kaganda, aliwapa changamoto wahitimu hao kuwa makini katika maisha ili kufikia malengo na ndoto zao.
“Katika hii dunia hakuna kisichowezekana, naomba muendelee kufanya kazi yoyote itakayopatikana bila kukata tamaa na usiruhusu mtu kukuvurugia ndoto zako,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Kamati ya Mandalizi ya maonyesho hayo, Wendo Lendo, alisema yametoa fursa kwa wahitimu kujuana na kampuni mbalimbali kubwa.
Alisema maonyesho hayo yamefana sana hasa ikizingatiwa kuwa mfumo wa elimu wa Tanzania hausaidii kuwajengea wahitimu uwezo wa kuajiriwa. Zaidi ya kampuni 20 zilishiriki katika maonyesho ya mwaka huu.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger