MASHIRIKA yanayoshughulikia haki za zeruzeru humu nchini yamewataka watu wanaoishi na hali hiyo kususia shughuli ya kuwahesabu kwa madai kuwa maandalizi ya zoezi hilo yalifanywa kiholela bila wao kushirikishwa.
Mashirika ambayo yanajumuhisha
Chama cha Maalbino nchini (ASK) na Mtandao wa kuwawezesha Maalbino
(AEN), yalishutumu Baraza kuu la kitaifa la Kushughulikia Watu Wanaoishi
na Ulemavu (NCPWD) kwa kuendesha sensa kabla ya kufanya uhamasisho wa
kutosha kupitia vyombo vya habari ili kuwaandaa walengwa huku wakidai
hiyo ilikuwa njama ya baadhi ya watu katika baraza hilo kufuja fedha
zilizotengewa maalbino.
“ NCPWD haiwezi kuendesha zezi la kuwahesabu watu wanaoishi na ulemavu
bila kuwashirikisha washikadau ambao wanafanya kazi kwa karibu na
walengwa wala kuwahamasisha kupitia vyombo vya habari. Hiyo ni njama ya
baadhi ya viongozi ndani ya NCPWD ambao wanapinga kuwekwa kwa hazina ya
watu wenye Ulemavu wa ngozi,” akasema Bw Mwaura Maigua Isaac, ambaye pia
ni mkurugenzi wa kitaifa wa Chama cha watu wanaoishi na ulemavu wa
ngozi nchini (ASK) na mbunge wa kuteuliwa kupitia Chama cha Orange
Democratic movement (ODM).
Akaongezea, “ Kwa hiyo tunawataka wanachama
wetu wasijitokeze kwa ajili ya zoezi hilo tatanishi. Vilevile, tunaitaka
serikali kusimamisha shughuli hiyo hadi hatua mwafaka zifuatwe la sivyo
zoezi hilo halitafua dafu.”
Mafuta
Aidha, mashirika hayo yalishutumu
vigezo vilivyotumika katika utoaji wa kandarasi ya uagizaji wa mafuta ya
losheni ya kuzuia jua kutoka nchi za nje ambapo chupa moja ya losheni
hiyo inagharimu sh 1,500 ilhali chupa ya aina hiyo inauzwa sh700 humu
nchini.
“Tunataka kuionya serikali kuwa
huenda ikapoteza jumla ya sh22 milioni na hivyo kuna haja ya serikali
kuanzisha uchunguzi ili kunusuru nchi kupoteza kiasi hicho kikubwa cha
fedha ndani ya mifuko ya watu,” akasema Bw Isaac.
Mashirika hayo pia yalilitaka bunge
la kitaifa kubuni kifungu cha sheria ambacho kitasaidia kuwalinda watu
wanaoishi na ulemavu wa ngozi.
Zoezi la kuwahesabu watu wenye ulemavu wa ngozi lilianza mnamo Juni 24 na linatarajiwa kumalizika July 5.