Search in This Blog

VITA YA UGAIDI YAPASUA BUNGE


MKURUGENZI wa Ulinzi na Usalama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), anayekabiliwa na kesi ya ugaidi mahakamani, Wilfred Lwakatare, jana alilitikisa Bunge baada ya kuhusishwa katika mjadala.

Lwakatare alijadiliwa wakati wabunge walipokuwa wakichangia hotuba ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha wa 2013/2014.

Aliyeanzisha mjadala huo, ni Mbunge wa Iramba Magharibi, Mwigulu Nchemba (CCM), ambaye alianza kwa kuwatuhumu viongozi wa Chadema, wamekuwa wakipanga kuua watu na wakati huo huo wakitaka wananchi wawape ridhaa ya kuongoza nchi.

Alisema pamoja na viongozi hao kuwa na tabia hiyo, wamekuwa wa kwanza kulalamika juu ya vitendo vyao na kwamba tabia hiyo ni sawa na mchawi ambaye akiroga mtu na kumuua, anakuwa wa kwanza kulia akionyesha uchungu alionao juu ya marehemu.

“Mheshimiwa Spika, kuna jambo ambalo limekuwa likiandikwa na kulalamikiwa na watu, kwamba ugaidi ugaidi. Katika jambo hili nawaomba Watanzania wasikilize kwa makini, kuna jambo lilitokea na jambo hili ni jambo la kigaidi, limeandikwa sana na kwa masikitiko linapotoshwa, yaani watu wanapotosha mpaka mambo yanayohusu maisha ya watu.

“Eti wanasema usalama wa taifa, mara wanasema polisi wanatesa watu, katika hili wala msihangaike na kwenye jambo hili hakuna polisi wala usalama wa taifa. Jambo la mkanda, aliyerekoki huo mkanda yuko tayari kusema kokote, aliyeniletea huo mkanda yuko tayari kusema kokote na mimi niko tayari kwenda kokote hata kama ni mbinguni.

“Chadema walipanga kuteka na kuua na huyu mwandishi walipanga kumuua eti wanadai picha ilitengenezwa, sasa kwa taarifa yenu hata pale alipokuwa anaongea, (akimaanisha Lwakatare), aliandika hata ile karatasi ninayo, ni hii hapa, fingerprint ni ya kwake, mwandiko ni wa kwake na vyote alivyokuwa anafanyia kazi vimepatikana na alisema atatoa ushahidi na mimi niko tayari kutoa ushahidi kokote iwe ni hapa na hata mbinguni nitakwenda,” alisema Mwigulu akionyesha karatasi hiyo na kuongeza.

“Eti Mbowe (Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe), anasema anayewasiliana na gaidi eti naye aunganishwe na ugaidi, hebu fikirieni, yule aliyekuwa akipanga njama ni Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, kama ni viongozi, amewasiliana na viongozi gani kama siyo wakubwa zake ambao wamemwagiza kufanya hayo tena?

“Jitihada zinazoonyeshwa ambazo ni za kumtetea mtu hata kabla hajafika mahakamani, inadhihirisha ule ulikuwa ni mpango wa chama.

“Kwa kauli hii, ambayo ameandika kiongozi wa upinzani, viongozi wanaowasiliana nao waunganishwe katika kesi ya ugaidi kuanzia leo wakamatwe na polisi, hapa simuoni kiongozi wa Kambi ya Upinzani, labda wameshamkamata,” alisema Mwigulu.

Katika mazungumzo yake, Mwigulu ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa CCM, alitaka Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Wilbrod Slaa, akamatwe kwa kuwa alihusika kumtetea Lwakatare.

Kwa mujibu wa Mwigulu, aliyekuwa akipanga njama za ugaidi huo ni mwanachama wa Chadema na kwamba fedha zilizotumika katika kufanikisha mpango huo, ni za chama hicho.

“Mnasubiri nini polisi, mtu ameshaomba kuunganishwa mwenyewe katika kesi?”

“Mkishapanga maovu mnawahi kwenda kutetea kama vile mchawi ambaye akishaua, anawahi kwenda kulia na kugalagala msibani. Mimi kwenye hili suala la mauaji, nawaomba Chadema mfanye vitu viwili, kwanza kimbieni haraka zaidi kwenye makanisa ama misikiti mliyokaribu nayo ili mkatubu kuwa mmepanga kuwauwa watu wasio na hatia.

“Baada ya kuomba toba, mrudi kutubu kwa wananchi, yaani mnataka uongozi halafu unawaza kuuwa watu, look at you,” alisema.

Wakati akiendelea kusema, Mbunge wa Mbulu, Mustafa Akunay (CHADEMA), aliomba utaratibu na kumlalamikia Mwigulu, kwamba anazungumzia masuala ya Lwakatare wakati akijua yako mahakamani.

Alipomaliza kusema hayo, Spika wa Bunge, Anne Makinda, alikubaliana naye na kuwataka wabunge waheshimu kanuni za Bunge. Hata hivyo hoja hiyo Mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Pauline Gekul alisimama na kuomba mwongozo kwa kutumia Kanuni ya 68 (7).

Alipokuwa akizungumza, alionyesha kutoridhishwa na maelezo ya Spika kwa kuhoji kama wabunge wanatakiwa kufuata kanuni kwa nini Mwigulu alipokuwa akizungumzia masuala yaliyo mahakamani hakuzuiwa na badala yake aliachwa na kuendelea kusema hadi mwisho.

Hoja hiyo, ilimfanya Spika asimame tena na kusema wabunge wanatakiwa kufuata kanuni kwa kuwa hata Mbowe alipokuwa akiwasilisha maoni ya kambi yake juzi kuhusu bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, kuna maneno yasiyofaa aliyasema, lakini akaachwa hadi mwisho.

LISSU AJIBU MAPIGO

Baada ya hatua hiyo, wabunge kadhaa walichangia na ilipofika zamu ya Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), alilazimika kujibu mapigo juu ya tuhuma za Lwakatare.

Lissu alianza kwa kulitumia Gazeti Dada la MTANZANIA la The African la wiki hii, ambalo alisema lilichapisha ripoti inayoonyesha jinsi Jeshi la Polisi linavyoongoza kwa kuwabambikia watu kesi.

“Makosa hayo kisheria hayana dhamana na ni pamoja na yale ya mauaji na ugaidi, kwa hiyo, Jeshi la Polisi linahitaji kusafishwa.

“Huo ni utamaduni wa kihalifu, kwani pia kuna watu kwa kushirikiana na polisi, wanapigiana simu na kulipana fedha, halafu wanakuja kufungua kesi za ugaidi.

“Kuna mtu amewasiliana na hao watu wanaoitwa magaidi, amepigiana nao simu kuliko alivyompigia mke wake, halafu leo anasema huyu aliyekuwa akipigiana naye simu ni gaidi.

“Mtu huyu, amemlipa huyu mtu anayeitwa gaidi baada ya kufanya ugaidi, leo anasimama na kusema huyo ni gaidi. Sheria ya ugaidi inasema kuwa, anayelipa fedha za kufanya ugaidi ni gaidi, sasa tunataka akamatwe na kufungwa.

“Siku ambayo mkutano wa kigaidi unafanyika, mheshimiwa huyu amezungumza na huyo mmoja wa magaidi na wiki mbili baadaye akamtumia fedha, huyu ni gaidi, naye anatakiwa akamatwe kwa sababu ugaidi ni mambo ya kutunga ya Jeshi la Polisi na baadhi ya watu walioko humu ndani na kama wanafikiri hakuna ushahidi, watashangaa,” alisema Lissu.

ANNA ABDALLAH AINGILIA KATI

Lissu alipokuwa akitaka kuendelea, alikatishwa na Mbunge wa Viti Maalum, Anna Abdallah (CCM), ambaye aliomba utaratibu kwa kutumia Kanuni ya 64 ambayo inaeleza kuwa mbunge hatatoa ndani ya Bunge taarifa zisizo za ukweli.

Katika maelezo yake, Anna alimtaka Lissu atoe uthibitisho wa madai ya baadhi ya wabunge kutoa fedha kwa ajili ya kufadhili mpango huo wa ugaidi.

SPIKA AINGILIA KATI

Alipomaliza kuzungumza, Spika Makinda ambaye alikuwa na kazi ya kuwatuliza wabunge, alisimama tena na kusema kuna haja Kamati ya Kanuni ikutane, kwani mambo yanayozungumzwa bungeni yako mahakamani.

“Hizo kesi mnazozungumzia zote zipo mahakamani, jana kiongozi wenu wa upinzani sikutaka kuingilia hotuba yake na wengine wote walinyamaza kimya, jamani katika dunia kila mtu ana haki ya kujibu.

“Mimi nina ripoti nzima hapa, mtajitetea nini, na mimi niliwaheshimu, nililinda heshima kwa sababu ni Kiongozi wa Upinzani ni kiongozi wenu, fuateni kanuni,” alisema Spika.

LISSU AENDELEA TENA

Spika alipomaliza kusema hayo, Lissu aliendelea na kusema hakuna chochote alichosema kuhusiana na kesi iliyoko mahakamani, kwa kuwa alikuwa akitoa ufafanuzi wa mambo yanayofanywa kati ya polisi na washirika wao walioko ndani ya Bunge.

“Ushahidi upo, kama mheshimiwa Anna Abdallah anautaka upo, mawasiliano yaliyofanyika tarehe 28 Desemba mwaka jana, yapo na yanahusu upande wa magaidi na mashahidi zake waliopo humu ndani,” alisema Lissu.


Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Lwakatare

No comments:

Post a Comment

 
Support : KARIBU TENA MDADISI MAM
Copyright © 2011. RISASI - Haki Zote Zimehifadhiwa.
KWA HISANI YA MDADISI MAMBO
Proudly powered by Blogger