Search in This Blog

UFAFANUZI WA Tsh 1,000,000,000 (BILIONI 1) ZA MAZISHI YA VIONGOZI

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi ametoa ufafanuzi kuhusu Sh1 bilioni zilizotengwa kwa ajili ya mazishi ya viongozi wa nchi mwaka huu, akisema ni za kununua eneo ambalo baadhi ya viongozi wa nchi watakuwa wakizikwa.
Lukuvi alisema fedha hizo zimetengwa kwa ajili ya kukunua eneo la hekta 129 zilizopo eneo la Iyumba mkoani Dodoma, ili liwe linatumika kwa mazishi ya viongozi hao kwa mujibu wa Sheria ya Maziko ya mwaka 2006.
“Fedha hizi zitalipwa kama fidia kwa wale watu wa eneo lile, kwani tayari tulikuwa tumeshapanga kufanya hivyo,” alisema Lukuvi na kuongeza:
“Siyo kila kiongozi atazikwa Dodoma, lakini kuna baadhi watakuwa wakizikwa eneo hilo.”
Lukuvi alisema hiyo inaonyesha kuwa nia ya Serikali kuhamia Dodoma iko palepale, ndiyo maana mwenyewe ni Mwenyekiti wa Bodi ya CDA ili kuharakisha mambo yafanyike haraka.
Lukuvi alilazimika kutoa ufafanuzi huo baada ya wabunge kulalamikia Ofisi ya Waziri Mkuu kutenga Sh1 bilioni kwa mazishi ya viongozi wa Serikali, wakati wananchi wanaishi hali duni ya umaskini.
Lukuvi alikuwa anajibu michango ya wabunge, akiwamo Lucy Owenya (Viti Maalumu - Chadema), aliyelalamikia kitendo hicho akieleza kuwa haiwezekani fedha hizo zikatengwa wakati haijulikani viongozi wangapi watakufa kwa mwaka huu.
Miongoni mwa wabunge ambao wamepinga kutengwa kwa fedha hizo ni Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola ambaye alidai fedha hizo ni ulaji kwa baadhi ya watu na kutoa wito kwa wenzake kutopitisha fedha hizo.
Hata hivyo, tangu kupitishwa Sheria ya Maziko ya Viongozi mwaka 2006, hakuna kiongozi ambaye amezikwa Dodoma ambako kunaelezwa kuwa watakuwa wakizikwa. Viongozi wengi huzikwa mikoa wanayotoka.
 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger